< 2 Wafalme 20 >

1 Katika siku hizo Hezekia aliugua akawa kwenye hatari ya kufa. Hivyo Isaya mwana wa Amozi, akaja, na kumwambia, “Yahwe asema, 'Weka nyumba yako kwenye mpangilio; kwa kuwa utakufa, na hutapona.'”
Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
2 Kisha Ahazi akageuza uso wake kwenye ukuta na kumuomba Yahwe, akisema,
Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana:
3 “Tafadhali, Yahwe, ukumbuke jinsi nilivyo mwaminifu kutembea mbele yako kwa moyo wangu wote, na jinsi nilivyofanya yaliyo mazuri usoni kwako.” Kisha Hezekia akalia kwa sauti.
“Ee Bwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
4 Kabla ya Isaya hajatoka nje kwenye mji wa kati, neno la Yahwe likamjia, kusema,
Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Bwana likamjia, akaambiwa:
5 '“Rudi, na umwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, 'Hivi ndivyo Yahwe, Mungu wa Daudi babu yako, asemavyo: “Nimesikia maombi yako, na nimeyaona machozi yako. Nitakuponya katika siku ya tatu, na utapanda juu kwenye nyumba ya Yahwe.
“Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda Hekalu la Bwana.
6 Nitakuongeza miaka kumi na tano ya maisha yako, na nitakulinda na huu mji kwa ajili yangu na kwa ajili ya mtumishi wangu."”'
Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’”
7 Hivyo Isaya akasema, “Chukueni mkate wa tini.” Walifanya hivyo na kuweka kwenye jipu lake, na akapona.
Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.
8 Hezekia akamwambia Isaya, “Je kutakuwa na alama gani ambayo Yahwe ataniponya, na kwamba nitapanda juu hadi kwenye hekalu la Yahwe katika siku ya tatu?”
Hezekia alikuwa amemuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Bwana ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana siku ya tatu tangu leo?”
9 Isaya akajibu, “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako kutoka kwa Yahwe, kwamba Yahwe atafanya kitu amacho alichokisema. Je kivuli kitaenda mbele hatua saba, au kurudi nyuma hatua saba?”
Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”
10 Hezekia akajibu, “Ni kitu chepesi kwa kivuli kwenda mbele hatua kumi. Hapana, hicho kivuli kirudi nyuma hatua kumi.”
Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”
11 Hivyo Isaya nabii akamlilia Yahwe, na akaleta kivuli hatua kumi nyuma, kutoka pale ambapo zilikuwa zimevuka kwenye ngazi za Ahazi.
Ndipo nabii Isaya akamwita Bwana, naye Bwana akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.
12 Katika kipindi hicho Merodak Baladani mfalme wa Babeli alituma barua na zawadi kwa Hezekia, kwa kuwa alisikia kwamba Hezekia alikuwa anaumwa.
Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia.
13 Hezekia akasikiliza hizo barua, na kisha kuwaonyesha wajumbe sehemu zote na sehemu zake za thamani, fedha, dhahabu, manukato na marhamu na nyumba yenye ghala la silaha zake, na yote yaliyokutwa kwenye ghala za nyumba zake. Hapakuwa na kitu kwenye nyumba, wala kwenye ufalme wake wote, ambao Hezekia hakuwaonyesha.
Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonyesha vitu vyote vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.
14 Kisha Isaya akaja kwa Hezekia na kumuuliza, “Hawa watu walikuwa wanakwambiaje? Wanatokea wapi?” Hezekia aksema, “Wamekuja kutoka nchi ya mbali ya Babeli.
Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?” Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”
15 Isaya akauliza, “Wameona nini kwenye nyumba yako?” Hezekia akajibu, “Wameona kila kitu kwenye nyumba yangu. Hakuna kitu miongoni mwa vitu vyangu vya thamani ambavyo sijawaonyesha.”
Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?” Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”
16 Basi Isaya akamwambia Hezekia, “Sikiliza neno la Yahwe:
Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana:
17 'Tazama siku zinakuja wakati kila kitu kwenye kwenye nyumba yako ya kifalme, vitu ambavyo babu zako walivitunza huko hadi leo, vitabebwa kwenda Babeli. Hakuna kitakachobakia, Yahwe asema.
Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana.
18 Watoto waliozaliwa na wewe, ambao umewazaa wewe mwenyewe-watawachukua mbali, na watakuwa matowashi kwenye nyumba ya kifalme ya mfalme wa Babeli.'”
Nao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
19 Hezekia akamwambia Isaya, “neno la Yahwe uliloliongea ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, Je sivyo ikiwapo amani na kweli katika siku zangu?”
Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Lakini si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”
20 Kama kwa mambo mengine yanamuhusu Hezekia, na ushujaa wake wote, na jinsi alivyotengeza bwawa la maji na mfereji, na kuleta maji kwenye mji-hayakuandikwa kwenye kitabu cha ya matukio ya wafalme wa Yuda?
Matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ambao ulileta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
21 Hezekia akalala na babu zake, na Manase mwanae akawa mfalme katika sehemu yake.
Hezekia akafa, akazikwa pamoja na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.

< 2 Wafalme 20 >