< 1 Samweli 9 >
1 Basi kulikuwa na mtu mmoja kutoka Benyamini, mtu mashuhuri. Jina lake aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Zerori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini.
Kulikuwako Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini.
2 Huyu alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Sauli, kijana mzuri wa uso. Hapakuwapo mwanaume mzuri wa uso kuliko huyu miongoni mwa watu wote wa Israeli. Kutoka mabegani kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wengine.
Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana anayevutia sana, hakuwepo aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli, alikuwa mrefu kuliko wengine wote.
3 Na punda wa Kishi, baba yake na Sauli walipotea. hivyo Kishi akamwambia Sauli mwanawe, “Mchukue mmoja wa watumishi; uamke uende kuwatafuta punda,”
Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.”
4 Sauli akapita katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu na akaenda akapita katika nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona. Kisha walipita katika nchi ya Shaalimu, lakini hawakuwa huko. Baadaye alipita katika nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwaona wale punda.
Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwepo huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata.
5 Na walipofika nchi ya Sufu, Sauli alimwambia mtumishi wake aliyekuwa naye, “Njoo na turudi, pengine baba aweza kuacha kuchunga punda na kuanza kutuhofia sisi.”
Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo, sisi na turudi, au baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda na kuanza kufadhaika kutuhusu sisi.”
6 Lakini mtumishi akamwmbia, “Sikiliza, Yupo mtu wa Mungu katika mji huu. Naye ni mtu wa kuheshimiwa sana; kila asemalo huwa kweli. Hebu twende huko; labda anaweza kutuambia tupitie wapi katika safari yetu.”
Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho hutokea kweli. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.”
7 Ndipo Sauli akamwambia mtumish iwake, “Lakini kama tukienda kwake, twaweza kumpelekea nini? Maana hata mkate katika mfuko wetu umekwisha, na hakuna zawadi ya kumpelekea mtumishi wa Mungu. Tuna kitu gani?
Sauli akamwambia mtumishi wake, “Kama tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?”
8 Huyo mtumishi akamjibu Sauli na kusema, “Hapa, ninayo robo ya shekeli ya fedha ambayo nitampa mtumishi wa Mungu, atuambie ni njia ipi yatupasa tuiendee.”
Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli. Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia twende kwa njia ipi.”
9 (Zamani katika Israeli, mtu alipotaka kujua neno kuhusu mapenzi ya Mungu, alisema, “Njoo, haya twende kwa mwonaji.” Kwa maana nabii wa leo, zamani aliitwa Mwonaji).
(Zamani katika Israeli, kama mtu alikwenda kuuliza neno kwa Mungu, angalisema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.)
10 Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, “Umesema vyema. Haya, njoo twende.” Basi wakaenda katika mji ambao mtu wa Mungu alikuwamo.
Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwepo huyo mtu wa Mungu.
11 Walipopanda mlima kuelekea mjini, walikutana na wasichana wakienda kuteka maji; Sauli na mtumishi wake wakawauliza, “Mwonaji hupo hapa?”
Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wanakuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?”
12 Nao wakawajibu, na kusema, “Yupo; tazameni, yuko mbele yenu. Harakisheni, kwa maana anakuja mjini leo, sababu leo watu wanatoa dhabihu zao mahali pa juu.
Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu.
13 Mara tu mtakapoingia mjini mtamuona, kabla hajapanda mahali pa juu kla chakula. Watu hawatakula hata atakapokuja, kwa sababu ndiye ataibariki dhabihu; na baadaye wale ambao wamealikwa hula. Basi pandeni, mtamuona sasa hivi.”
Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula. Watu hawataanza kula mpaka atakapofika kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”
14 Kwa hiyo walikwea kwenda mjini. Walipokuwa wakiingia mjini, walimuona Samweli akija mbele yao, akipanda kwenda mahali pa juu.
Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikokwenda mahali pa juu.
15 Siku moja kabla Sauli hajafika, BWANA alikuwa amemfunulia Samweli:
Basi siku moja kabla Sauli hajaja, Bwana alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili:
16 “Kesho wakati kama huu nitakutumia mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe utamtia mafuta awe mfalme juu ya watu wangu Israeli. Atawaokoa watu wangu kutoka mkono wa Wafilisti. Kwa kuwa nimewaonea huruma watu wangu na kilio cha kutaka msaada kimenifikia.”
“Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umtie mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli, ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”
17 Samweli alipomuona Sauli, BWANA akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekwambia habari zake! Yeye ndiye atakayewatawala watu wangu.”
Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”
18 Ndipo Sauli akaja karibu na Samweli katika lango na kusema, “Niambie nyumba ya Mwonaji iko wapi?
Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, waweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”
19 Samweli akamjibu Sauli akisema, “Mimi ndiye mwonaji. Tangulia mbele hadi mahali pa juu, nami nitakueleza kila kitu kilichomoyoni mwako.
Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu mpaka mahali pa juu, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako.
20 Kama punda wenu waliopotea siku tatu zilizopita, msihofu kuhusu hao punda, kwa kuwa wamekwishapatikana. Na yote yaliyotamanika kwa ajili ya Israeli yanamwangukia nani? Siyo kwako na nyumba ya baba yako yote?”
Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”
21 Sauli akamjibu na kusema, Siyo mimi Mbenyamini, kutoka kabila lililo dogo sana kwa makabila ya Israeli? Siyo ukoo wangu ulio mdogo sana kwa kabila la Benyamini? Kwa nini basi unaniambia kwa namna hii?”
Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo la namna hiyo?”
22 Hivyo Samweli akamchukua Sauli na mtumishi wake, akawaingiza ukumbini, akawakalisha mahali pa heshima pa wale walioalikwa, idadi yao takribani watu thelathini.
Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ndani ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini.
23 Samweli akamwambia mpishi, “Lete sehemu niliyokupatia, sehemu ambayo nilikwambia hivi, “Itenge.”'
Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.”
24 Basi mpishi alichukua paja lililokuwa limeinuliwa katika dhabihu na kile kilichokuwa pamoja nalo, akaitenga mbele ya Sauli. Kisha Samweli akasema, “Angalia kile kilichokuwa kimetunzwa kwa ajili yako! Kula, kwa sababu kilitunzwa hadi wakati maalum ufike kwa ajili yako. Na kwa sasa waweza kusema, 'Nimewaalika watu.”' Kwa hiyo Sauli alikula pamoja na Samweli siku hiyo.
Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile.
25 Walipokuwa wamekwisha shuka chini kutoka sehemu ya juu na kuingia mjini, Samweli akazungumza na Sauli darini.
Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake.
26 Na kulipopambazuka, Samweli alimwita Sauli darini na kusema, “Amka, kusudi nikusindikize uende zako,” Hivyo Sauli aliamka, na wote wawili, yeye na Samweli walitoka kwenda mtaani.
Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja.
27 Walipokuwa wakienda nje ya viunga vya mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi wako atanguliye mbele yetu(na alitangulia mbele), Lakini wewe sharti usubiri kidogo, nipate kukuambia ujumbe wa Mungu.”
Hata walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Lakini subiri hapa kwa kitambo kidogo, ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.”