< 2 Samweli 17 >
1 Kisha Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Niruhusu sasa nichague watu elfu kumi na mbili nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu.
Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nipe ruhusa niwachague watu kumi na mbili elfu na waanze safari usiku huu huu kumfuatia Daudi.
2 Nitampata kwa ghafla wakati amechoka na dhaifu nami nitamstukiza kwa hofu. Watu waliopamoja naye watakimbia nami nitamshambulia mfalme peke yake.
Nitamshambulia wakati akiwa amechoka na ni dhaifu. Nitampiga na hofu, na kisha watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake
3 Nitawarejesha watu wote kwako kama bibi harusi ajavyo kwa bwana wake, na watu wote watakuwa katika amani chini yako.”
na kuwarudisha watu wote kwako. Kifo cha mtu yule unayemtafuta kitamaanisha kurudi kwa wote, hakuna hata mtu mmoja atakayeumizwa.”
4 Alichokisema Ahithofeli kikampendeza mfalme na wazee wote wa Israeli.
Mpango huu ulionekana mzuri kwa Absalomu na kwa wazee wote wa Israeli.
5 Kisha Absalomu akasema, “Sasa mwiteni pia Hushai Mwarki ili tusikie yeye pia anasemavyo.”
Lakini Absalomu akasema, “Pia mwiteni Hushai, Mwariki, ili tuweze kusikia anachokisema.”
6 Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamweleza kile ambacho Ahithofeli alikuwa amesema na kisha akamwuliza Hushai, “Je tufanye alivyosema Ahithofeli? Ikiwa hapana, tueleze kile unachoshauri.”
Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa shauri hili. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.”
7 Hivyo Hushai akamwambia Absalomu, “Ushauri aliotoa Ahithofeli siyo mzuri kwa wakati huu.”
Hushai akamjibu Absalomu, “Shauri la Ahithofeli alilotoa halifai kwa wakati huu.
8 Hushai akaongeza, “Unamjua baba yako na kwamba watu wake ni mashujaa na kwa sasa wanauchungu, ni kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake mwituni. Baba yako ni mtu wa vita; hatalala na jeshi usiku huu.
Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu mwitu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi.
9 Tazama, kwa wakati huu pengine amejificha katika shimo fulani au mahali pengine. Itakuwa kwamba baadhi ya watu wako watakapokuwa wameuawa mwanzoni mwa shambulio hata kila mtu atakayesikia atasema, mauaji yamefanyika kwa askari wanaomfuata Absalomu.'
Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’
10 Kisha hata askari jasiri zaidi ambao moyo wao ni kama moyo wa simba, wataogopa kwa kuwa Israeli yote inajua kwamba baba yako ni mtu mwenye nguvu na kwamba watu alionao ni wenye nguvu sana.
Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari.
11 Hivyo ninashauri kwamba Israeli wote wakutanike kwako pamoja kutoka Dani hadi Beersheba, wengi kama mchanga ufuoni mwa bahari na kwamba wewe mwenyewe uende vitani.
“Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyikie kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, katika wingi wao jinsi walivyo kama mchanga wa ufuoni mwa bahari, wewe mwenyewe ukiwaongoza vitani.
12 Kisha tutampata popote atakapokuwa nasi tutamfunika kama umande uangukavyo juu ya nchi. Hatutamwachia hata mmoja aliye hai kati ya watu wake wala yeye mwenyewe.
Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe wala watu wake hakuna atakayeachwa hai.
13 Ikiwa ataingia ndani ya mji kisha Israeli wote tutaleta kamba juu ya mji huo na kuukokotea mtoni, hata kusionekane hata jiwe moja dogo lililosalia.”
Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo mpaka bondeni hadi isionekane hata changarawe ya huo mji.”
14 Kisha Absalomu na watu wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai Mwarki ni jema kuliko lile la Ahithofeli. Yahwe aliwafanya wakatae shauri jema la Ahithofeli ili kumwangamiza Absalomu.
Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai, Mwariki, ni jema zaidi kuliko lile la Ahithofeli.” Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kupinga shauri nzuri la Ahithofeli, ili kuleta maafa juu ya Absalomu.
15 Kisha Hushai akawambia Sadoki na Abiathari makuhani, “Ahithofeli alimshauri Absalomu na wazee wa Israeli hivi na hivi, lakini mimi nimeshauri vinginevyo.
Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya kadha wa kadha, lakini mimi nimewashauri wao kufanya kadha wa kadha.
16 Sasa basi, nendeni haraka na mmtaarifu Daudi kusema, 'Usipige kambi usiku huu katika vivuko vya Araba, lakini kwa namna yoyote vukeni, tofauti na hapo mfalme atamezwa pamoja na watu wote walio pamoja naye.”
Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’”
17 Yonathani na Ahimaasi walikuwako katika chemichemi za En Rogeli. Hivyo kijakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapasha habari waliyopaswa kuifahamu, ili kwamba wasihatarishe maisha yao kwa kuonwa wakiingia mjini. Ujumbe ulipofika ndipo huenda na kumtaarifu mfalme Daudi.
Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli, naye mtumishi mmoja wa kike akawa anakwenda kuwapasha habari nao wakawa wanakwenda kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini.
18 Lakini kijana mmoja akawaoni mara akamwambia Absalomu. Hivyo Yonathani na Ahimaasi wakaenda kwa haraka na wakaingia katika nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu, aliyekuwa na kisima katika ua wake wakaingia humo.
Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda mpaka kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima katika ua wa nyumba yake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho.
19 Mke wa mtu huyo akachukua kifuniko na kukikufunika kwenye mlango wa kisima kisha akaanika nafaka juu yake, hivyo hakuna aliyejua kwamba Yonathani na Ahimaasi walikuwa kisimani.
Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka kwenye mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo.
20 Watu wa Absalomu wakaja kwa mwanamke na kumwuliza, “Ahimaasi na Yonathani wako wapi?” Mwanamke akawaambia, “Wamevuka mto.” Hivyo baada ya kuwatafuta bila kuwaona kurejea Yerusalemu.
Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu.
21 Ikawa baada yao kuondoka Yonathani na Ahimaasi wakatoka ndani ya kisima. Wakaenda kumtaarifu mfalme Daudi; wakamwambia, “Inuka na uvuke maji haraka kwa maana Ahithofeli ametoa mashauri haya na haya juu yako.”
Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke haya maji haraka. Ahithofeli ameshauri kadha wa kadha dhidi yako.”
22 Kisha Daudi akainuka pamoja na watu wote walikuwa pamoja naye, nao wakauvuka Yordani. Hata ilipofika alfajiri hakuna hata mmoja aliyesalia kwa kutouvuka Yordani.
Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja ambaye alikuwa hajavuka Mto Yordani.
23 Ikawa Ahithofeli alipoona kwamba ushauri wake haukufuatwa, akapanda punda wake na kuondoka. Akaenda nyumbani katika mji wake mwenyewe, akaweka mambo yake katika utaratibu na kisha akajinyonga. Kwa hiyo akafa na kuzikwa katika kaburi la baba yake.
Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani kwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake.
24 Ndipo Daudi akaja Mahanaimu. Lakini Absalomu yeye akavuka Yordani yeye pamoja na watu wote wa Israeli waliokuwa pamoja naye.
Daudi akaenda Mahanaimu, naye Absalomu akavuka Yordani pamoja na watu wote wa Israeli.
25 Absalomu alikuwa amemweka Amasa juu ya jeshi badala ya Yoabu. Naye huyo Amasa alikuwa mwana wa Yetheri Mwishmaeli, aliyekuwa amelala na Abigaili, aliyekuwa binti Nahashi na dada wa Seruya, mamaye Yoabu.
Absalomu alikuwa amemweka Amasa juu ya jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa mtu mmoja aliyeitwa Yetheri, Mwisraeli, ambaye alikuwa amemwoa Abigaili binti Nahashi, dada yake Seruya mamaye Yoabu.
26 Kisha Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi.
Waisraeli na Absalomu wakapiga kambi huko nchi ya Gileadi.
27 Ikawa wakati Daudi alipokuwa amekuja Mahanaimu, huyo Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni na Makiri mwana wa Amieli wa kutoka Lo Debari, na Berzilai Mgileadi wa Rogelimu,
Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu
28 wakaleta magodoro na mabulangeti, mabakuri na vyungu, na ngano, unga wa shayiri, nafaka zilizokaangwa, maharage, dengu,
wakaleta matandiko ya kitandani, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde,
29 asali, siagi, kondoo na samli, ili kwamba Daudi na watu waliokuwa pamoja naye waweze kula. Kwani walisema, “Watu wana njaa, wamechoka na wana kiu huko nyikani.”
asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka kwenye maziwa ya ngʼombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”