< 2 Samweli 12 >

1 Kisha Yahwe akamtuma Nathani kwa Daudi. Akaja kwake na kusema, “Kulikuwa na watu wawili katika mji. Mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa masikini.
Bwana akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwepo na watu wawili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini.
2 Yule tajiri alikuwa na kundi la ng'ombe na kondoo wengi sana,
Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ngʼombe,
3 lakini maskini hakuwa na chochote isipokuwa mwanakondoo, aliyekuwa amemnunua na kumlisha na kumlea. Akakua pamoja naye na pamoja na watoto wake. Yule mwanakondoo hata alikula naye na kunywa kutoka katika kikombe chake, naye akalala katika mikono yake na alikuwa kama binti kwake.
lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.
4 Siku moja tajiri akapata mgeni, lakini yeye hakuwa tiyari kuchukua mnyama kutoka katika kundi lake la ng'ombe au kundi la kondoo ili kumwandalia chakula. Badala yake alichukua mwanakondoo wa masikini na akampika kwa ajili ya mgeni wake.
“Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri akaacha kuchukua mmoja wa kondoo au ngʼombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”
5 Hasira ya Daudi ikawaka dhidi ya tajiri yule, naye akamwambia Nathani kwa hasira, “Kama Yahwe aishivyo, mtu aliyelitenda jambo hili anastahili kufa.
Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Bwana aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa!
6 Ni lazima alipe mwanakondoo mara nne zaidi kwa ajili ya kile alichokifanya, na kwa sababu hakuwa na huruma kwa mtu maskini.
Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”
7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiye yule mtu! Yahweh, Mungu wa Israeli, asema, 'Nilikutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, na nilikuokoa kutoka katika mkono wa Sauli.
Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli.
8 Nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake zake mikononi mwako. Nilikupa pia nyumba ya Israeli na Yuda. Na ikiwa hayo yalikuwa kidogo zaidi kwako, ningeweza kukuongezea mengine zaidi.
Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba ya Israeli na Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi.
9 Hivyo basi kwa nini umedharau maagizo ya Yahwe, hata ukafanya yaliyo maovu mbele zake? Umeua Uria Mhiti kwa upanga na umechukua mkewe kuwa mke wako. Uliua kwa upanga wa jeshi la Amoni.
Kwa nini ulilidharau neno la Bwana kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria, Mhiti kwa upanga na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni.
10 Hivyo basi upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria mhiti kuwa mke wako.'
Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria, Mhiti kuwa mkeo.’
11 Yahwe asema, 'Tazama, nitaleta maafa dhidi yako kutoka katika nyumba yako mwenyewe. Nitachukua wake zako, mbele ya macho yako na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako wakati wa mchana.
“Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu.
12 Kwa maana wewe ulitenda dhambi hii sirini, lakini mimi nitatenda jambo hili wakati wa mchana mbele za Israeli wote.
Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’”
13 Ndipo Daudi alipomwambia Nathani, “Nimemtenda dhambi Yahwe.” Nathani akamjibu Daudi, “Yahwe naye ameiachilia dhambi yako. Hautakufa.
Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.” Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa.
14 Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umemdharau Yahwe, mtoto aliyezaliwa kwako hakika atakufa.”
Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Bwana kuonyesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”
15 Kisha Nathani akaondoka na kwenda kwake. Yahwe akampiga mtoto ambaye mke wa Uria alimzaa kwa Daudi, naye akaugua sana.
Baada ya Nathani kurudi nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua.
16 Kisha Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya kijana. Daudi akafunga naye akaingia ndani na kulala usiku wote juu ya sakafu.
Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha.
17 Wazee wa nyumba yake wakainuka na kusimama kando yake, ili wamwinue kutoka sakafuni. Lakini hakuinuka, na hakula pamoja nao.
Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.
18 Ikawa siku ya saba mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kwamba mtoto amekufa, kwa maana walisema, “Tazama, wakati mtoto alipokuwa hai tuliongea naye, lakini hakuisikiliza sauti yetu. Atakuwaje ikiwa tutamwambia kwamba kijana amekufa?!”
Kunako siku ya saba yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Wakati mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”
19 Daudi alipoona kwamba watumishi wake walikuwa wakinong'onezana, Akatambua kwamba mtoto amekufa. Akawauliza, “Je mtoto amekufa?” Wakajibu, “Amekufa.”
Daudi akaona kuwa watumishi wake wananongʼonezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?” Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”
20 Kisha Daudi akainuka kutoka sakafuni naye akaoga, akajipaka mafuta, na kubadili mavazi yake. Akaenda katika hema la kukutania na akaabudu pale, kisha akarudu katika kasri lake. Akataka chakula kiletwe, wakamwandalia, naye akala.
Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Bwana, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani kwake kwa kutaka kwake, wakamwandalia chakula, naye akala.
21 Ndipo watumishi wake walipomwambia, “Kwa nini umefanya jambo hili? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto wakati alipokuwa hai, lakini mtoto alipokufa, ukainuka na kula.”
Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”
22 Daudi akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa hai nilifunga na kulia. Nilisema, Ni nani ajuaye kwamba Yahwe angeweza kunihurumia mtoto akaishi au sivyo?
Akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa bado yungali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Bwana aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’
23 Lakini sasa amekufa, hivyo nifungie nini? Je naweza kumrudisha tena? Nitakwenda kwake, lakini yeye hawezi kunirudia.”
Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”
24 Daudi akamfariji Bethsheba mkewe, akaingia kwake, na akalala naye. Baadaye akazaa mtoto wa kiume, naye akaitwa Selemani. Yahwe akampenda
Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina lake Solomoni. Bwana alimpenda Solomoni.
25 naye akatuma neno kupitia nabii Nathani kumwita Yedidia, kwa sababu Yahwe alimpenda.
Kwa kuwa Bwana alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia kwa ajili ya Bwana.
26 Basi Yoabu akapigana na Raba, mji wa kifalme wa watu wa Amoni, naye akaiteka ngome yake.
Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome la kifalme.
27 Hivyo Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi na kusema, “Nimepigana na Raba, nami nimeshikilia sehemu inayosambaza maji ya mji.
Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji.
28 Kwa hiyo sasa likusanye jeshi lililosalia uhuzingire mji na kuuteka, kwa maana ikiwa nitauteka, utaitwa kwa jina langu.”
Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.”
29 Hivyo Daudi akalikusanya jeshi lote na kwenda Raba; akapigana nao na kuuteka.
Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka.
30 Daudi akachukua taji ya dhahabu kutoka katika kichwa cha mfalme wao iliyokuwa na uzito wa talanta, na ilikuwa na jiwe la thamani ndani yake. Taji ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Kisha akachukua nyara za mji kwa wingi.
Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo.
31 Akawatoa watu waliokuwa mjini naye akawalazimisha kufanya kazi kwa misumeno, sululu na shoka; lakini pia akawalazimisha kutengeneza matofali. Daudi akailazimisha miji yote ya watu wa Amoni kufanya kazi hiyo. Kisha Daudi na jeshi lote wakarudi Yerusalemu
Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.

< 2 Samweli 12 >