< 2 Samweli 10 >

1 Ikawa baadaye mfalme wa watu wa Amoni akafa, na Hanuni mwanaye akawa mfalme mahali pake.
Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akaingia mahali pake.
2 Daudi akasema, “Nitaonesha fadhiri Hanuni mwana wa Nahashi, kwa kuwa baba yake alinifadhiri.” Hivyo Daudi akatuma watumishi wake kumfariji Hanuni kwa habari ya baba yake. Watumishi wake wakaingia katika nchi ya watu wa Amoni.
Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma wajumbe kuonyesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake. Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni,
3 Lakini viongozi wa watu wa Amoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “Je unathani kwa hakika Daudi anamweshimu baba yako hata ametuma watu kukutia moyo? Daudi hajawatuma watumishi wake kwako ili kuuangalia mji, kuupeleleza, ili kuupindua?
wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonyesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?”
4 Hivyo Hanuni akawachukuwa watumishi wa Daudi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akachana mavazi yao hadi kwenye matako, naye akawaacha waende zao.
Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaacha waende zao.
5 Daudi alipoelezwa kuhusu hili, akatuma watu kwenda kuwalaki, kwa kuwa walikuwa wamefedheheshwa sana. Mfalme akawambia, “Kaeni Yeriko mpaka ndevu zenu zitakapoota, ndipo mrudi.”
Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu ziote ndipo mje.”
6 Watu wa Amoni walipoona kwamba wamenuka kwa Daudi, wakatuma wajumbe na kuwaajiri Washami wa Bethi Rehobu na Soba, askari elfu ishirini waendao kwa mguu, na mfalme wa Maaka pamoja na watu elfu, na watu wa Tobu elfu kumi na mbili.
Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, wakaajiri askari wa miguu 20,000 Waaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka pamoja na watu 1,000, na vilevile watu 12,000 kutoka Tobu.
7 Daudi aliposikia, akamtuma Yoabu na jeshi lote la askari.
Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.
8 Waamoni wakatoka na wakafanya mistari ya vita katika maingilio ya lango la mji wao, wakati Washami wa Soba na wale wa Rehobu, na watu wa Tobu na Maaka, wakasimama peke yao uwandani.
Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati Waaramu wa Soba, wa Rehobu, watu wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi.
9 Yoabu alipoona mistari ya vita ikimkabili pote mbele na nyuma, alichagua baadhi ya waisraeli wajuao kupigana vizuri na akawapanga dhidi ya Washami.
Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu.
10 Na sehemu iliyosalia ya jeshi, akawaweka chini ya Abishai nduguye, naye akawaweka katika mistari ya vita dhidi ya jeshi la Amoni.
Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni.
11 Yoabu akasema, “ikiwa Washami watakuwa na nguvu zaidi juu yangu, kisha wewe, Abishai, lazima uniokoe. Lakini ikiwa jeshi la Amoni litakuwa na nguvu zaidi juu yako, nitakuja kukuokoa.
Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itawabidi mje kunisaidia. Lakini kama Waamoni watawazidi nguvu, basi nitakuja kuwasaidia.
12 Iweni na nguvu, nasi tujioneshe kuwa wenye nguvu kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu, kwa maana Yahwe atatenda yapendezayo kwa ajili ya kusudi lake.
Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake.”
13 Hivyo Yoabu na askari wa jeshi lake wakasonga mbele katika vita dhidi ya Washami, waliolazimika kukimbia mbele ya jeshi la Israeli.
Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake.
14 Jeshi la Amoni lilipoona kwamba Washami wamekimbia, nao pia wakakimbia kutoka kwa Abishai wakarudi ndani ya mji. Ndipo Yoabu akarudi kutoka kwa watu wa Amoni na akarejea Yerusalemu.
Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.
15 Washami walipoona kwamba wameshindwa na Israeli, walijikusanya pamoja tena.
Baada ya Waaramu kuona wameshindwa na Israeli, wakajikusanya tena.
16 Kisha Hadareza akatuma kuleta vikosi vya Washami ng'ambo ya Mto Frati. Wakaja Helamu pamoja na Shobaki, mkuu wa jeshi la Hadareza juu yao.
Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ngʼambo ya Mto Frati, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza.
17 Daudi alipoambiwa, aliwakusanya Israeli wote pamoja, akavuka Yordani, na akafika Helamu. Washami wakajipanga katika mistari ya vita dhidi ya Daudi na wakapigana naye.
Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi.
18 Washami wakakimbia mbele ya Israeli. Daudi akaua askari mia saba wa magari na askari wa farasi elfu arobaini. Shobaki mkuu wa jeshi lao alijeruhiwa na akafa huko.
Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari mia saba na askari wao wa miguu 40,000. Vilevile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko.
19 Wafalme wote waliokuwa watumishi wa Hadareza walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, walifanya amani na Israeli na wakawa watumishi wao. Hivyo washami wakaogopa kuwasaidia watu wa Amoni tena.
Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao. Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.

< 2 Samweli 10 >