< 1 Timotheo 3 >
1 Usemi huu ni wakuaminika: Kama mtu anatamani kuwa Msimamizi, anatamani kazi njema.
Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri.
2 Kwa hiyo msimamizi ni lazima asiwe na lawama. Ni lazima awe mume wa mke mmoja. Ni lazima awe na kiasi, busara, mwenye utaratibu, mkarimu. Ni lazima awe uwezo wa kufundisha.
Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha,
3 Asiwe anatumia mvinyo, asiwe mgomvi, bali mpole, mwenye amani. Ni lazima asiwe mwenye kupenda fedha.
asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.
4 Inampasa kuwasimamia vema watu wa nyumbani mwake mwenyewe, na watoto wake imewapasa kumtii kwa heshima zote.
Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia.
5 Maana ikiwa mtu hajui kuwasimamia watu wa nyumbani mwake mwenyewe, atalileaje kanisa la Mungu?
(Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)
6 Asiwe mwamini mpya, ili kwamba asije akajivuna na kuanguka katika hukumu kama yule mwovu.
Asiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi.
7 Lazima pia awe na sifa njema kwa wote walioko nje, ili asije akaanguka kwenye aibu na mtego wa mwovu.
Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.
8 Mashemasi, vilevile wanapaswa kuwa wenye kustahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili. Wasitumie mvinyo kupita kiasi au kuwa na tamaa.
Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.
9 Waweze kuitunza kwa dhamiri safi ile kweli ya imani iliyofunuliwa.
Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi.
10 Wawe pia wamethibitishwa kwanza, halafu waweze kuhudumu kwa sababu hawana lawama.
Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.
11 Wanawake vivyo hivyo wawe wenye heshima. Wasiwe wasingiziaji. Wawe na kiasi na waaminifu kwa mambo yote.
Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.
12 Mashemasi ni lazima wawe waume wa mke mmoja mmoja. Lazima waweze kuwasimamia vema watoto wao na wa nyumbani mwao.
Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.
13 Kwa kuwa wale wanaotumika vizuri hupata msimamo mzuri na ujasiri mkubwa katika imani iliyo katika Kristo Yesu.
Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.
14 Ninaandika mambo haya kwako, na ninatumaini kuja kwako hivi karibuni.
Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba,
15 Lakini ikiwa nitachelewa, ninaandika ili upate kujua namna ya kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambalo ni kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msaada wa kweli.
kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.
16 Na haipingiki kwamba kweli ya Uungu uliyofunuliwa ni mkuu: “Alionekana katika mwili, akathibitishwa na Roho, akaonekana na malaika, akatangazwa miongoni mwa mataifa, akaaminiwa na ulimwengu, na akachukuliwa juu katika utukufu.”
Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa: Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu, akathibitishwa kuwa na haki katika Roho, akaonekana na malaika, akahubiriwa miongoni mwa mataifa, akaaminiwa ulimwenguni, akachukuliwa juu katika utukufu.