< 2 Wakorintho 5 >
1 Tunajua kwamba kama maskani ya ulimwenguni ambayo tunaishi humo yanaharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu. Ni nyumba isiyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, bali ni nyumba ya milele, katika mbingu. (aiōnios )
Kwa maana twajua kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. (aiōnios )
2 Kwa kuwa katika hema hii tunaugua, tukitamani kuvikwa kwa maskani yetu mbinguni.
Katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni,
3 Tunatamani kwa ajili ya hii kwa sababu kwa kuivaa hatutaonekana kuwa tu uchi.
kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena kuwa uchi.
4 Kwa hakika wakati tuko ndani ya hema hii, twaugua tukilemewa. Hatutaki kuvuliwa. Badala yake, tunataka kuvalishwa, ili kwamba kile kilicho kufa kiweze kumezwa na uzima.
Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hii twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kwamba kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima.
5 Yule aliyetuandaa sisi kwa kitu hiki ni Mungu, ambaye alitupa sisi Roho kama ahadi ya kile kitakacho kuja.
Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo naye ametupa Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.
6 Kwa hiyo muwe na ujasiri siku zote. Muwe macho kwamba wakati tuko nyumbani katika mwili, tuko mbali na Bwana.
Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana,
7 Kwa kuwa tunatembea kwa imani, sio kwa kuona. Kwa hiyo tunaujasiri.
kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona.
8 Ni bora tuwe mbali kutoka kwenye mwili na nyumbani pamoja na Bwana.
Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.
9 Kwa hiyo tunaifanya kuwa lengo letu, kama tukiwa nyumbani au mbali, tumpendeze yeye.
Kwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana.
10 Kwa kuwa lazima wote tuonekane mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kwamba kila mmoja aweze kupokea kile kinachostahili kwa mambo yaliyofanyika katika mwili, ikiwa ni kwa uzuri au kwa ubaya.
Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.
11 Kwa hiyo, kwa kuijua hofu ya Bwana, tunawashawishi watu. Jinsi tulivyo, inaonekana wazi na Mungu. Ninatumaini kuwa inaeleweka pia kwenye dhamiri zenu.
Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.
12 Hatujaribu kuwashawishi ninyi tena kutuona sisi kama wakweli. Badala yake, tunawapa ninyi sababu ya kujivuna kwa ajili yetu, ili kwamba muweze kuwa na jibu kwa wale wanaojivunia kuhusu mwonekano lakini sio kile kilicho ndani ya moyo.
Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu mweze kuwajibu hao wanaoona fahari juu ya mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni.
13 Kwa kuwa ikiwa kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu. Na kama tuko kwenye akili zetu timamu, ni kwa ajili yenu.
Kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu.
14 Kwa kuwa upendo wa Kristo watushurutisha, kwa sababu tuna uhakika na hili: kuwa mtu mmoja alikufa kwa ajili ya wote, na kwa hiyo wote wamekufa.
Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa.
15 Na Kristo alikufa kwa ajili ya wote, ili kwamba wale wanaoishi wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe. Badala yake, lazima waishi kwa ajili yake yeye ambaye alikufa na alifufuliwa.
Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.
16 Kwa sababu hii, kuanzia sasa na kuendelea hatumuhukumu mtu kulingana na viwango vya wanadamu, ingawa hapo kwanza tulimtazama Kristo katika namna hii. Lakini sasa hatumuhukumu yeyote kwa namna hii tena.
Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Kristo kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo.
17 Kwa hiyo, ikiwa mtu yeyote yuko ndani ya Kristo, yeye ni kiumbe kipya. Mambo ya kale yamepita. Tazama, yamekuwa mapya.
Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya.
18 Vitu vyote hivi vyatoka kwa Mungu. Alitupatanisha sisi kwake mwenyewe kupitia Kristo, na ametupatia huduma ya upatanisho.
Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho:
19 Hiyo ni kusema, katika Kristo, Mungu anaupatanisha ulimwengu kwake mwenyewe, sio kuhesabu makosa yao dhidi yao. Anawekeza kwetu ujumbe wa upatanisho.
Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho.
20 Kwa hiyo tunateuliwa kama wawakilishi wa Kristo, kana kwamba Mungu alikuwa anafanya rufaa yake kupitia sisi. Tunawasihi ninyi kwa ajili ya Kristo: “Mpatanishwe kwa Mungu!”
Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.
21 Alimfanya Kristo kuwa sadaka kwa ajili ya dhambi zetu. Yeye ndiye ambaye hakutenda dhambi. Alifanya hivi ili tuweze kufanyika haki ya Mungu katika yeye.
Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.