< 1 Wathesalonike 1 >
1 Paulo, Silwano na Timotheo kwa kanisa la Wathesalonike katika Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. Neema na amani iwe nanyi.
Paulo, Silvano na Timotheo: Kwa kanisa la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu Baba yetu na ndani ya Bwana Yesu Kristo: Neema iwe kwenu na amani.
2 Tunatoa shukrani kwa Mungu kila mara kwa ajili yenu nyote, wakati tunapowataja katika maombi yetu.
Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima.
3 Tunaikumbuka bila kukoma mbele ya Mungu na baba yetu kazi yenu ya imani, juhudi ya upendo, na uvumilivu wenye ujasiri kwa ajili ya baadaye katika Bwana Yesu Kristo.
Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo.
4 Ndugu Mnaopendwa na Mungu, tunajua wito wenu.
Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua,
5 Na jinsi injili yetu ilivyokuja kwenu si kwa neno tu, bali pia katika nguvu, katika Roho Mtakatifu, na katika uhakika. Kwa namna hiyo, mnajua pia sisi tulikuwa watu wa namna gani miongoni mwenu kwa ajili yenu.
kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda katikati yenu kwa ajili yenu.
6 Mlikuwa watu wa kutuiga sisi na Bwana, kama mlivyopokea neno katika taabu kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.
Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu.
7 Na matokeo yake, mkawa mfano kwa wote katika Makedonia na Akaiya ambao wanaamini.
Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya.
8 Kwa kuwa kutoka kwenu neno la Mungu limeenea kote, na si kwa Mekadonia na Akaiya peke yake. Badala yake, kwa kila mahali imani yenu katika Mungu imeenea kote. Na matokeo yake, hatuhitaji kusema chochote.
Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali kiasi kwamba hatuna haja ya kusema lolote kwa habari yake.
9 Kwa kuwa wao wenyewe wanaarifu ujio wetu ulikuwa wa namna gani kati yenu. Wanasimulia jinsi mulivyomgeukia Mungu kutoka katika sanamu na kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli.
Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli
10 Walitoa habari kuwa mnamsubiri Mwana wake kutoka mbinguni, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu. Na huyu ni Yesu, anayetuweka huru kutoka kwenye ghadhabu ijayo.
na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani, Yesu, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.