< 2 Samweli 18 >

1 Daudi akawahesabu askari waliokuwa pamoja naye na akaweka akida wa elfu na akida wa mia juu yao.
Daudi akakusanya watu aliokuwa nao na kuweka majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia.
2 Kisha Daudi akalipeleka jeshi, thelusi moja chini ya Yoabu, thelusi nyingine chini ya Abishai mwana wa Seruya, ndugu wa Yoabu, na thelusi nyingine tena chini ya Itai Mgiti. Mfalme akaliambia jeshi, “kwa hakika mimi mwenyewe pia nitakwenda pamoja nanyi.
Daudi akatuma vikosi vya askari: theluthi moja ilikuwa chini ya amri ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Mfalme akaviambia vikosi, “Hakika mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nanyi.”
3 Lakini watu wakasema, “Wewe usiende vitani, kwani ikiwa tutakimbia hawatatujari sisi, ama nusu yetu wakifa hawatajari. Lakini wewe ni zaidi ya elfu kumi yetu sisi! Kwa hiyo ni afadhari zaidi ukitusaidia ukiwa mjini.”
Lakini watu wakasema, “Haikupasi kwenda, ikiwa sisi tutalazimika kukimbia, wao hawatatujali. Hata kama nusu yetu tukifa hawatajali, lakini wewe una thamani ya watu kama sisi kumi elfu. Ingekuwa bora zaidi kwako basi kutupatia msaada kutoka mjini.”
4 Hivyo mfalme akawajibu, “Nitafanya lolote lionekanalo jema machoni penu.” Mfalme akasimama kati ya lango la mji wakati jeshi lilipoondoka katika mamia na katika maelfu.
Mfalme akajibu, “Nitafanya lolote linaloonekana jema zaidi kwenu.” Kwa hiyo mfalme akasimama kando ya lango wakati watu wote wakitoka nje kwa makundi ya mamia na maelfu.
5 Mfalme akawaagiza Yoabu, Abishai, na Itai kusema, “Mmtendee huyo kijana, Absalomu, kwa upole kwa ajili yangu.” Watu wote wakasikia jinsi mfalme alivyowaagiza maakida kuhusu Absalomu.
Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kuweni wapole kwa kijana Absalomu kwa ajili yangu.” Vikosi vyote vikasikia mfalme akitoa amri kwa kila jemadari kumhusu Absalomu.
6 Hivyo jeshi likaenda nyikani dhidi ya Israeli; vita ikaenea katika msitu wa Efraimu.
Jeshi likatoka kwenda kwenye uwanja wa vita kupigana na Israeli, hivyo vita vikapiganwa katika msitu wa Efraimu.
7 Jeshi la Israeli likashindwa mbele ya askari wa Daudi; kulikuwa na machinjo makuu kwa watu elfu ishirini siku hiyo.
Huko jeshi la Israeli likashindwa na watu wa Daudi, siku hiyo majeruhi walikuwa wengi kiasi cha watu ishirini elfu.
8 Vita ikaenea katika eneo lote na watu wengi wakaangamizwa na msitu kuliko upanga.
Vita vikaenea nchi nzima, watu wengi zaidi wakifia msituni siku hiyo kuliko waliouawa kwa upanga.
9 Ikatukia kwamba Absalomu akakutana na askari wa Daudi. Absalomu alikuwa amepanda juu ya nyumbu wake na nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mti wa mwaloni, na kichwa chake kikanaswa katika matawi ya mti. Akaachwa akining'inia kati ya nchi na anga wakati nyumbu alipoendelea mbele.
Basi ikawa Absalomu alikutana na watu wa Daudi. Yeye alikuwa amepanda nyumbu wake, naye nyumbu alipopita chini ya matawi yaliyosongana ya mwaloni mkubwa, kichwa cha Absalomu kilinaswa kwenye mti. Akaachwa akiningʼinia hewani, wakati nyumbu aliyekuwa amempanda aliendelea kwenda.
10 Mtu mmoja akaona lililotukia na akamwambia Yoabu, “Tazama, nilimwona Absalomu akining'inia katika mwaloni!”
Mmojawapo wa wale watu alipoona, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akiningʼinia kwenye mti wa mwaloni.”
11 Yoabu akamwambia aliyemwambia kuhusu Absalomu, “Tazama! Ulimwona! Kwa nini haukumpiga hata chini. Ningekupa shekeli kumi za fedha na mkanda.”
Yoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo mpaka chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi za fedha na mkanda wa askari shujaa.”
12 Yule mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepewa shekeli elfu za fedha hata hivyo nisingeinua mkono wangu juu ya mwana wa mfalme, kwa maana sisi sote tulimsikia mfalme akiwaagiza wewe, Abishai na Itai kusema, mtu asimguse huyo kijana Absalomu.'
Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000 mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’
13 Ikiwa ningehatarisha maisha yangu kwa uongo(na hakuna jambo linalofichika kwa mfalme), ungejitenga nami.”
Nami kama ningekuwa nimemtendea kwa hila, na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme, wewe mwenyewe ungejitenga nami.”
14 Ndipo Yoabu aliposema, “sitakusubiri.” Kisha akachukua mishale mitatu mkononi mwake na akairusha katika moyo wa Absalomu wakati yu ngali hai na amening'inia katika mwaloni.
Yoabu akasema, “Mimi sitapoteza muda hapa pamoja nawe.” Hivyo akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu nayo moyoni alipokuwa angali hai akiningʼinia katika ule mwaloni.
15 Kisha vijana kumi waliochukua slaha za Yoabu wakamzunguka Absalomu, wakampiga na kumwua.
Nao wabeba silaha kumi wa Yoabu wakamzunguka Absalomu, wakampiga na kumuua.
16 Kisha Yoabu akapiga tarumbeta na jeshi likarudi kutoka kuwafuatia Israeli, hivyo Yoabu akalirudisha jeshi.
Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, navyo vikosi vikaacha kuwafuata Israeli, kwa maana Yoabu aliwasimamisha.
17 Wakamchukua Absalomu na kumtupa katika shimo kubwa msituni; wakaufukia mwili wake chini ya rundo kubwa la mawe, wakati Israeli wote walipokimbia kila mtu nyumbani kwake.
Wakamchukua Absalomu, wakamtupa katika shimo kubwa huko msituni na kulundika lundo kubwa la mawe juu yake. Huko nyuma, Waisraeli wote wakakimbilia nyumbani kwao.
18 Wakati Absalomu alipokuwa yu ngali hai alijijengea nguzo kubwa ya jiwe katika Bonde la Mfalme, kwani alisema, “Sina mwana wa kuchukua kumbukumbu ya jina langu.” Akaiita nguzo kwa jina lake, hivyo inaitwa Mnara wa Absalomu hata leo.
Wakati wa uhai wa Absalomu alikuwa amechukua nguzo na kuisimamisha katika Bonde la Mfalme, kwa maana alifikiri, “Sina mwana atakayeendeleza kumbukumbu ya jina langu.” Akaita nguzo hiyo kwa jina lake mwenyewe. Nayo inaitwa Mnara wa Ukumbusho wa Absalomu mpaka leo.
19 Kisha Ahimaasi mwana wa Sadoki akasema, “Niruhusu niende kwa mfalme na habari njema, jinsi Yahwe alivyomwokoa kutoka mkono wa adui zake.”
Basi Ahimaasi mwana wa Sadoki akasema, “Niruhusu mimi nikimbie na kumpelekea mfalme habari kwamba Bwana amemwokoa mfalme kutoka mikononi mwa adui zake.”
20 Yoabu akamjibu, “Wewe hautakuwa mchukua habari leo; utafanya hivyo siku nyingine. Leo hautachukua habari yoyote kwa maana mwana wa mfalme ameuawa.”
Yoabu akamwambia Ahimaasi, “Leo si wewe utakayepeleka habari. Unaweza kupeleka habari wakati mwingine, lakini leo haikupasi kupeleka, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.”
21 Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi, “Nenda umwambia mfalme ulichokiona.” Mkushi akamwinamia Yoabu, na kisha akakimbia.
Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja Mkushi, “Nenda, ukamwambie mfalme kile ulichoona.” Mkushi akasujudu mbele ya Yoabu akaondoka mbio.
22 Kisha tena, Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia Yoabu, “Pamoja na yote yanayoweza kutokea, tafadhari niruhusu nami pia niende nimfuate Mkushi.” Yoabu akajibu, “Mwanangu kwa nini unataka kwenda, hautapata thawabu yoyote kwa ajili ya habari hii?”
Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia tena Yoabu, “Liwalo na liwe, tafadhali niruhusu nikimbie nyuma ya huyo Mkushi.” Lakini Yoabu akajibu, “Mwanangu, mbona wataka kwenda? Wewe huna habari yoyote itakayokupa tuzo.”
23 “Vyovyote itakavyokuwa niache niende,” Ahimaasi alijibu. Hivyo Yoabu akamjibu, “Nenda.” Ndipo Ahimaasi akakimbia kwa njia ya tambarare na akampita Mkushi.
Ahimaasi akasema, “Liwalo na liwe, nataka kukimbia.” Kwa hiyo Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia!” Ndipo Ahimaasi akakimbia kufuata njia ya kupitia tambarare, akafika kabla ya huyo Mkushi.
24 Basi Daudi alikuwa amekaa kati ya lango la ndani na lango la nje. Na mlinzi alikuwa juu ya lango ukutani naye akainua macho yake. Alipokuwa akiangalia, akamwona mtu anakaribia huku akikimbia peke yake.
Wakati Daudi alipokuwa ameketi kati ya lango la ndani na la nje, mlinzi akapanda juu ya paa la lango kupitia ukutani. Alipotazama nje, akaona mtu mmoja akikimbia peke yake.
25 Mlinzi akaita kwa sauti na kumwambia mfalme. Ndipo mfalme akasema, “Ikiwa yupo peke yake ana habari katika kinywa chake.” Mkimbiaji akasogea na kuukaribia mji.
Mlinzi akampazia mfalme sauti na kumpa taarifa. Mfalme akasema, “Ikiwa yuko peke yake, lazima atakuwa na habari njema.” Naye yule mtu akazidi kusogea karibu.
26 Kisha mlinzi akaona mtu mwingine aliyekuwa anakimbia, naye akamwambia bawabu; kusema, “Tazama, kuna mtu mwingine anakimbia peke yake.” Mfalme akasema, “Yeye pia analeta habari.”
Kisha mlinzi akaona mtu mwingine anakuja akikimbia, akamwita bawabu, “Tazama, mtu mwingine anakuja akikimbia peke yake!” Mfalme akasema, “Lazima atakuwa analeta habari njema pia.”
27 Ndipo mlinzi akasema, Nadhani kukimbia kwake mtu aliye mbele ni kama kukimbia kwake Ahimaasi mwana wa Sadoki.” Mfalme akasema, “Yeye ni mtu mwema naye anakuja na habari njema.”
Mlinzi akasema, “Ninaona kuwa yule wa kwanza anakimbia kama Ahimaasi mwana wa Sadoki.” Mfalme akasema, “Yeye ni mtu mwema. Analeta habari njema.”
28 Ndipo Ahimaasi akaita na kumwambia mfalme, “Yote ni mema.” Kisha akainama yeye mwenyewe uso wake chini mbele ya mfalme na kusema, Atukuzwe Yahwe Mungu wako, aliyewatoa watu walioinua mkono wao kinyume cha bwana wangu mfalme.”
Ndipo Ahimaasi akamwita mfalme, akasema, “Mambo yote ni mema!” Akasujudu mbele ya mfalme uso wake mpaka ardhini, akasema, “Ahimidiwe Bwana Mungu wako! Yeye aliyewatoa watu wale walioinua mikono yao dhidi ya mfalme bwana wangu.”
29 Hivyo mfalme akauliza, “Je huyo kijana Absalomu hajambo?” Ahimaasi akajibu, “Wakati Yoabu ananituma kwako mfalme, mimi mtumishi wa mfalme, niliona fujo kubwa sana lakini sikutambua ilihusu nini.”
Mfalme akauliza, “Je, huyo kijana Absalomu yuko salama?” Ahimaasi akajibu, “Kulikuwa na machafuko mengi mara tu Yoabu alipokuwa anataka kumtuma mtumishi wa mfalme pamoja nami mtumishi wako, lakini sijui ilikuwa nini?”
30 Mfalme akamwambia, “Geuka usimame kando.” Hivyo Ahimaasi akageuka na kusimama.
Mfalme akasema, “Simama kando na usubiri hapa.” Basi akasogea kando na kusimama hapo.
31 Mara Mkushi akafika na kusema, “Kuna habari njema kwa bwana wangu mfalme kwa kuwa leo Yahwe amekulipia kisasi kwa wale wote walioinuka kinyume chako.”
Ndipo huyo Mkushi akawasili na kusema, “Mfalme bwana wangu, sikia habari njema! Leo Bwana amekuokoa kutoka kwa wale wote walioinuka dhidi yako.”
32 Ndipo mfalme akamwuliza, “Je huyo kijana Absalomu ni mzima?” Mkushi akajibu, “Adui wa bwana wangu mfalme na wote wainukao kukudhuru na wawe kama huyo kijana.”
Mfalme akamuuliza huyo Mkushi, “Je, kijana Absalomu yuko salama?” Huyo Mkushi akajibu, “Adui wa mfalme bwana wangu na wote wale walioinuka kukudhuru na wawe kama huyo kijana.”
33 Ndipo mfalme alipohuzunishwa sana naye akaenda chumbani juu ya lango na kulia. Kadili alivyokwenda aliomboleza, mwanangu Absalomu, mwanangu, mwanangu Absalomu! afadhari ningekufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
Mfalme akatetemeka. Akapanda chumbani juu kupitia langoni akilia. Alipokuwa akienda, akasema, “Ee mwanangu Absalomu! Mwanangu, mwanangu Absalomu! Laiti ningekufa badala yako: Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”

< 2 Samweli 18 >