< 1 Wathesalonike 5 >
1 Sasa, kwa habari ya muda na nyakati, ndugu, hamna haja kwamba kitu chochote kiandikwe kwenu.
2 Kwa kuwa ninyi wenyewe mwajua kwa usahihi ya kuwa siku ya Bwana inakuja kama mwizi ajapo usiku.
3 Pale wasemapo kuna “Amani na usalama”, ndipo uharibifu huwajia ghafla. Ni kama utungu umjiavyo mama mwenye mimba. Hawataepuka kwa njia yeyote.
4 Lakini ninyi, ndugu hampo kwenye giza hata ile siku iwajie kama mwizi.
5 Kwa maana ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi siyo wana wa usiku au wa gizani.
6 Hivyo basi, tusilale kama wengine walalavyo. Bali tukeshe na kuwa makini.
7 Kwa kuwa wanaolala hulala usiku na wanao lewa hulewa usiku.
8 Kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, tuwe makini. Tuvae ngao ya imani na upendo, na, kofia ya chuma, ambayo ni uhakika wa wokovu wa wakati ujao.
9 Kwa kuwa Mungu hakutuchagua mwanzo kwa ajili ya gadhabu, bali kwa kupata wokovu kwa njia ya Bwana Yesu Kristo.
10 Yeye ndiye aliyetufia ili kwamba, tukiwa macho au tumelala, tutaishi pamoja naye.
11 Kwa hiyo, farijianeni na kujengana ninyi kwa ninyi, kama ambavyo tayari mnafanya.
12 Ndugu, twawaomba muwatambue wale wanaotumika miongoni mwenu na wale walio juu yenu katika Bwana na wale wanao washauri.
13 Tunawaomba pia muwatambue na kuwapa heshima katika upendo kwa sababu ya kazi yao. Muwe na amani miongoni mwenu ninyi wenyewe.
14 Twawasihi, ndugu: muwaonye wasio kwenda kwa utaratibu, watieni moyo walio kata tamaa, Wasaidieni walio wanyonge, na muwe wavumilivu kwa wote.
15 Angalieni asiwepo mtu yeyote anayelipa baya kwa baya kwa mtu yeyote. Badala yake, fanyeni yaliyo mema kwa kila mmoja wenu na kwa watu wote.
16 Furahini siku zote.
17 Ombeni bila kukoma.
18 Mshukuruni Mungu kwa kila jambo, kwa sababu hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwenu katika Yesu Kristo.
19 Msimzimishe Roho.
20 Msiudharau unabii.
21 Yajaribuni mambo yote. Mlishike lililo jema.
22 Epukeni kila mwonekano wa uovu.
23 Mungu wa amani awakamilishe katika utakatifu. Roho, nafsi na mwili vitunzwe pasipo mawaa katika kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu, naye ndiye mwenye kutenda.
25 Ndugu, tuombeeni pia.
26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.
27 Nawasihi katika Bwana kwamba barua hii isomwe kwa ndugu wote.
28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.