< 1 Samweli 30 >

1 Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Ziklagi siku ya tatu, Waamaleki walifanya mashambulizi katika Negevu na Ziklagi. Waliupiga Ziklagi, wakauchoma moto mji,
Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto,
2 na kuwachukua mateka wanawake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake, mkubwa kwa mdogo. Wao hawakuua hata mmoja, lakini waliwachukua watu na kuondoka nao.
nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakuua yeyote, bali waliwachukua wakaenda zao.
3 Daudi na watu wake walipofika kwenye mji, ulikuwa umechomwa moto - na wake zao, watoto wao wakiume na wakike walichukuliwa mateka.
Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao na binti zao wamechukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu aliokuwa nao wakapaza sauti zao na kulia hadi walipokuwa hawana nguvu zaidi za kulia.
Hivyo Daudi na watu wake wakapiga yowe mpaka wakaishiwa na nguvu za kulia.
5 Wake wawili wa Daudi walichukuliwa mateka, yaani Ahinoamu Myezreeli, na Abigaili aliyekuwa mke wa Nabali Mkarmeli.
Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.
6 Daudi aliguswa sana, maana watu walikuwa wanaongea kuhusu kumpiga mawe, kwa sababu roho za watu wote walihuzunika, kila mtu kwa ajili ya mtoto wake wakiume na wakike, lakini Daudi alijiimarisha katika BWANA, Mungu wake.
Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana juu ya kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe na binti zake. Lakini Daudi akajitia nguvu katika Bwana, Mungu wake.
7 Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, “Tafadhali, niletee hapa ile naivera.”Abiathari akaileta hiyo naivera kwa Daudi.
Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kisibau.” Abiathari akamletea,
8 Daudi akamwomba BWANA kwa ajili ya mwongozo, akisema, “Je, kama nikiliandama jeshi hili, nitalipata?” BWANA akamjibu, “Wafuate, maana kweli utawapata, na kwa hakika utarudisha kila kitu.”
naye Daudi akamuuliza Bwana, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?” Bwana akajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”
9 Kwa hiyo Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye; nao wakafika katika kijito cha Bethori, mahali walipokaa wale walioachwa nyuma.
Daudi pamoja na watu wake 600 wakafika kwenye Bonde la Besori, mahali ambapo wengine waliachwa nyuma,
10 Lakini Daudi aliendelea kuwafuata, yeye na watu mia nne; maana wale mia mbili walibaki nyuma, wakiwa wamechoka kiasi cha kutoweza kuvuka kijito cha Besori.
kwa kuwa watu 200 walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu 400 wakaendelea kufuatia.
11 Nao walimkuta Mmisri shambani na wakamleta kwa Daudi; wakampatia mkate, na akala; wakampa maji ya kunywa;
Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula;
12 kisha walimpa kipande cha keki ya tini na vishada viwili vya zabibu. Alipomaliza kula, akapata nguvu tena, kwa kuwa alikuwa hajala mkate wala kunywa maji, siku tatu mchana na usiku.
kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana.
13 Ndipo Daudi akamuuliza, “Wewe ni mtu wa nani? Je, unatoka wapi?” Naye akajibu, “Mimi ni kijana wa Misri, mtumishi wa Mwamaleki mmoja; bwana wangu aliniacha, kwa sababu siku tatu zilizopita nilikuwa mgonjwa.
Daudi akamuuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?” Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita.
14 Tulifanya mashambulizi dhidi ya Negevu ya Wakerethi, na iliyochini ya Yuda, na ile Negevu ya Kalebu, na kuichoma moto Ziklagi.”
Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”
15 Daudi akamwambia, “Je, utanipeleka hadi kwa jeshi lililofanya mashabulizi?” Huyo Mmisri akasema, “Uniapie kwa Mungu kwamba hautaniua au kunisaliti na kuniweka katika mikono ya bwana wangu, nami nitakupeleka liliko hilo jeshi.”
Daudi akamuuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?” Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”
16 Yule Mmisri alipompeleka huko Daudi, hao wateka nyara walikuwa wametawanyika kila sehemu, wakila na kunywa, na wakicheza, kwa sababu ya nyara zote walizokuwa wamezitwaa kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka nchi ya Yuda.
Akamwongoza Daudi mpaka mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda.
17 Daudi akawashambulia tangu jua lilipozama hadi jioni ya siku ya pili. Hakuna mtu aliyeponyoka isipokuwa vijana mia nne, waliopanda ngamia na kukimbia.
Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana wanaume 400 waliopanda ngamia na kutoroka.
18 Daudi akarudisha vyote ambavyo Waamaleki walikuwa wamevichukua; na Daudi akawaokoa wake zake wawili.
Daudi akarudisha kila kitu Waamaleki walikuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili.
19 Hakuna kilichopotea, si kidogo wala kikubwa, si watoto wa kiume wala wa kike, si mali iliyotekwa, wala chochote ambacho wavamizi alikichukuwa kwa ajili yao. Daudi akawa amerejesha kila kitu.
Hakuna chochote kilichopotea: kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine chochote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu.
20 Akachukua makundi yote ya kondoo na ng'ombe, ambayo watu waliyatanguliza mbele ya ng'ombe wengine. Wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”
Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya wanyama wengine wa kufugwa, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”
21 Daudi akafika kwa wale watu mia mbili waliokuwa wamechoka kufuatana naye, wale walioachwa wakae katika kijito cha Besori. Watu hawa wakajitokeza kumlaki na watu waliokuwa naye.
Kisha Daudi akafika kwa wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu.
22 Ndipo watu wote waovu na wasiofaa miongoni mwa waliokwenda na Daudi wakasema, “Kwa sababu watu hawa hawakwenda nasi, hatutawapa chochote kutoka katika nyara tulizorudisha. Isipokuwa kila mtu aweza kuchukuwa mke na watoto wake, wawatoe na kwenda zao.”
Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakwenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”
23 Ndipo Daudi akasema, “Ndugu zangu, msifanye hivyo, kwa vitu ambavyo BWANA ametupatia. Ametuhifadhi na kuwaweka mkononi mwetu wavamizi waliotuinukia.
Daudi akajibu, “La hasha, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Bwana ametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu.
24 Ni nani atawasikiliza kuhusu jambo hili? Kwa maana mgawo ni kwa yeyote aendae vitani, basi pia mgawo ni kwa yeyote aliyelinda mizigo; Nao watapata tena kilicho sawa.”
Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyekwenda vitani. Wote watashiriki sawa.”
25 Ilikuwa hivyo tangu siku hiyo hadi leo, maana Daudi aliamua iwe sheria na amri kwa Israeli.
Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.
26 Daudi alipofika Ziklagi, alituma sehemu ya nyara kwa wazee wa Yuda, kwa rafiki zake, akisema, “Tazama, hii ni zawadi yenu kutokana na nyara za adui wa BWANA.”
Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka nyara za adui za Bwana.”
27 Zawadi zilienda kwa wazee waliokuwa Bethueli, na kwa hao waliokuwa Ramothi iliyoko kusini, na kwa hao waliokuwa Yatiri,
Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri;
28 na kwa hao waliokuwa Aroeri, na kwa hao waliokuwa Sifmothi, na kwa hao waliokuwa Eshtemoa
kwa wale walioko Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa
29 Pia kwa wazee waliokuwa Rakali, na kwa hao waliokuwa katika miji ya Wayerameeli, na kwa hao waliokuwa katika miji ya Wakeni,
na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni;
30 na kwa hao waliokuwa Horma, na kwa hao waliokuwa Borashani, na kwa hao waliokuwa Athaki,
na kwa wale walioko Horma, Bori-Ashani, Athaki,
31 na kwa hao waliokuwa Hebroni, na kwa sehemu zote ambazo Daudi mwenyewe na watu wake walizoea kwenda.
na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.

< 1 Samweli 30 >