< 1 Timotheo 4 >
1 Sasa Roho anasema waziwazi kwamba katika nyakati zijazo baadhi ya watu wataiacha imani na kuwa makini kusikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya kipepo yatakayofundishwa
2 katika uongo na unafiki. Dhamiri zao zitabadilishwa.
3 Watawazuia kuoa na kupokea vyakula ambavyo Mungu aliviumba vitumiwe kwa shukrani miongoni mwao waaminio na wenye kuijua kweli.
4 Kwa sababu kila kitu ambacho Mungu amekiumba ni chema. Hakuna ambacho tunapokea kwa shukrani kinastahili kukataliwa.
5 Kwa sababu kinatakaswa kupitia neno la Mungu na kwa njia ya maombi.
6 Kama utayaweka mambo haya mbele ya ndugu, utakuwa mtumishi mzuri wa Yesu Kristo. Kwa sababu umestawishwa kwa maneno ya imani na kwa mafundisho mazuri ambayo umeyafuata.
7 Lakini zikatae hadithi za kidunia ambazo zinapendwa na wanawake wazee. Badala yake, jifunze mwenyewe katika utaua.
8 Kwa maana mazoezi ya mwili yafaa kidogo, bali utauwa wafaa sana kwa mambo yote. Hutunza ahadi kwa maisha ya sasa na yale yajayo.
9 Ujumbe huu ni wakuaminiwa na unastahili kukubaliwa kabisa.
10 Kwa kuwa ni kwa sababu hii tunataabika na kufanya kazi kwa bidii sana. Kwa kuwa tunao ujasiri katika Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, lakini hasa kwa waaminio.
11 Uyaseme na kuyafundisha mambo haya.
12 Mtu yeyote asiudharau ujana wako. Badala yake, uwe mfano kwa wote waaminio, katika usemi, mwenendo, upendo, uaminifu, na usafi.
13 Mpaka nitakapokuja, dumu katika kusoma, katika kuonya, na katika kufundisha.
14 Usiipuuze karama iliyomo ndani yako, ambayo ulipewa kupitia unabii, kwa kuwekewa mikono na wazee.
15 Uyajali mambo haya. Ishi katika hayo ili kukua kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Zingatia sana mwenendo wako na mafundisho.
16 Dumu katika mambo haya. Maana kwa kufanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.