< 2 Samweli 11 >
1 Ikawa wakati wa majira ya kipupwe, wakati ambapo kwa kawaida wafalme huenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu, mtumishi wake, na jeshi lote la Israeli. Wakaliaribu jeshi la Amoni na kuuhusuru Raba. Lakini Daudi akakaa Yerusalemu.
Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme watokapo kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzunguka kwa jeshi mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.
2 Hivyo ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi akaamka kutoka kitandani na akatembea katika dari la kasri. Akiwa pale akamwona mwanamke aliyekuwa akioga, mwanamke yule alikuwa mzuri sana kwa mwonekano.
Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Kutokea kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura,
3 Hivyo Daudi akatuma na kuuliza watu waliomfahamu yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, “Je huyu siye Bathsheba, binti Eliamu, naye si mke wa Uria mhiti?
naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria, Mhiti?”
4 Daudi akatuma wajumbe nao wakamchukua; akaja kwake, na akalala naye(kwani ndo alikuwa amejitakasa kutoka siku zake). Kisha akarudi nyumbani kwake.
Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani kwake.
5 Mwanamke akawa mjamzito, naye akatuma na kumwambia Daudi; akasema, “mimi ni mjamzito.”
Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”
6 Kisha Daudi akatuma watu kwa Yoabu kusema, “Umtume kwangu Uria mhiti.” Hivyo Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.
Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria, Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.
7 Uria alipofika, Daudi akamuuliza hali ya Yoabu. Jinsi jeshi lilivyokuwa likiendelea, na jinsi vita vilivyokuwa vinaendelea.
Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje.
8 Daudi akamwambia Uria, “Shuka nyumbani kwako, unawe miguu yako. “Hivyo Uria akaondoka katika kasri la mfalme, mfalme akamtumia zawadi kwa Uria.
Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akaondoka kutoka kwenye jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme.
9 Lakini Uria akalala pamoja na watumishi wa bwana wake katika lango la kasri, wala hakushuka nyumbani kwake.
Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani kwake.
10 Daudi alipoambiwa, “Uria hakushuka nyumbani kwake,” akamwambia Uria, Je haukutoka safarini? Kwa nini haukushuka nyumbani kwako?”
Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakwenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukwenda nyumbani?”
11 Uria akamjibu Daudi, “Sanduku, na Israeli na Yuda wamo kwenye mahema, na Yoabu na watumishi wa bwana wangu wamepiga hema uwandani. Jinsi gani basi mimi naweza kwenda nyumbani kwangu kula kunywa na kulala na mke wangu? kwa hakika kama uishivyo, sitafanya hivyo.
Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani kwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo la namna hiyo!”
12 Hivyo Daudi akamwambia Uria, “Ukae leo pia, kesho nitakuacha uende.” Kwa hiyo uria akakaa Yerusalemu siku hiyo na iliyofuata.
Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata.
13 Daudi alipomwita, alikula na kunywa pamoja naye, Daudi akamfanya alewe. Wakati wa jioni Uria akaenda kulala kitandani pake pamoja na watumish wa bwana wake; hakushuka nyumbani kwake.
Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakwenda nyumbani.
14 Hivyo asubuhi Daudi akamwandikia Yoabu barua, naye akaituma kwa mkono wa Uria.
Asubuhi yake Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka.
15 Ndani ya barua Daudi aliandika hivi, “Mweke Uria mbele ya vita vikali sana, na kisha, mmwache, ili apigwe na afe.
Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele mahali ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.”
16 Hivyo Yoabu alipoona mji ukizingirwa, alimweka Uria katika sehemu aliyojua askari adui wenye nguvu wangekuwa wakipigana.
Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali ambapo alijua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana.
17 Wakati watu wa mji walipotoka na kupigana dhidi ya jeshi la Yoabu, baadhi ya askari wa Daudi wakaanguka, na Uria Mhiti pia akauwawa.
Wakati watu wa mjini walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa, zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, akafa.
18 Wakati Yoabu alipotuma neno kwa mfalme kuhusu hali ya vita,
Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita.
19 alimwagiza mjumbe, kusema, “Utakapomaliza kumwambia mfalme kuhusu hali ya vita,
Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita,
20 yawezekana mfalme akakasirika, naye akakwambia, 'Kwa nini mlipigana na mji kwa karibu hivyo, hamkujua kwamba wangeweza kushambulia kutokea ukutani?
hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani?
21 Ni nani aliyemwua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Siye mwanamke aliyerusha jiwe la kusagia juu yake kutoka ukutani, hata akafa huko Thebesi? Kwanini basi mliukaribia ukuta jinsi hiyo? Nawe umjibu, 'Uria mtumishi wako amekufa pia.”
Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Ikiwa atakuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa.’”
22 Hivyo mjumbe akaondoka na kwenda kwa Daudi akamwambia kila jambo ambalo Yoabu alimtuma kusema.
Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema.
23 Na mjumbe akamwambia Daudi, “Mwanzoni adui walikuwa na nguvu kuliko sisi; walitukabili uwandani, lakini tukawarudisha nyuma kwenye maingilio ya lango.
Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma mpaka kwenye ingilio la mji.
24 Na wapiga mishale wao wakawarushia watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watumishi wa mfalme wameuawa, na mtumishi wako Uria mhiti pia ameuawa.”
Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, mtumishi wako amekufa.”
25 Kisha Daudi akamwambia mjumbe, “Mwambie hivi Yoabu, 'Usiruhusu jamba hili likuhuzunishe, kwa maana upanga huangamiza huyu kama uangamizavyo na mwingine. Vifanye vita vyako kuwa vyenye nguvu zaidi dhidi ya mji, na uuteke.' Mtie moyo Yoabu.”
Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”
26 Hivyo mke Uria aliposikia kwamba mme wake amekufa, akaomboleza sana kwa ajili yake.
Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea.
27 Huzuni yake ilipoisha, Daudi akatuma na kumchukua kwake katika kasri lake, naye akawa mkewe na akamzalia mwana. Lakini alichokifanya Daudi hakikumpendeza Yahwe.
Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akamtaka aletwe nyumbani kwake, naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilokuwa amefanya Daudi lilimchukiza Bwana.