< 1 Samweli 4 >
1 Neno la Samweli likawafikia Israeli wote. Basi Israeli wakatoka kupigana dhidi ya Wafilisti. Nao wakaweka kambi hapo Ebenezeri, na Wafilisti waliweka kambi yao huko Afeki.
Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote. Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki.
2 Nao Wafilisti walijipanga kwa ajili ya vita dhidi ya Waisraeli. Vita ilipopamba moto, Israeli ilishindwa na Wafilisti, wakauawa watu wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita.
Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao 4,000 kwenye uwanja wa vita.
3 Watu walipokuja kambini, wazee wa Israeli walisema, “Kwa nini BWANA ametushinda leo mbele ya Wafilisti? Hebu tulilete hapa sanduku la ushuhuda wa BWANA kutoka Shilo, ili kwamba liwe hapa pamoja nasi, ili litufanye tuwe salama kutokana na nguvu za maadui zetu.”
Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa nini Bwana ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Bwana kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu.”
4 Hivyo waliwatuma watu huko Shilo; kutokea huko walilibeba sanduku la ushuhuda wa BWANA wa majeshi, akaaye juu ya makerubi. Hofni na Finehasi, watoto wawili wa Eli, walikuwapo pamoja na lile sanduku la ushuhuda wa Mungu.
Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwako huko pamoja na Sanduku la Agano la Mungu.
5 Sanduku la ushuhuda wa BWANA lilipofika kambini, watu wote wa Israeli walipiga yowe, na nchi ikavuma.
Wakati Sanduku la Agano la Bwana lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika.
6 Wafilisti waliposikia kelele za mayowe, wakasema, “sauti hii ya mayowe katika kambi ya Waebrania inamaanisha nini?” Baadaye walitambua kwamba sanduku la BWANA limefika kambini.
Wafilisti waliposikia makelele wakauliza, “Ni nini makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?” Walipofahamu kuwa Sanduku la Bwana limekuja kambini,
7 Wafilisti waliogopa sana, “Mungu ameingia kambini.” Wakasema, “Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea huko nyuma!
Wafilisti wakaogopa, wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo.
8 Ole wetu! Ni nani atatulinda dhidi ya nguvu za Mungu mwenye uwezo? Huyu ndiye Mungu aliyewashambulia Wamisri kwa aina tofauti za mapigo mengi jangwani.
Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani.
9 Enyi Wafilisti, iweni hodari, na fanyeni kiume, vinginevyo mtakuwa watumwa wa Waebrabia, kama walivyokuwa watumwa wenu. Fanyeni kiume, na piganeni nao.”
Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!”
10 Wafilisti walipigana, na Waisraeli wakashindwa. Kila mtu alikimbilia nyumbani kwake, na mauaji yalikuwa makubwa sana; maana askari wa Israeli elfu thelathini waendao kwa miguu vitani, walianguka.
Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia hemani mwake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari 30,000 waendao kwa miguu.
11 Lile sanduku la Mungu lilichukuliwa, na watoto wa Eli, Hofni na Finehasi waliuawa.
Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.
12 Mtu mmoja wa Benjamini alikimbia kutoka uwanja wa vita akaja Shilo siku iyo hiyo, aliwasili na mavazi yake yamechanika na matope kichwani pake.
Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka kwenye uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake.
13 Alipofika, Eli alikuwa amekaa kitini pake karibu na barabara akitazama kwa sababu moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kutoa taarifa, mji wote ulilia.
Alipofika, Eli alikuwa ameketi juu ya kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia.
14 Eli aliposikia kelele ya kilio kile, alisema, “Kilio hicho kina maana gani?” Kwa haraka mtu yule alikuja na kumweleza Eli.
Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?” Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli,
15 Basi Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane; macho yake yamepofuka, na hakuweza kuona.
wakati huu Eli alikuwa na miaka tisini na minane nayo macho yake yalikuwa yamepofuka na hakuweza kuona.
16 Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi ndiye nimechomoka kutoka vitani. Nimetoroka kutoka kwenye mapigano leo.” Eli akasema, “Mambo yalienda namna gani, mwanangu?”
Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko leo hii.” Eli akamuuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?”
17 Yule mtu aliyeleta hizo habari alijibu na kusema, “Israeli wamewakimbia Wafilisti. Pia watu wengi wameuwawa. Watoto wako, Hofni na Finehasi, wamekufa, na sanduku la Mungu limechukuliwa.”.
Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Israeli amekimbia mbele ya Wafilisti, nalo jeshi limepata hasara kubwa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.”
18 Alipotamka sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake karibu na mlango. akavunjika shingo lake, na kufariki, kwa sababu alikuwa mzee tena mzito. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka arobaini.
Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kutoka kwenye kiti chake kwa nyuma kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa amewaongoza Israeli kwa miaka arobaini.
19 Basi mkwewe, mke wa Finihasi, alikuwa mjamzito akikaribia kujifungua. aliposikia habari kwamba sanduku la Mungu limetekwa nyara na kwamba baba mkwe na mme wake wamefariki, alichuchumaa chini akajifungua, lakini utungu wake ulimzidi na ulimtaabisha sana.
Mkwewe, mke wa Finehasi, alikuwa mjamzito na karibu wakati wa kujifungua. Aliposikia habari kwamba Sanduku la Mungu limetekwa na ya kuwa baba mkwe wake na mumewe wamekufa, akapata utungu naye akajifungua lakini akazidiwa na utungu.
20 Alipokaribia kufariki, wanawake waliokuwa wakimhudumia walisema, “Usiogope, maana umejifungua mtoto wa kiume.” Lakini hakuwajibu lolote au kuzingatia alichoambiwa.
Alipokuwa akifa, wanawake waliokuwa wanamhudumia wakamwambia, “Usikate tamaa, umemzaa mwana.” Lakini hakujibu wala kuweka maanani.
21 Akamwita mtoto Ikabodi, akisema, “Utukufu umetoweka Israeli!” Kwa sababu sanduku la Mungu limetekwa nyara, na kwa sababu ya kifo cha baba mkwe na mme wake.
Alimwita yule mtoto Ikabodi, akisema, “Utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa sababu ya kutekwa kwa Sanduku la Mungu na vifo vya baba mkwe na mumewe.
22 Na alisema, “Utukufu umetoweka kutoka Israeli, kwa sababu sanduku la Mungu limetekwa nyala.”
Akasema, “Utukufu umeondoka katika Israeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu limetekwa.”