< 2 Petro 1 >

1 Simon Petro, Mtumwa na Mtume wa Yesu Kristo, Kwa wale walioipokea imani ile ile ya thamani kama tulivyoipokea sisi, imani iliyo ndani ya haki ya Mungu na mwokozi wetu Yesu Kristo.
Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo: Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:
2 Neema iwe kwenu; amani iongezeke kupitia maarifa ya Mungu na Bwana wetu Yesu.
Neema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Kupitia maarifa ya Mungu tumepata mambo yake yote kwa ajili ya uchaji wamaisha, Toka kwa Mungu aliyetuita kwa ajili ya uzuri wa utukufu wake.
Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.
4 Kwa njia hii alitutumainishia ahadi kuu za thamani. Alifanya hili ili kutufanya warith wa asili ya Mungu, kwa kadiri tunavyoendelea kuuacha uovu wa dunia hii.
Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
5 Kwa sababu hii, fanyeni bidii kuongeza uzuri kwa njia ya imani yenu, kwa sababu ya uzuri, maarifa.
Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa;
6 Kupitia maarifa, kiasi, na kupitia kiasi saburi, na kupitia saburi, utauwa.
katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa;
7 Kupitia utauwa upendo wa ndugu na kupitia upendo wa ndugu, upendo.
katika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo.
8 Kama mambo haya yamo ndani yenu, yakiendelea kukua ndani yenu, basi ninyi hamtakuwa tasa au watu msiozaa matunda katika maarifa ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Lakini yeyote asiyekuwa na mambo haya, huyaona mambo ya karibu tu; yeye ni kipofu. amesahau utakaso wa dhambi zake za kale.
Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, na ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni juhudi ili kujihakikishia uteule na wito kwa ajili yenu. Kama mtayafanya haya, hamtajikwaa.
Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe,
11 Hivyo mtajipatia wingi wa lango la kuingilia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu na mwokozi Yesu Kristo. (aiōnios g166)
na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. (aiōnios g166)
12 Kwa hiyo mimi nitakuwa tayari kuwakumbusha mambo haya kila mara, hata kama mnayafahamu, na sasa mmekuwa imara katika kweli.
Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo.
13 Nafikiria kuwa niko sahihi kuwaamsha na kuwakumbusha juu ya mambo haya, ningali nimo katika hema hii.
Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niwapo katika hema hili ambalo ni mwili wangu,
14 Kwa maana najua kuwa si muda mrefu nitaiondoa hema yangu, kama Bwana Yesu Kristo alivyonionyesha.
kwa sababu najua ya kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Yesu Kristo alivyoliweka wazi kwangu.
15 Nitajitahidi kwa bidii kwa ajili yenu ili mkumbuke mambo haya baada ya mimi kuondoka.
Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.
16 Kwa kuwa sisi hatukufuata hadthi zilizoingizwa kwa ustadi pale tulipowaeleza juu ya nguvu na kujidhihirisha kwa Bwana wetu Yesu Kristo, bali sisi tulikuwa mashahidi wa utukufu wake.
Tulipowafahamisha juu ya uweza na kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake.
17 Yeye alipokea Utukufu na heshima toka kwa Mungu baba pale sauti iliposikika toka katika utukufu mkuu ikisema, “Huyu ndiye mwanangu, mpendwa wangu ambaye nimependezwa naye.”
Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.”
18 Tuliisikia sauti hii ikitokea mbinguni pale tulipokuwa naye kwenye ule mlima mtakatifu.
Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.
19 Tunalo hili neno la unabii lililothibitika, ambalo kwalo mwafanya vyema kulitekeleza. Ni kama taa ing'aayo gizani mpaka kuchapo na nyota za mawio zionekanazo katika mioyo yenu.
Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu.
20 Tambueni haya ya kwamba, hakuna unabii unaoandikwa kwa sababu ya kujifikirisha kwa nabii mwenyewe.
Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe.
21 Kwa kuwa hakuna unabii uliokuja kwa mapenzi ya mwanadamu, isipokuwa wanadamu waliwezeshwa na Roho Mtakatifu aliyeongea toka kwa Mungu.
Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

< 2 Petro 1 >