< 2 Samweli 19 >

1 Yoabu akaambiwa, “Tazama, mfalme analia na kumwombolea Absalomu.”
Yoabu akaambiwa, “Mfalme analia na kumwombolezea Absalomu.”
2 Hivyo siku ile ushindi uligeuzwa kuwa maombolezo kwa jeshi lote, kwa maana jeshi likasikia ikisemwa siku hiyo, “Mfalme anaomboleza kwa ajili ya mwanaye.”
Kwa jeshi lote, ushindi wa siku ile ukageuka kuwa maombolezo, kwa sababu siku ile vikosi vilisikia ikisemwa, “Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.”
3 Siku ile askari waliingia mjini kwa kunyemelea kimyakimya kama watu waonao haya baada ya kukimbia vitani.
Siku ile watu wakaingia mjini kimya kama vile waingiavyo kwa aibu watu waliokimbia kutoka vitani.
4 Mfalme akafunika uso wake na kulia kwa sauti, “Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwangangu!”
Mfalme akafunika uso wake akalia kwa sauti, akisema, “Ee mwanangu Absalomu! Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
5 Ndipo Yoabu akaingia ndani kwa mfalme na kumwambia, “Leo umeziaibisha nyuso za askari wako, waliookoa maisha yako leo, maisha ya wanao na binti zako, maisha ya wake zako na maisha ya masuria wako,
Kisha Yoabu akaingia ndani ya nyumba ya mfalme na kusema, “Leo umewaaibisha watu wako wote, waliookoa maisha yako, maisha ya wanao na binti zako, maisha ya wake zako na masuria wako.
6 kwa maana wawapenda wakuchukiao na kuwachukia wakupendao. Kwa kuwa leo umeonesha kwamba maakida na askari si chochote kwako. Natambua sasa kwamba kame Absalomu angesalia na sisi sote tungekufa hilo lingekufurahisha.
Unawapenda wale wanaokuchukia, na unawachukia wale wanaokupenda. Leo umeonyesha wazi kwamba majemadari wako na watu wao hawana maana kwako. Naona kwamba ungefurahi kama Absalomu angekuwa hai leo na sisi sote tuwe tumekufa.
7 Sasa basi, inuka na uende kuongea na askari wako kwa upole, kwani nakuapia kwa Yahwe, ikiwa hutakwenda hakuna mtu hata mmoja atakayesalia nawe usiku huu. Na hii itakuwa vibaya sana kwako kuliko madhara yoyote yaliyowai kukupata tangu ujana wako.”
Sasa utoke nje ukawatie moyo watu wako. Naapa kwa Bwana kwamba ikiwa hutatoka nje, hakuna mtu atakayesalia pamoja nawe ifikapo leo jioni. Hii itakuwa mbaya zaidi kwako kuliko maafa yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi sasa.”
8 Hivyo mfalme akainuka na kuketi kati ya lango la mji, watu wote wakaambiwa, “Tazama, mfalme ameketi kati ya lango.” Ndipo watu wote wakaja mbele za mfalme. Walakini, Israeli walikimbia kila mtu nyumbani kwake.
Kwa hiyo mfalme akaondoka akaketi kitini pake penye lango. Watu walipoambiwa, “Mfalme ameketi langoni,” watu wote wakamjia. Wakati huo, Waisraeli walikuwa wamekimbilia nyumbani kwao.
9 Watu wote wakahojiana wao kwa wao katika jamaa zote za Israeli kusema, “Mfalme alituokoa na mkono wa adui zetu. Alitukomboa na mkono wa Wafilisti lakini sasa ameikimbia nchi mbele ya Absalomu.
Katika makabila yote ya Israeli, watu walikuwa wanabishana wao kwa wao, wakisema, “Mfalme alituokoa kutoka mikononi mwa adui zetu; ndiye alituokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa mfalme ameikimbia nchi kwa sababu ya Absalomu,
10 Na Absalomu tuliyemtia mafuta juu yetu amekufa vitani. Hivyo kwa nini hatuongei juu ya kumrudisha mfalme tena?”
naye Absalomu, tuliyemtia mafuta atutawale, amekufa vitani. Basi mbona hamsemi lolote kuhusu kumrudisha mfalme?”
11 Mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na kwa Abiathari makuhani kusema, “Ongeeni na wazee wa Yuda kusema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho kumrudisha mfalme kwenye kasri lake tena, kwa vile usemi wa Israeli wote unamtaka mfalme arudi katika kasri lake?
Mfalme Daudi akapeleka ujumbe huu kwa makuhani Sadoki na Abiathari, kusema: “Waulizeni wazee wa Yuda, ‘Kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme katika jumba lake la kifalme, maadamu kile kinachosemwa katika Israeli yote kimemfikia mfalme katika makao yake?
12 Ninyi ni ndugu zangu, mwili na mifupa yangu. Kwa nini basi mmekuwa wa mwisho kumrudisha mfalme?'
Ninyi ni ndugu zangu, nyama yangu na damu yangu mwenyewe. Kwa hiyo kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme?’
13 Na mwambieni Amasa, 'Je wewe si mwili na mfupa wangu? Mungu anifanyie hivyo na kuzidi pia ikiwa hautakuwa jamadari wa jeshi langu tangu sasa na baadaye mahali pa Yoabu.
Nanyi mwambieni Amasa, ‘Je, wewe si nyama yangu mwenyewe na damu yangu? Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama kuanzia sasa na kuendelea wewe si jemadari wa jeshi langu mahali pa Yoabu.’”
14 Naye akaishinda mioyo ya watu wote wa Yuda kama mtu mmoja, hata wakatuma kwa mfalme kusema, “Rudi sasa na watu wako wote.”
Aliipata mioyo ya watu wote wa Yuda kama vile walikuwa mtu mmoja. Wakapeleka ujumbe kwa mfalme, kusema, “Rudi, wewe na watu wako wote.”
15 Hivyo mfalme akarudi naye akaja Yordani. Na watu wa Yuda wakaja Gilgali kwenda kumlaki mfalme ili kumvusha mfalme juu ya Yordani.
Ndipo mfalme akarudi, akaenda hadi kufikia Mto Yordani. Basi watu wa Yuda walikuwa wamekuja mpaka Gilgali ili kutoka kwenda kumlaki mfalme na kumvusha Mto Yordani.
16 Shimei mwana wa Gera, Mbenjamini, kutoka Bahurimu, akaharakisha kushuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi.
Shimei mwana wa Gera, wa kabila la Benyamini kutoka Bahurimu, akaharakisha kuteremka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki Mfalme Daudi.
17 Kulikuwa na watu elfu moja kutoka Benjamini waliokuwa pamoja naye, na Siba mtumishi wa Sauli na wanawe kumi na watano na watumish wake ishirini walikuwa pamoja naye. Wakavuka Yordani mbele za mfalme.
Pamoja naye walikuwepo Wabenyamini elfu moja wakiwa wamefuatana na Siba, msimamizi wa nyumba ya Sauli, pia wanawe kumi na watano, na watumishi ishirini. Wakaharakisha kwenda Yordani, mahali mfalme alipokuwa.
18 Wakavuka ili kuivusha familia ya mfalme na kumfanyia lolote aliloona jema. Shimei mwana wa Gera akainama chini mbele za mfalme mara alipoanza kuuvuka Yordani.
Wakavuka kivuko ili kuwachukua watu wa nyumbani mwa mfalme ili kuwavusha na kufanya kila kitu alichotaka. Shimei mwana wa Gera alipovuka Yordani, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme,
19 Shimei akamwambia mfalme, “Bwana wangu asinione mwenye hatia au kuyaweka moyoni ambayo mtumishi wake alifanya kwa ukaidi siku bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Tafadhari, mfalme na asiyaweke moyoni.
na kumwambia, “Bwana wangu na asinihesabie hatia. Usikumbuke jinsi mtumishi wako alivyofanya kosa siku ile bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Mfalme aliondoe moyoni mwake.
20 Kwa maana mtumishi wako anatambua kwamba amekosa. Tazama, ndiyo maana nimekuja leo wa kwanza katika nyumba ya Yusufu ili kumlaki bwana wangu mfalme.”
Kwa maana mimi mtumishi wako najua nimefanya dhambi, lakini leo nimekuja hapa kama wa kwanza wa nyumba yote ya Yosefu kushuka na kumlaki bwana wangu mfalme.”
21 Lakini Abishai mwana wa Seruya akajibu na kusema, “Je Shimei asife kwa hili kwa vile alivyomlaani mtiwa mafuta wa Yahweh?”
Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa ajili ya hili? Alimlaani mpakwa mafuta wa Bwana.”
22 Ndipo Daudi akasema, “Nifanye nini nanyi enyi wana wa Seruya, hata leo mkawa adui zangu? Je mtu yeyote atauawa leo katika Israeli? Kwani sijui kama leo mimi ni mfalme juu ya Israeli?
Daudi akajibu, “Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya? Leo hii mmekuwa adui zangu! Je, leo kuna yeyote atakayeuawa katika Israeli? Je, mimi sijui kuwa leo ndimi mfalme katika Israeli yote?”
23 Hivyo mfalme akamwambia Shimei, “Hautakufa.” Mfalme akamwahidi kwa kiapo.
Basi mfalme akamwambia Shimei, “Hutakufa.” Naye mfalme akamwahidi kwa kiapo.
24 Kisha Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka ili kumlaki mfalme. Hakuwa ameivalisha miguu yake wala kunyoa ndevu zake wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka hata siku aliporudi kwa amani.
Pia Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka kwenda kumlaki mfalme. Hakuwa amenawa miguu wala kunyoa ndevu zake wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka siku aliporudi ile salama.
25 Na hivyo alipotoka Yerusalemu ili kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, “Mefiboshethi Kwa nini haukwenda pamoja nami?”
Wakati alipotoka Yerusalemu kuja kumlaki mfalme, mfalme akamuuliza, “Mefiboshethi, kwa nini hukufuatana nami?”
26 Akajibu, “Bwana wangu mfalme mtumishi wangu alinidanganya, kwani nilisema, nitapanda juu ya punda ili niende na mfalme, kwa kuwa mtumishi wako ni mlemavu.'
Akasema, “Bwana wangu mfalme, maadamu mimi mtumishi wako ni kiwete, nilisema, ‘Nitandikiwe punda wangu, nimpande, ili niweze kwenda pamoja na mfalme.’ Lakini Siba mtumishi wangu akanisaliti.
27 Mtumishi wangu Siba amenisemea uongo, mtumishi wako, kwa bwana wangu mfalme. Lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu. Kwa hiyo fanya lililojema machoni pako.
Naye amemchongea mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme. Bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu, kwa hiyo fanya lolote linalokupendeza.
28 Kwa maana nyumba yote ya baba yangu walikuwa maiti mbele ya bwana wangu mfalme, lakini ukamweka mtumishi wako miongoni mwao walao mezani pako. Kwa hiyo nililiye haki gani zaidi kwa mfalme?”
Wazao wote wa baba yangu hawastahili kitu kingine isipokuwa kifo kutoka kwa bwana wangu mfalme, lakini ulimpa mtumishi wako nafasi miongoni mwa wale waliokula mezani pako. Je, ninayo haki gani kumwomba mfalme zaidi ya hayo?”
29 “Kisha mfalme akamwambia, “Kwa nini kueleza yote zaidi? Nimekwisha amua kwamba wewe na Siba mtagawana mashamba.”
Mfalme akamwambia, “Kwa nini useme zaidi? Naamuru wewe na Siba mgawanye mashamba.”
30 Ndipo Mefiboshethi akamjibu mfalme, “Sawa, acha achukue yote kwa vile bwana wangu mfalme amerudi salama nyumbani kwake.”
Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu achukue kila kitu, kwa kuwa sasa bwana wangu mfalme amerudi nyumbani salama.”
31 Kisha Berzilai Mgileadi akashuka kutoka Rogelimu ili avuke Yordani pamoja na mfalme, naye akamsaidia mfalme kuuvuka Yordani.
Barzilai, Mgileadi, pia akashuka kutoka Rogelimu ili kuvuka Yordani pamoja na mfalme na kumsindikiza kutoka huko.
32 Basi Berzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amemsaidia mfalme kwa mahitaji alipokuwako Mahanaimu kwani alikuwa na mali nyingi.
Basi Barzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amempatia mfalme mahitaji wakati alipokuwa anaishi huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa mtu tajiri sana.
33 Mfalme akamwambia Berzilai, njoo pamoja nami, nami nitaandaa kwa ajili yako huko Yerusalemu.”
Mfalme akamwambia Barzilai, “Vuka pamoja nami na ukae nami huko Yerusalemu, nami nitakupatia mahitaji yako.”
34 Berzilai akamjibu mfalme, “Kwani kuna siku ngapi zilizosalia maishani mwangu, hata niende na mfalme huko Yerusalemu?
Lakini Barzilai akamjibu mfalme, “Je, nitaishi miaka mingine mingapi, hata nipande kwenda Yerusalemu pamoja na mfalme?
35 Nina umri wa miaka themanini. Je naweza kutofautisha mema na mabaya? Je mtumishi wako anaweza kuonja ninachokula au kunywa? Je naweza kusikia sauti zaidi za wanaume na wanawake waimbao? Kwa nini basi mtumishi wako awe mzigo kwa bwana wangu mfalme?
Sasa nina miaka themanini. Je, naweza kutofautisha kati ya lililo jema na lililo baya? Je, mtumishi wako anaweza kujua ladha ya kile anachokula au anachokunywa? Je, bado naweza kusikiliza sauti za waimbaji wa kiume na za wanawake? Kwa nini mtumishi wako aongeze mzigo kwa bwana wangu mfalme?
36 Mtumishi wako angependa tu kuvuka Yordani pamoja na mfalme. Kwa nini mfalme anilipe kwa thawabu kama hiyo?
Mtumishi wako atavuka Yordani pamoja na mfalme kwa umbali mfupi tu, lakini kwa nini mfalme anizawadie kwa namna hii?
37 Tafadhari mruhusu mtumishi wako arudi nyumbani, ili kwamba nife katika mji wangu katika kaburi la baba na mama yangu. Lakini tazama, huyu hapa mtumishi wako Kimhamu. Haya yeye na avuke na bwana wangu mfalme na umfanyie lolote lipendezalo kwako.”
Mruhusu mtumishi wako arudi, ili mimi nikafie katika mji wangu mwenyewe karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini yupo hapa mtumishi wako Kimhamu. Mruhusu avuke pamoja na bwana wangu mfalme. Mtendee lolote linalokupendeza.”
38 Mfalme akajibu, “Kimhamu atakwenda pamoja nami, nami nitamtendea kila lionekanalo jema kwako, na lolote unalotamani kutoka kwangu nitakutendea.”
Mfalme akamwambia Barzilai, “Kimhamu atavuka Yordani pamoja nami, nami nitamtendea lolote litakalokupendeza. Nawe kitu chochote unachotaka kutoka kwangu nitakutendea.”
39 Kisha watu wote wakavuka Yordani, mfalme naye akavuka, kisha mfalme akambusu Berzilai na kumbariki. Kisha Berzilai akarudi nyumbani kwake.
Kwa hiyo watu wote wakavuka Yordani, kisha mfalme akavuka. Mfalme akambusu Barzilai na kumbariki; Barzilai akarudi nyumbani kwake.
40 Hivyo mfalme akavuka kuelekea Gilgali, na Kimhamu akavuka pamoja naye. Jeshi la Yuda lote na nusu ya jeshi la Israeli likamleta mfalme.
Mfalme alipovuka kwenda Gilgali, Kimhamu akavuka pamoja naye. Vikosi vyote vya Yuda na nusu ya vikosi vya Israeli vilimvusha mfalme.
41 Mara watu wa Israeli wote wakaanza kuja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda, wamemwiba na kumleta mfalme na familia yake juu ya Yordani na watu wote wa Daudi pamoja naye?
Baada ya kitambo kidogo watu wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda, wamemrudisha mfalme kwa siri bila kutushirikisha, na kumvusha ngʼambo ya Yordani, yeye na nyumba yake, pamoja na watu wake wote?”
42 Hivyo watu wa Yuda wakawajibu watu wa Israeli, “Ni kwa kuwa mfalme anahusiana nasi kwa karibu zaidi. Kwa nini basi mkasirike juu ya hili? Je sisi tumekula chochote ambacho mfalme amekitoa? Je ametupa zawadi yoyote?
Watu wote wa Yuda wakawajibu watu wa Israeli, “Tulifanya hivi kwa sababu mfalme ni jamaa yetu wa karibu. Kwa nini mnakasirikia jambo hili? Je, tumekula kitu chochote cha mfalme? Je, tumejichukulia kitu chochote kwa ajili yetu wenyewe?”
43 Watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, Sisi tuna kabila kumi zaidi kwa mfalme hivyo tuna sehemu kubwa zaidi kwa Daudi kuliko ninyi. Kwa nini basi mlitudharau? Je hatukuwa wa kwanza kupendekeza kumrudisha mfalme wetu? Lakini maneno ya watu wa Yuda hata yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.
Ndipo watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, “Tunayo haki mara kumi kwa mfalme; sisi tunahusika zaidi na Daudi kuliko ninyi. Kwa nini basi mnatudharau? Je, hatukuwa wa kwanza kuzungumza kuhusu kumrudisha mfalme nyumbani?” Lakini watu wa Yuda wakajibu kwa ukali hata zaidi kuliko watu wa Israeli.

< 2 Samweli 19 >