< 2 Wafalme 9 >
1 Nabii Elisha akamwita mmoja wa watoto wa manabii na kumwambia, “Vaa kwa kwa safari, halafu chukua hii chupa ndogo ya mafuta kwenye mikono yako na uende Romoth Geliadi.
Nabii Elisha akamwita mtu mmoja kutoka kwa wana wa manabii na kumwambia, “Jikaze viuno, uichukue hii chupa ya mafuta, na uende Ramoth-Gileadi.
2 Wakati utakapofika, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati mwana wa Nimshi, na uende ukaingie na kumfanya ainuke kutoka miongoni mwa rafiki zake, na ukampeleke katika chumba cha ndani.
Ukifika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi. Enda kwake, umtenge na wenzake, na umpeleke katika chumba cha ndani.
3 Kisha chukua ile chupa ya mafuta na imiminie kwenye kichwa chake na kusema, 'Yahwe anasema hivi: “Nimekumiminia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. “Halafu fungua mlango, na kukimbia; usichelewe.”
Kisha chukua hii chupa na umimine mafuta juu ya kichwa chake, nawe utangaze, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ Kisha ufungue mlango na ukimbie; usikawie!”
4 Basi yule kijana, yule nabii kijana, akaenda Romoth Geliadi.
Basi yule kijana nabii akaenda Ramoth-Gileadi.
5 Wakati alipofika, kumbe, wale manahodha wa lile jeshi walikuwa wamekaa. Hivyo yule nabii kijana akasema, “Nimekuja mara moja naneno kwako, nahodha.” Yehu akajibu, “kwa yupi katika sisi?” Yule nabii kijana akajibu, “Kwako nahodha.”
Wakati alipofika, akawakuta maafisa wa jeshi wameketi pamoja, akasema, “Nina ujumbe wako, ee jemadari.” Yehu akauliza, “Kwa yupi miongoni mwetu?” Akamjibu, “Kwako wewe, jemadari.”
6 Basi Yehu akainuka na kwenda kwenye nyumba, na yule nabii akammiminia mafuta kwenye kichwa chake na kumwambia Yehu, “Yahwe, Mungu wa Israeli, anasema hivi: 'Nimekumiminia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Yahwe, juu ya Isaraeli.
Yehu akainuka na kuingia ndani ya nyumba. Ndipo yule nabii akamimina mafuta juu ya kichwa cha Yehu na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Bwana, yaani Israeli.
7 Wewe lazima uiue familia ya Ahabu bwana wako, ili niweze kulipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii, na damu ya watumishi wote wa Yahwe, ambao waliokuwa wameuawa kwa mkono wa Yezebeli.
Inakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote wa Bwana iliyomwagwa na Yezebeli.
8 Kwa kuwa nyumba yote ya Ahabu itaangamia, na nitamkatilia mbali kila mtoto wa kiume wa Ahabu, yeyote awe mtumwa au mtu huru.
Nyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa Ahabu katika Israeli, aliye mtumwa ama aliye huru.
9 Nitaifanya nyumba ya Ahabu kama nyumba ya Yerobohamu mwana wa Nebati na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
Nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
10 Mbwa watamla Yezebeli katika Yezreeli, na hakutakuwa na mtu wa kumzika.” Kisha nabii akafungua mlango na kukimbia.
Kuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli, wala hakuna mtu atakayemzika.’” Kisha akafungua mlango na kukimbia.
11 Kisha Yehu akatoka kwenda kwa watumishi wa bwana wake, na mmoja akamwambia, “Je kila kitu kiko sawa? Kwa nini huyu mwenda wazimu amekuja kwako?” Yehu akawajibu, “Mnamjua huyo mtu na mambo asemayo.”
Yehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamuuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?” Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu, na aina ya mambo ambayo yeye husema.”
12 Wakasema, “Huo ni uongo. Tuambie.” Yehu akajibu, “Alisema hivi na vile juu yangu, na pia akasema, 'hivi ndivyo Yahwe asemavyo: Nimekumiminia mafuta kama mfalme juu ya Israeli.””
Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.” Yehu akasema, “Haya ndiyo aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’”
13 Kisha kila mmoja wao akachukua vazi haraka na kuweka chini ya Yehu juu ya madaraja. Wakapiga baragumu na kusema, “Yehu ni mfalme.”
Wakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”
14 Katika njia hii Yehu mwana wa Yehoshafati mwana wa Nimshi akafanya njama juu ya Yoramu. Basi Yoramu alikuwa akiilinda Ramothi Gileadi, yeye na Israeli yote, kwa sababu ya Hazaeli mfalme wa Shamu,
Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya shauri baya dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Israeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu,
15 lakini mfalme Yoramu alikuwa amesharudi kwa Yezreeli ili kuponywa yale majeraha aliyokuwa ameyapewa na Washami, wakati akiwa anapigana dhidi ya Hazaeli mfalme wa Shamu. Yehu akawaambia watumishi wa Yoramu, “kama hili ndilo wazo lako, kisha usimwache mtu aondoke na kwenda nje ya mji, ili aende kupeleka habari hii Yezreeli.”
lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.”
16 Basi Yehu akaendesha gari la farasi mpaka Yezreeli; kwa kuwa Yoramu alikuwa amelala huko. Basi Ahazi mfalme wa Yuda alikuwa ameshuka chini kuonana na Yoramu.
Ndipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.
17 Mlinzi alikuwa amesimama juu ya mnara katika Yezreeli, akaliona lile kundi la Yehu alipokuwa akija kwa mbali kidogo; akasema, “Naona kundi la watu wanakuja.” Yoramu akasema, “Chukua mwendesha farasi, na umtume akakutane nao; mwambie aseme, “Je mnakuja kwa amani?””
Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.” Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’”
18 Hivyo mwendesha farasi akatoka kumlaki; akasema, “Mfalme asema hivi: Je mnakuja kwa amani?”' Basi Yehu akasema, “Wewe una nini na amani? Geuka na unifuate nyuma.” Kisha yule mlinzi akamwambia mfalme, Yule mjumbe ameshaonana nao, lakini anarudi.”
Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’” Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.” Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”
19 Kisha akapeleka mpanda farasi wa pili, ambaye alikuja kwao na kusema, “Mfalme asema hivi: 'Je mnakuja na amani?”' Yehu akajibu, “Wewe una nini na amani? Geuka na kunifuata nyuma.
Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Wakati alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’” Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”
20 Tena yule mlinzi akatoa taarifa, “Amekwisha kuonana nao, lakini hatorudi. Kwa kuwa hilo gari la farasi limekuwa likiendeshwa ndivyo ambavyo Yehu mwana wa Nimshi aendeshavyo; anaendesha kwa kasi.”
Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”
21 Hivyo Yoramu akasema, “Andaa gari langu la farasi liwe tayari.” Wakaandaa gari lake la farasi, na Yoramu mfalme wa Israeli na Ahazi mfalme wa Yuda akaendesha, kila mmoja kwenye gari lake la farasi, kumlaki Yehu. Wakamkuta kwenye mali ya Nabothi Myezreeli.
Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli.
22 Wakati Yoramu alipomuona Yehu, alisema, “Je unakuja katika hali ya amani, Yehu?” Akajibu, “Amani gani hapo, wakati uzinzi wa ukahaba hufanywa na uchawi wa mama yako Yezebeli umejaa tele?”
Yoramu alipomwona Yehu akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?” Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli ungaliko?”
23 Basi Yoramu akarudisha magari yake ya farasi na kukimbia na kumwambia Ahazia, “Kuna udanganyifu, Ahazia.
Yoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”
24 Ndipo Yehu akauvuta upinde wake kwa nguvu zake zote na kumpiga Yoramu kati ya mabega yake; mshale ukaenda kwenye moyo wake, akaanguka chini kwenye gari lake la farasi.
Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake.
25 Ndipo Yehu akamwambia Bidkari nahodha wake, “Mchukue na mtupie kwenye shamba la Nabothi Myezreeni. Fikiria kuhusu vile ambavyo wewe na mimi tulivyoendesha pamoja baada ya Ahabu baba yake, Yahwe aliuweka juu unabii dhidi yake:
Yehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Bwana alipotoa unabii huu kumhusu:
26 Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya watoto wake - asema Yahwe - na nitahakikisha unalipia hili shamba - asema Yahwe. Sasa basi, mchukue na mtupe kwenye hili shamba, sawa sawa na neno la Yahwe.”
‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Bwana.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Bwana.”
27 Wakati Ahazi yule mfalme wa Yuda alipoliona hili, akakimbia kwa njia ya Bethi Hagani. Lakini Yehu akamfuata, na kusema, “Muulie humo kwenye gari la farasi,” na wakampiga mahali pa kupandia Guri, karibu na Ebleamu. Ahazi akakimbilia Megido na kufia pale.
Wakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko.
28 Watumishi wake wakaubeba mwili wake kwa magari ya farasi kwenda Yerusalemu na kumzika kwenye kaburi lake pamoja na baba zake katika mji wa Daudi.
Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi.
29 Basi ilikuwa mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu huyo Ahazia akaanza kutawala juu ya Yuda.
(Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)
30 Wakati Yahu alipokuja kwa Yezebeli, Yezebeli akasikia juu ya hilo, akapaka wanja kwenye macho yake, akatengeneza nywele zake vizuri, na kuchungulia kwenye dirisha.
Kisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake rangi, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani.
31 Kadiri Yehu alipokuwa akiingia kwenye lango, akamwambia, “Je unakuja kwa amani, wewe Zimri, muuaji wa bwana wako?”
Yehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe muuaji wa bwana wako?”
32 Yehu akatazama juu ya dirisha na kusema, “Ni nani yuko upande wangu? Nani?” Matowashi wawili au watatu wakachungulia nje.
Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama.
33 Basi Yehu aksema, “Mtupeni chini.” Hivyo wakamtupa Yezebeli chini, na damu yake nyingine ikamwagika kwenye ukuta na farasi, na Yehu akamkanyaga kanyaga chini ya miguu.
Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, nayo baadhi ya damu yake ikatapanyika ukutani na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.
34 Basi Yehu akaingia hiyo sehemu, akala na kunywa. Kisha akasema, “Mtazamani sasa huyu mwanamke aliyelaaniwa na kumzika, kwa kuwa ni binti wa mfalme.”
Yehu akaingia ndani, akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa. Mzikeni, kwa sababu alikuwa binti wa mfalme.”
35 Wakaenda kumzika, lakini hawakumkuta ila fuvu, miguu, na viganga vya mikono yake.
Lakini walipotoka kwenda kumzika, hawakukuta kitu chochote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono.
36 Basi wakarudi na kumwambia Yehu. Akasema, “Hili ndilo neno la Yahwe ambalo ameliongea kupitia Eliya Mtishbi, likisema, 'Katika nchi Yezreeli mbwa ataula mwili wa Yezebeli,
Wakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno la Bwana alilosema kupitia kinywa cha mtumishi wake Eliya Mtishbi, kwamba: Katika kiwanja cha Yezreeli, mbwa wataikula nyama ya Yezebeli.
37 na mwili wa Yezebeli utakuwa kama kinyesi juu ya uso wa mashamba katika nchi ya Yezreeli, kwa hiyo basi hakuna atakayeweza kusema, “Huyu ni Yezebeli.””
Maiti ya Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwepo mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ndiye Yezebeli.’”