< 1 Samweli 5 >
1 Basi Wafilisti wakawa wamelitwaa sanduku la Mungu, wakalileta kutoka Ebenezeri hadi Ashdodi.
Baada ya Wafilisti kuteka Sanduku la Mungu, walilichukua kutoka Ebenezeri mpaka Ashdodi.
2 Wafilisti walilichukua sanduku la Mungu, wakalileta ndani ya nyumba ya Dagoni, na wakalikalisha pembeni mwa Dagoni.
Kisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni.
3 Watu wa Ashdodi walipoamka mapema siku ya pili, tazama, Dagoni ilianguka chini kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA. Hivyo waliichukua Dagoni na kuisimamisha tena katika sehemu yake.
Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake, kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake.
4 Lakini walipoamka mapema kesho yake, tazama, Dagoni alikuwa ameanguka chini kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA. Kichwa cha Dagoni na vitanga vyake miwili vilikatika na kulala mlangoni. Kiwiliwili cha Dagoni ndicho kilibaki tu.
Lakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta huyo Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa navyo vimelala kizingitini, ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki.
5 Na hii ndiyo sababu, makuhani wa Dagoni na yeyote aingiae ndani ya nyumba ya Dagoni, hata leo, hawezi kukanyaga mlango wa Dagoni katika Ashdodi.
Ndiyo sababu mpaka leo makuhani wa Dagoni wala wengine waingiao katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti.
6 Mkono wa BWANA ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi. Aliwaangamiza akawatesa kwa majipu, Ashdodi na wilaya zake kwa pamoja.
Mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu.
7 Watu wa Ashdodi walipotambua kilichokuwa kinatokea, walisema, “Sanduku la Mungu wa Israeli lisikae kwetu, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya mungu wetu Dagoni.”
Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.”
8 Basi wakawatuma watu wawakusanye pamoja viongozi wote wa Wafilisti; wakawambia, “Tufanye nini na sanduku la Mungu wa Israeli?” Wakawajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli lihamishwe na kupelekwa Gathi.” Basi wakalihamisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli hadi huko Gathi.
Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?” Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.
9 Lakini baada ya kulipeleka huko, mkono wa BWANA ulikuwa juu ya mji huo, ukasababisha machafuko makubwa. Akawatesa watu wa mji huo, wakubwa kwa wadogo; na majipu yakaota juu ya miili yao.
Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu.
10 Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu hadi Ekroni. Lakini mara tu sanduku la Mungu lilipoingia Ekroni, watu wa Ekroni walipiga kelele wakisema, “Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli kutuua sisi na watu wetu.”
Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni. Wakati Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.”
11 Basi wakawatuma watu wawakusanye pamoja viongozi wote wa Wafilisti; wakawambia, “Lipelekeni mbali sanduku la Mungu wa Israeli, na lirudishwe katika makao yake, ili lisije kutuua sisi na watu wetu.” Kwa maana kulikuwa na hofu ya kutisha mjini mwote; Mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko.
Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake.
12 Watu ambao hawakufa waliteswa na majipu, na kilio cha mji kilipanda hadi mbinguni.
Wale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilikwenda juu hadi mbinguni.