< 2 Nyakati 7 >

1 Sasa Selemani alipokuwa amemaliza kuomba, moto ukaja kutoka mbinguni na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, na utukufu wa Yahwe ukaijaza nyumba.
Baada ya Solomoni kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa Bwana ukalijaza Hekalu.
2 Makuhani hawakuweza kuingia kwenye nyumba ya Yahwe, kwa sababu utukufu wake uliijaza nyumba yake.
Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la Bwana kwa sababu utukufu wa Bwana ulilijaza.
3 Watu wote wa Israeli wakaangalia juu moto uliposhuka chini na utukufu wa Yahwe ulikuwa juu ya nyumba. Wakalala kwa nyuso zao juu ya sakafu ya mawe, wakaabudu, na kutoa shukrani kwa Yahwe. Wakasema, “Kwa maana yeye ni mwema, kwa maana agano lake la kifame ladumu milele.”
Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa Bwana ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu nyuso zao mpaka chini, nao wakamwabudu na kumshukuru Bwana wakisema, “Yeye ni mwema; upendo wake unadumu milele.”
4 Kwa hiyo mfalme na watu wote wakamtolea Yahwe sadaka Yahwe.
Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana Mungu.
5 Mfalme Selemani akatoa sadaka ya ng'ombe ishirini na mbili elfu na kondoo 120, 000 na mbuzi. Kwa hiyo mfalme na watu wote wakaiweka wakifu nyumba ya Mungu.
Naye Mfalme Solomoni akatoa dhabihu ya ngʼombe 22,000 pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na watu wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mungu.
6 Makuhani wakasimama, kila mmoja akasimama mahali pake pa kuhudumu; Walawi pia pamoja na vyombo vya muziki vya Yahwe, ambavyo mfalme Daudi alivitengeza kwa ajili ya kumpa shukrani Yahwe katika nyimbo, “Kwa maana uaminifu wa agano lake wadumu milele.” Makuhani wote wakapiga matarumbeta mbele yao, na Israeli wote wakasimama.
Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao, vivyo hivyo Walawi wakiwa na vyombo vya uimbaji vya Bwana ambavyo Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza kwa ajili ya kumsifu Bwana, navyo vilitumika wakati aliposhukuru, akisema, “Upendo wake wadumu milele.” Mkabala na Walawi, makuhani walipiga tarumbeta zao, nao Waisraeli wote walikuwa wamesimama.
7 Selemani akaitakasa sehemu ya katikati ya kiwanja cha mfalme mbele ya nyumba ya Yahwe. Humo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba ambayo alikuwa ametengeza haikuweza kuzibeba sadaka, sadaka za nafaka, na za mafuta.
Solomoni akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Bwana na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba aliyokuwa ametengeneza haikutosha kuweka sadaka hizo zote za kuteketezwa, sadaka za nafaka na za mafuta.
8 Kwa hiyo Selemani akaitisha sikukuu wakati huo kwa siku saba, na Israeli wote pamaoja naye, kusanyiko kubwa, kutoka Lebo Hamathi mpaka kijito cha Misiri.
Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu wakati ule kwa muda wa siku saba, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri.
9 Siku ya nane wakaitisha kusanyiko la makini, kwa maana kwa siku saba walishika kuwekwa wakfu kwa ile madhabahu.
Katika siku ya nane walifanya kusanyiko, kwa kuwa walikuwa wanaadhimisha kuwekwa wakfu kwa madhabahu kwa muda wa siku saba na sikukuu kwa muda wa siku nyingine saba zaidi.
10 Katika siku ya ishini na tatu ya mwezi wa saba, Selemani akawatanya watu kwenda kwenye nyumba zao kwa furaha na mioyo ya shangwe kwa sababu ya wema aliokuwa ameuonesha Yahwe kwa Daudi, Selemani, Israeli, na watu wake.
Katika siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba Solomoni akawaaga watu waende nyumbani mwao, wakishangilia na kufurahi mioyoni mwao, kwa wema mwingi Bwana Mungu aliomtendea Daudi na Solomoni na kwa ajili ya watu wake Israeli.
11 Hivyo Selemani akaimaliza nyumba ya Yahwe na nyumba yake mwenyewe. Kila kitu kilichokuja katika moyo wa Selemani kwa ajili ya kukitengeneza katika nyumba ya mfalme na katika nyumba yake mwenyewe, alikitimiza kwa mafanikio.
Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, naye akiwa amefanikiwa kutenda yale yote aliyokuwa nayo moyoni mwake kufanya katika Hekalu la Bwana na katika jumba lake mwenyewe la kifalme,
12 Yahwe akamtokea Selemani usiku na kusema kwake, “Nimesikia maombi yako, na nimeichagua sehemu hii kwa ajili yangu mwenyewe kama nyumba ya dhabihu.
Bwana akamtokea Solomoni usiku na kumwambia: “Nimesikia maombi yako nami nimechagua mahali hapa kwa ajili yangu mwenyewe kuwa Hekalu kwa ajili ya dhabihu.
13 Kama nitazifunga mbingu ili kwamba kusiwepo mvua, au kama nitaamuru nzige waimeze nchi, au kama nitatuma magonjwa kati kati ya watu wangu,
“Wakati nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu,
14 kisha watu wangu, ambao wameitwa kwa jina langu, watajinyenyekeza, kuomba, kuutafuta uso wangu, na kuziacha njia zao mbaya, nitasikia kutoka mbinguni, kuwasamehe dhambi zao, na kuiponya nchi yao.
kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao.
15 Sasa macho yangu yatakuwa wazi na masikio yangu yatasikiliza maombi yanayofanywa katika sehemu hii.
Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yaombwayo mahali hapa.
16 Kwa maana sasa nimeichagua na kauitakasa nyumba hii ili kwamba jina langu lipate kuwa humo milele. Masikio yangu na moyo wangu vitakuwako kila siku.
Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili kwamba Jina langu lipate kuwa huko milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwepo huko daima.
17 Kwako wewe, kama utatembe mbele zangu kama baba yako Daudi alivyotembea, ukitii yote nilyokuamuru na kuzishika sheria zangu na maagizo yangu,
“Kwa habari yako wewe, kama ukienenda mbele zangu kama Daudi baba yako alivyoenenda na kufanya yote nikuamuruyo, nawe ukizishika amri zangu na sheria zangu,
18 basi nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyosema katika agano na Daudi baba yako, niliposema, 'Mzaliwa wako hatashindwa kamwe kuwa mtawala katika Israeli.'
Nitakiimarisha kiti chako cha enzi kama nilivyoagana na Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe mtu wa kutawala juu ya Israeli.’
19 Lakin ukigeuka, na kuzisahau sheria zangu na amri amabzo nimeweka mbele yenu, na kama utaenda kuabudu miungu wengine na kuwasujudia,
“Lakini kama ukigeuka na kuyaacha maagizo na amri nilizowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
20 basi nitawang'oa kutoka kwenye nchi yangu amabayo nimewapa. Nyumba hii ambayo nimeitakasa kwa ajili ya jina langu, nitaitupilia mbali kutoka mbele zangu, na nitaifanya kuwa methali na utani miongini mwa watu wote.
ndipo nitakapoingʼoa Israeli kutoka nchi yangu niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Nitalifanya kitu cha kudharauliwa na kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote.
21 Ingawa hekalu hili hili zuri sana kwa sasa, kila mtu apitaye karibu yake atashangazwa na ataguna. Watauliza, 'Kwa nini Yahwe ameifanyia hivi nchi hii na nyumba hii',
Ingawa Hekalu hili linavutia sana sasa, wote watakaolipita watashangaa na kusema, ‘Kwa nini Bwana amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’
22 wengine watajibu, 'Kwa sababu walimsahau Yahwe, Mungu wao, ambaye alikuwa amewatoa babu zao nje ya nchi ya Misiri, na wakashikamana na miungu wengine na kuwainamia chini na kuwaabudu. Hii ndiyo maana Yahwe ameleta majanga haya yote juu yao”
Watu watajibu, ‘Ni kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewatoa Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’”

< 2 Nyakati 7 >