< 2 Samweli 21 >

1 Kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu katika siku za utawala wa Daudi, na Daudi akautafuta uso wa Yahwe. “Hivyo Yahwe akasema, “njaa hii ni kwa sababu ya mauaji ya Sauli na familia yake, kwa kuwa aliwauwa Wagibeoni.”
Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”
2 Basi Wagibeoni hawakuwa uzao wa Israeli; walikuwa ni masalia ya Waamori. Watu wa Israeli walikuwa wameapa kutowauwa, lakini Sauli alitaka kuwaangamiza wote kwa husuda kwa ajili ya watu wa Israeli na Yuda.
Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa wa wana wa Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.)
3 Ndipo Daudi alipowaita pamoja Wagibeoni na kuwaambia, “Niwafanyie nini kwa ajili ya upatanisho? Ili kwamba mweze kuwabariki watu wa Yahwe wanaorithi wema na ahadi zake?”
Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi wa Bwana?”
4 Wagibeoni wakamjibu, “Hili siyo jambo la fedha wala dhahabu kati yatu na Sauli au familia yake. Na siyo hitaji letu kumwua mtu yeyote katika Israeli.” Daudi akasema, “Chochote mtakacho omba nitawafanyia.”
Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.” Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
5 Wakamjibu mfalme, “Mtu aliyetaka kutuuwa aliyepanga kunyume chetu, ili kutuangamiza na kukosa eneo katika mipaka ya Israeli -
Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kufanya hila mbaya dhidi yetu ili kwamba tuangamizwe na tusiwe na yeyote katika Israeli,
6 haya na tupewe watu saba kutoka katika uzao wake, nasi tutawatundika mbele ya Yahwe katika Gibea ya Sauli, palipochaguliwa na Yahwe.” Mfalme akasema, “Nitawapeni”
tupatieni wazao wake saba wa kiume tuwaue hadharani mbele za Bwana huko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa na Bwana.” Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”
7 Lakini mfalme akamwifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo cha Yahwe kati ya Daudi na Yonathani mwana wa Sauli.
Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele za Bwana kati ya Daudi na Yonathani.
8 Mfalme akawachukua wana wawili wa Rispa binti Ayia aliomzalia Sauli, hawa wana wawili waliitwa Armoni na Mefiboshethi; na pia Daudi akawachukua wana watano wa Mikali binti Sauli, aliomzalia Adrieli mwana wa Berzilai Mmeholathi.
Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Aiya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi.
9 Akawaweka katika mikono ya Wagibeoni. Nao wakawatundika juu ya mlima mbele za Bwana, na wote saba wakafa pamoja. Waliuawa katika kipindi cha mavuno, katika siku ya kwanza mwanzoni mwa mavuno ya shayiri.
Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele za Bwana. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.
10 Kisha Rispa, binti Aiya, akachukua nguo ya gunia na akajitanda mwenyewe juu ya mlima kando ya miili ya waliokufa tangu mwanzo wa mavuno mpaka wakati mvua ilipoanza kunyesha. Hakuruhusu ndege wa angani kutua juu ya miili mchana wala ayawani wa mwituni wakati wa usiku.
Rispa binti Aiya akachukua nguo ya gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno mpaka mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama wa mwitu wakati wa usiku.
11 Daudi akaambia alichokifanya Rispa, binti Aiya, suria wa Sauli.
Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Aiya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya,
12 Hivyo Daudi akaenda na kuchukua mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe kutoka kwa watu wa Yabeshi Gileadi, waliokuwa wameiiba kutoka katika eneo la jumuiya la Beth Shani, Wafilisti walipokuwa wamewatundika baada ya Wafilisti kumwua Sauli katika Gilboa.
alikwenda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabeshi-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, mahali ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumuua Sauli huko Gilboa.)
13 Daudi akaiondoa pale mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe, na wakakusanya pia mifupa ya wale watu saba waliotundikwa.
Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale waliokuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa.
14 Wakaizika mifupa ya Sauli na Yonathani mwanawe huko Zela katika nchi ya Benjamini, katika kaburi la Kishi babaye. Wakafanya kila alichoagiza mfalme. Ndipo Mungu akajibu maombi yao kwa ajili ya nchi.
Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.
15 Kisha Wafilisti wakaenda tena katika vita na Israeli. Hivyo Daudi na jeshi lake wakashuka na kupigana na Wafilisti. Akiwa vitani Daudi akachoshwa na vita.
Kwa mara nyingine tena kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Israeli. Daudi akashuka pamoja na watu wake ili kupigana dhidi ya Wafilisti, naye akawa amechoka sana.
16 Ishbibenobu, wa uzao wa majitu, ambaye mkuki wake wa shaba ulikuwa na uzito wa shekeli mia tatu na alikuwa na upanga mpya, alitaka kumwua Daudi.
Naye Ishbi-Benobu, mmoja wa wazao wa Warefai, ambaye mkuki wake ulikuwa na uzito wa shekeli 300 za shaba, alikuwa amejifunga upanga mpya, naye alisema angemuua Daudi.
17 Lakini Abishai mwana wa Seruya akamwokoa Daudi, akampiga Mfilisti na kumwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, kusema, “Hautakwenda vitani pamoja nasi tena usije ukaizima taa ya Israeli.”
Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumuua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutakwenda tena nasi vitani, ili kwamba taa ya Israeli isije ikazimwa.”
18 Ikawa baadaye kuwa na vita tena kati ya Wafilisti huko Gobu, wakati Sibekai Mhushathi alipomwua Safu, aliyekuwa miongoni mwa uzao wa Warefai.
Baada ya muda, kukawa na vita nyingine na Wafilisti, huko Gobu. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Safu, mmoja wa wazao wa Warefai.
19 Ikawa tena katika vita na Wafilisti huko Gobu, huyo Elhanani mwana wa Jari Mbethlehemu akamwua Goliathi Mgiti, ambaye fumo la mkuki wake lilikuwa kama mti wa mfumaji.
Katika vita vingine na Wafilisti huko Gobu, Elhanani mwana wa Yaare-Oregimu, Mbethlehemu, alimuua nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.
20 Ikawa katika vita nyingine huko Gathi kulikuwa na mtu mrefu sana mwenye vidole sita katika kila mkono na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne. Yeye naye alikuwa wa uzao wa Warefai.
Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwako na mtu mmoja mkubwa mwenye vidole sita katika kila mkono na vidole sita kila mguu, jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai.
21 Alipowatukana Israeli, Yonathani mwana mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua.
Alipowadhihaki Israeli, Yonathani mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.
22 Hawa walikuwa wa uzao wa Warefai wa Gathi, waliuawa kwa mkono wa Daudi na kwa mkono wa askari wake
Hawa wanne walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.

< 2 Samweli 21 >