< 1 Timotheo 5 >
1 Usimkemee mwanamume mzee. Bali mtiye moyo kama baba yako. Uwatiye moyo vijana wa kiume kana kwamba ni ndugu zako.
2 Uwatiye moyo wanawake wazee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako kwa usafi wote.
3 Waheshimu wajane, wale walio wajane kweli kweli.
4 Lakini kama mjane ana watoto au wajukuu, waache kwanza wajifunze kuonesha heshima kwa watu wa nyumbani mwao wenyewe. Waache wawalipe wazazi wao mema, kwa kuwa hii inapendeza mbele za Mungu.
5 Lakini mjane kweli kweli ni yule aliyeachwa peke yake. Naye huweka tegemeo lake kwa Mungu. Siku zote hudumu katika sala na maombi usiku na mchana.
6 Hata hivyo, mwanamke yule aishiye kwa anasa amekufa, ingawaje yu hai.
7 Na uyahubiri haya mambo ili kwamba wasiwe na lawama.
8 Ila kama mtu asipowatunza ndugu zake, hususani wale walioko nyumbani mwake, ameikana imani na ni mmbaya kuliko mtu asiye amini.
9 Basi mwanamke aandikishwe kwenye orodha kama mjane akiwa na umri usiopungua miaka sitini, na ni mke wa mume mmoja.
10 Lazima awe amejulikana kwa matendo mema, ikiwa ni kwamba amewajali watoto, au ameshakuwa mkarimu kwa wageni, au ameosha miguu ya waaminio, au alimesaidia ambao wamekuwa wakiteswa, au alijitoa kwa kazi yeyote njema.
11 Lakini kwa wale wajane vijana, kataa kuwaandikisha kwenye orodha ya wajane. Kwa kuwa wakiingia kwenye matamanio ya kimwili dhidi ya Kristo, wanataka kuolewa.
12 Kwa njia hii huingia kwenye hatia kwa kuwa huvunja kujitoa kwao kwa awali.
13 Na pia huingia kwenye mazoea ya uvivu. Wao huzunguka nyumba kwa nyumba. Si tu kwamba ni wavivu, bali pia huwa wasengenyaji na na wenye kuingilia mambo ya wengine. Wao husema mambo wasiyopaswa kuyasema.
14 Kwa hiyo mimi nataka wanawake vijana waolewe, wazae watoto, wasimamie nyumba zao, ili kutokumpa adui nafasi ya kutushitaki kwa kufanya dhambi.
15 Kwa sababu baadhi yao wameshamgeukia Shetani.
16 Kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane, basi na awasaidie, ili kanisa lisilemewe, ili liweze kuwasaidia wale walio wajane kweli kweli.
17 Basi wazee wale watawalao vyema wahesabiwe kuwa wamestahili heshima maradufu, hasa wale wanaojishughulisha na kufundisha neno la Mungu.
18 Kwa kuwa maandiko yanasema, “Usimfumbe ng'ombe kinywa apulapo nafaka,” na “Mfanya kazi anastahili mshahara wake.”
19 Usipokee mashitaka dhidi ya mzee isipokuwa kuna mashahidi wawili au watatu.
20 Waonye wakosaji mbele ya watu wote ili wengine waliobaki labda wataogopa.
21 Nakuagiza kwa dhati mbele ya Mungu, na mbele ya Kristo Yesu, na malaika wateule, kwamba uzitunze maagizo haya bila ubaguzi wowote, na kwamba usifanye jambo lolote kwa upendeleo.
22 Usimwekee mtu yeyote mikono haraka. Usishiriki dhambi ya mtu mwingine. Yakupasa kujitunza mwenyewe uwe usafi.
23 Hakupasi kunywa maji pekee. Badala yake, unywe mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo na magonjwa yako ya mara kwa mara.
24 Dhambi za baadhi ya watu hujulikana kwa uwazi, na huwatangulia hukumuni. Lakini baadhi ya dhambi hufuata baadaye.
25 Vivyo hivyo, baadhi ya kazi njema hujulikana kwa uwazi, lakini hata zingine hazitafichika.