< 1 Samweli 1 >

1 Palikuwa na mtu mmoja wa Rama Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu; jina lake aliitwa Elikana mwana Yerohamu mwana Elihu mwana wa Tohu mwana wa Sufu, Mwefraimu.
Kulikuwepo na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ambaye jina lake aliitwa Elikana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu.
2 Mtu huyo alioa wanawake wawili, jina la mke wa kwanza aliitwa Hana, na yule wa pili aliitwa Penina, Penina alizaa watoto, lakini Hana hakuzaa.
Alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto.
3 Kila mwaka, mtu huyu aliondoka mjini kwake kwenda kuabudu na kutoa dhabihu kwa BWANA wa majeshi huko Shilo. Wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa BWANA, walikuwepo huko Shilo.
Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Bwana.
4 Kila mwaka zamu ya Elikana ya kutoa dhabihu ilipofika, alikuwa daima akimpa sehemu ya nyama Penina mkewe, watoto wake wote wa kiume na wakike
Kila mara ilipofika siku ya Elikana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote pamoja na binti zake.
5 Lakini kwa mgawo wa Hana daima alimpa mara mbili zaidi, kwa sababu alimpenda Hana, ingawa BWANA alikuwa amelifunga tumbo lake.
Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo.
6 Hasimu wake alimchokoza sana ili kumkasilisha, kwa sababu BWANA alikuwa amelifunga tumbo lake. 8
Kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi.
7 Hivyo kila mwaka, alipokuwa akienda katika nyumba ya BWANA pamoja na familia yake, hasimu wake alizidi kumchokoza, Hatimaye alikuwa mtu wa kulia kila wakati na hakula kitu chochote.
Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda katika nyumba ya Bwana, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha mpaka analia na kushindwa kula.
8 Elikana mmewe kila wakati alimuuliza, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli chakula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Mimi sibora kwako kuliko wana kumi?
Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”
9 Wakati fulani, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alinyanyuka. Wakati huo Eli, kuhani alikuwa amekaa juu ya kiti chake mlangoni kuelekea nyumba ya BWANA.
Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la Bwana.
10 Hana alijawa na uchungu sana; akamwomba BWANA na akalia mno.
Kwa uchungu wa rohoni Hana alilia sana na akamwomba Bwana.
11 Aliweka nadhili na kusema, “BWANA wa majeshi, kama utalitazama teso la mjakazi wako na kunikumbuka, na usipomsahau mjakazi wako, na kumpatia mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo nitamtoa huyo mtoto kwa BWANA siku zote za maisha yake, na wembe hautapita juu ya kichwa chake kamwe”.
Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa Bwana kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”
12 Hana kiendelea kuomba mbele za BWANA, Eli alikitazama kinywa chake.
Alipokuwa anaendelea kumwomba Bwana, Eli alichunguza kinywa chake.
13 Hana aliongea moyoni mwake. Midomo yake ilitikisika, lakini sauti yake haikusikika. Hivyo Eli alimdhania kuwa amelewa.
Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa
14 Eli akamwambia, “Utakuwa mlevi mpaka lini? Weka mbali divai yako.”
naye akamwambia, “Utaendelea kulewa mpaka lini? Achilia mbali mvinyo wako.”
15 Hana akajibu, “Sivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni. Sijanywa divai wala kinywaji chochote cha kulevya, bali nimekuwa nikiimimina nafsi yangu mbele za BWANA.”
Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Bwana.
16 Usimchukulie mjakazi wako kama mwanamke duni; nimekuwa nikiongea kutokana na maumivu na masikitiko yangu.” 18
Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa katika wingi wa uchungu mkuu na huzuni.”
17 Kisha Eli alimjibu na kusema, “Nenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akupatie kile ulichomuomba.”
Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.”
18 Hana akasema, “Na mjakazi wako apate kibali machoni pako.” Ndipo huyo mwanamke alienda zake na kula chakula na hakuhuzunika tena.
Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.
19 Waliamka asubuhi na mapema wakaenda wakamtukuza BWANA, na baadaye walirudi nyumbani kwao Rama. Elikana alilala na mke wake Hana, na BWANA akamkumbuka.
Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za Bwana na kisha wakarudi nyumbani kwao huko Rama. Elikana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye Bwana akamkumbuka.
20 Baada ya muda fulani, Hana alibeba mimba na akazaa mtoto wa kiume. Akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa sababu huyu nilimuomba kutoka kwa BWANA.”
Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa Bwana.”
21 Mara nyingine, Elikana na nyumba yake, walipanda kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya Mwaka na kuondoa nadhiri yake.
Wakati huyo mtu Elikana alipanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa Bwana na kutimiza nadhiri yake,
22 Lakini Hana hakwenda huko; alikuwa amekwisha mwambia mmewe, “Sitaenda huko hadi mtoto aache kunyonya; ndipo nitamleta, ili ahudhurie mbele za BWANA na akae huko daima.”
Hana hakwenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za Bwana, naye ataishi huko wakati wote.”
23 Mme wake Hana, Elikana, akamwambia, “Fanya yale yakupendezayo. Ngojea hadi utakapokuwa umemwachisha kunyonya; BWANA aweze peke yake kuthibitisha neno lake.” Hivyo yule mwanamke alibaki akimnyonyesha mtoto wake mpaka pale alipomwachisha ziwa.
Elikana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa mpaka utakapomwachisha kunyonya, Bwana na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe mpaka alipomwachisha kunyonya.
24 Alipokuwa amemwachisha kunyonya, alimbeba, akimchukua pamoja ng'ombe dume wa miaka mitatu, unga kama kilo thelathini na chupa ya mvinyo, akampeleka katika nyumba ya BWANA huko Shilo. Na mtoto huyo alikuwa bado mdogo.
Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya Bwana huko Shilo.
25 Walimchinja yule ng'ombe, na wakamkabidhi mtoto kwa Eli.
Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli,
26 Akasema, “Ee bwana wangu! Kama uishivyo, bwana wangu, Mimi ndiye yule mwanamke niliyesimama hapa karibu nawe nikimwomba BWANA.
naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Bwana.
27 Niliomba kwa ajili ya mtoto huyu na BWANA akawa amenijibu ombi la dua yangu nililomwomba.
Niliomba mtoto huyu, naye Bwana amenijalia kile nilichomwomba.
28 Nami nimemtoa kwa BWANA; kwa maisha yake yote, nimempa BWANA.” Ndipo Elikana na familia yake wakamtukuza BWANA huko Shilo.
Hivyo sasa ninamtoa kwa Bwana. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Bwana.” Naye akamwabudu Bwana huko.

< 1 Samweli 1 >