< 2 Nyakati 30 >

1 Hzekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda, na pia akawaandikia barua Efraimu na Manase, kwamba waje kwenye nyumba ya Yahwe katika Yerusalemu, kusherekea Pasaka ya Yahwe, Mungu wa Israeli.
Hezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Bwana huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Bwana, Mungu wa Israeli.
2 Kwa maana mfalme, viongozi wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walikuwa wameshauriana pamoja, wakakubaliana kusherekea Pasaka katika mwezi wa pili.
Mfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili.
3 Hawakuweza kuisherekea mapema kabla ya hapo, kwa sababu hapakuwa na makuhani wa kutosha waliojitakasa wenyewe, wala watu hawakuwa wamekusanyika pamoja Yerusalemu.
Kwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa idadi ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida.
4 Pendekezo hili likaonekana sahihi katika macho ya mfalme na ya kusanyiko lote.
Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote.
5 Kwa hiyo wakakubaliana kufanya tangazo katika Israeli yote, kuanzia Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu lazima waje kusherehekea Paska ya Yahwe, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu. Kwa maana walikuwa hawakuwa wameisherehekea kwa hesabu kubwa ya watu, kwa mujibu wa jinsi ilivyokuwa imeandikwa.
Wakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Bwana, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.
6 Hivyo matarishi wakaenda na barua kutoka kwa mfalme na viongozi wake katika Israeli na Yuda yote, kwa agizo la mfalme. wakasema, “Ninyi watu wa Israeli, rudini kwa Yahwe, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, ili kwamba aweze kuwarudia masalia wenu ninyi mlipona kutoka kwenye mkono wa wafalme wa Ashuru.
Kwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema: “Watu wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7 Msiwe kama babu zenu au ndugu zenu, ambao walimuasi Yahwe, Mungu wa mababu zao, hivyo akawaweka katika kuangamia, kama mnavyoona.
Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona.
8 Sasa msiwe wasumbufu, kama babu zenu walivyokuwa; badala yake, jitoeni wenyewe kwa Yahwe na njoeni kwenye sehemu yake takatifu, ambayo ameitakasa milele, na mwabuduni Yahwe Mungu wenu, ili kwamba uso wake wenye hasira uwageukie mbali.
Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Bwana. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Bwana Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi.
9 Kwa maana ikiwa mtageuka nyuma kwa Yahwe, ndugu zenu na watoto wenu watapata huruma mbele ya hao wanaowaongoza kama wafungwa, na watarudi katika nchi hii. Kwa maana Yahwe Mungu wenu, ni mkarimu na mwenye huruma, na hatawageuzia mbali uso wake, kama mtarudi kwake.”
Kama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”
10 Kwa hiyo matarishi wakapita mji kwa mji katika majimbo ya Efraimu na Manase, njia yote hadi Zabuloni, lakini watu waliwacheka na kuwazomea.
Matarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika mpaka Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki.
11 Lakini, watu wengine wa Asheri na Manase na Zabuloni walijinyenyekesha wenyewe na wakaja Yerusalemu.
Lakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu.
12 Mkono wa Mungu pia ukaja juu ya Yuda, kuwapa moyo mmmoja, ili kulikubali agizo la mfalme na viongozi kwa neno la Yahwe.
Pia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno la Bwana.
13 Watu wengi, kusanyiko kubwa, likakusanyika Yerusalemu kusherehekea Sikukuu ya Mikate Isiyochacha katika mwezi wa pili.
Basi umati mkubwa wa watu ukakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili.
14 Waliinuka na kuchukua madhabahu zizilizokuwa Yerusalemu, madhabahu zote kwa ajili ya sadaka za kufukiza; wakazirusha katika kijito Kidroni.
Wakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakayaondoa pia yale madhabahu ya kufukizia uvumba kwa miungu na kuyatupa Bonde la Kidroni.
15 Kisha wakamuua mwanakondoo wa Paska katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi wakaona aibu, kwa hiyo wakajitakasa wenyewe na kuleta sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Yahwe.
Kisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu la Bwana.
16 Wakasimama katika sehemu zao katika makaundi yao, wakifuata maelekezo yaliyotolewa na sheria ya Musa, mtu wa Mungu. Makuhani wakainyunyiza damu waliyoipokea kutoka kwenye mikono ya Walawi.
Kisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi.
17 Kwa maana walikuwepo wengi katika kusanyikao amaabao hawakuwa wamejitakasa wenyewe. Kwa hiyo Makuhani wakamchinja mwanakondoo wa Pasaka kwa ajili ya kila mmoja ambaye hakuwa amejisafisha na hakuweza kuzitakasa sadaka zake kwa Yahwe.
Kwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa safi, kwa kufuata taratibu za ibada ili kuwatakasa kwa Bwana.
18 Kwa kuwa wingi wa watu, wengi wao kutoka Efraimu na Manase, Asakari na Zabuloni, hawakuwa wamejitakasa wenyewe, bado waliula mlo wa Paska, kinyume na maelekezo yaliyoandikwa. Kwa kuwa Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, “Mungu Yahwe amsamehe kila mmoja
Ingawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Bwana, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja
19 ambaye anaulekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Yahwe, Mungu wa babu zake, hata kama hajasafiswa kwa utakaso wa viwango vya patakatifu.”
ambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.”
20 Kwa hiyo Yahwe akamsikiliza Hezekia na akawaponya watu.
Naye Bwana akamsikia Hezekia akawaponya watu.
21 Watu wa Israeli waliokuwepo Yerusalemu wakaitunza Sikukuu ya Mikaate Isiyochachwa na furaha kubwa kwa siku saba. Walawi na makuhani wakamsifu Yahwe siku baada ya siku, wakiimwimbia Yahwe kwa vyombo vya sauti kuu.
Waisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba, nao Walawi na makuhani walikuwa wakiimba kila siku, wakiwa na ala za uimbaji za kumsifu Bwana.
22 Hezekia akazungumza kwa kuwatia moyo Walawi wote walioilewa ibada ya Yahwe, Kwa hiyo wakala kwa kipindi cha siku saba, wakitoa sadaka za amani, na kufanya toba kwa Yahwe, Mungu wa babu zao.
Hezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionyesha ustadi katika kumtumikia Bwana. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa sadaka za amani na kumshukuru Bwana, Mungu wa baba zao.
23 Kusanyiko lote kisha likaamua kusherehekea kwa siku zingine saba, na wakafanya hivyo kwa furaha.
Kisha kusanyiko lote likakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi, kwa hiyo kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha.
24 Kwa kuwa Hezekia mfalme wa Yuda aliwapa kusanyiko ng'ombe dume elf moja, na kondoo elfu saba kama sadaka; na viongozi wakawapa kusanyiko ng'ombe dume elfu moja na kondoo na mbuzi elfu kumi. Idadi kubwa ya makuhani wakajitakasa wenyewe.
Hezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali 1,000, kondoo na mbuzi 7,000 kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali 1,000 pamoja na kondoo na mbuzi 10,000. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu.
25 Kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na watu wote walikuja pamoja kutoka nchi ya Israeli na wale walioishi Yuda—wote wakafurahia.
Kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na lile kusanyiko lote lililotoka Israeli, pamoja na wale wageni waliotoka Israeli na wale walioishi katika Yuda wakafurahi.
26 Hivyo kulikuwa na furaha kuu katika Yerusalemu, kwa kuwa tangu wakati wa Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hapakuwa na kitu kama hicho katika Yerusalemu.
Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Solomoni mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwepo jambo kama hili katika Yerusalemu.
27 Kisha makuhani, Walawi, wakainuka na kuwabariki watu. Sauti zao zilisikika na maombi yao yakaenda juu mbinguni, sehemu takatifu ambapo Mungu anaishi.
Ndipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.

< 2 Nyakati 30 >