< 1 Samweli 29 >
1 Basi Wafilisti walikusanya pamoja majeshi yao yote huko Afeki; Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.
2 Nao wakuu wa Wafilisti wakapitwa na mamia kwa maelfu; Daudi na watu wake wakapita wakiwa wa mwisho pamoja na Akishi.
3 Kisha wakuu wa Wafilisti wakasema, “Hawa Waebrania wanafanya nini hapa?” Akishi akawaambia wakuu wengine wa Wafilisti, “Huyu si Daudi, mtumishi wa Sauli, mfalme wa Israeli, ambaye amekaa nami kwa siku hizi, au kwa miaka hii, nami nimeona hana kosa tangu aje kwangu hadi leo?”
4 Lakini wale wakuu wa Wafilisti walimkasirikia Akishi; wakamwabia, Mfukuze mtu huyo, aende kwake kule ulikompatia; usimruhusu aende nasi vitani, ili asiwe adui yetu katika vita. Kwa jinsi gani mtu huyu angeweza kufanya amani na bwana wake? Siyo kwa gharama ya vichwa vya watu wetu?
5 Je, huyu siye Daudi ambaye walimuimba kwa kupokezana na kucheza, wakisema: 'Sauli ameua maelfu yake, Na Daudi makumi elfu yake?”'
6 Ndipo Akishi alimwita Daudi na kumwambia, “Kama BWANA aishivyo, umekuwa mwema, na kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema kama nionavyo mimi; maana sijaona kosa kwako tangu siku unakuja kwangu hadi siku hii ya leo. Hata hivyo, wakuu hawakupendi.
7 Basi sasa rudi na uende kwa amani, ili usiwakwaze wakuu wa Wafilisti.”
8 Daudi akamwambia Akishi, “Lakini nimefanya nini? Kitu gani umekiona kwa mtumishi wako kwa muda ambao nimekuwa mbele yako hadi leo, kiasi kwamba nisiende kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”
9 Akishi akajibu na kumwambia Daudi, “Najua kwamba hauna lawama mbele zangu kama alivyo malaika wa Mungu; hata hivyo, wale wakuu wa Wafilisti wamesema, Kamwe hatapanda pamoja nasi hadi vitani.'
10 Basi sasa amka asubuhi na mapema na watumishi wa bwana wako waliokuja pamoja nawe; mara tu muamkapo asubuhi na mapema na kupata mwanga, ondokeni.”
11 Hivyo Daudi aliamka mapema, yeye pamoja na watu wake, waondoke asubuhi, warudi kule katika nchi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walipanda kwenda Yezreeli.