< 1 Samweli 28 >

1 Ikawa katika siku hizo Wafilisti walikusanya majeshi yao pamoja kwa ajili ya vita, wapigane na Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Ujue kwa hakika kwamba utakwenda nami ndani ya jeshi, wewe na watu wako.”
Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”
2 Naye Daudi akamwambia Akishi, “Sasa utajua kile ambacho mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamwambia Daudi, “Basi sasa, nitakufanya uwe mlinzi wangu binafsi daima.”
Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.”
3 Samweli alikuwa amefariki; Waisraeli wote walimwomboleza na kumzika huko Rama, katika mji wake mwenyewe. Wakati huo Sauli alikuwa amewafukuza kutoka nchini wote walioongea na wafu au pepo.
Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Israeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.
4 Wafilisti walijikusanya wao wenyewe wakaja na kuweka kambi huko Shunemu; na Sauli akawakusanya Israeli wote pamoja, na wakaweka kambi yao huko Gilboa.
Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa.
5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, aliogopa na moyo wake ukatetemeka sana.
Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu.
6 Sauli alipomuomba BWANA kwa ajili ya msaada, BWANA hakumjibu - si kwa ndoto wala kwa Urimu, wala kwa manabii.
Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Bwana, lakini Bwana hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa njia ya manabii.
7 Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, “Mnitafutie mwanamke ambaye anaweza kuongea na wafu, ili ni mwendee na kutafuta msaada wake.” Watumishi wake wakamwambia, “Tazama, yupo mwanamke huko Endori awezaye kuongea na wafu.”
Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.” Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.”
8 Basi Sauli akajigeuza, akavaa nguo nyingine tofauti, akaondoka yeye pamoja na watu wawili; wakamwendea yule mwanamke wakati wa usiku. Akasema, “Nitabirie, nakuomba, kwa kuongea na wafu, na uniinulie yule nitakayekutajia.”
Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”
9 Yule mwanamke akamwambia, “Tazama, unajua alichofanya Sauli, jinsi alivyowafukuza kutoka katika nchi wanaoongea na wafu au mizimu. Basi kwa nini mnatega mtego kwa ajili ya uhai wangu, ili kuniua?”
Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”
10 Sauli akamwapia kwa BWANA na kusema, “Kama BWANA aishivyo, hakuna adhabu utakayopata kutokana na jambo hili.”
Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Bwana, akasema, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”
11 Kisha yule mwanamke akasema, “Je, nikuinulie nani?” Sauli akasema, “Niinulie Samweli.”
Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?” Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.”
12 Yule mwanamke alipomwona Samweli, akalia kwa sauti kuu na kusema na Sauli, akisema, “Kwa nini umenidanganya? Maana wewe ni Sauli.”
Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”
13 Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona kitu gani?” Yule mwanamke akamwambia Sauli, “Naona mungu akitoka katika nchi.” Akamuuliza mwanamke,
Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?” Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.”
14 “Je, anafanana na nani?” Mwanamke akajibu, “Mtu mzee anazuka; naye amevaa kanzu.” Sauli akafahamu kuwa huyo ni Samweli, naye Sauli akainamisha uso wake hadi chini akionesha heshima.
Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?” Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu kifudifudi, uso wake hadi ardhini.
15 Samweli akamwambia Sauli, “Kwa nini umenisumbua na kuniinua juu?” Sauli akajibu, “Nimetaabika sana, maana Wafilisti wamepanga vita dhidi yangu, na Mungu ameniacha na hanipi majibu tena, si kwa manabii, wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita, ili unijulishe kile nitakachofanya.”
Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?” Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena wala kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.”
16 Samweli akasema, “Kwa kuwa BWANA amekuacha, basi unaniuliza nini, naye amekuwa adui yako?
Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadamu Bwana amekuacha na kuwa adui yako?
17 BWANA amekutendea kile alichosema kuwa angekifanya. BWANA amerarua ufalme kutoka mkononi mwako na amempa ufalme mtu mwingine - amempa Daudi.
Bwana ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Bwana ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani Daudi.
18 Kwa sababu hukuitii sauti ya BWANA na hukutekeleza hasira yake kali juu ya Amaleki, kwa hiyo leo naye amefanya hili kwako.
Kwa sababu wewe hukumtii Bwana, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Bwana amekutendea mambo haya leo.
19 Zaidi ya hayo, BWANA atamweka Israeli pamoja na wewe katika mkono wa Wafilisti. Kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. BWANA pia ataliweka jeshi la Israeli katika mkono wa Wafilisti.”
Zaidi ya hayo, Bwana atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Bwana pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”
20 Ndipo ghafla Sauli alianguka chini kifudifudi na aliogopa kwa sababu ya yale maneno ya Samweli. Aliishiwa nguvu mwilini mwake, kwa kuwa siku hiyo alikuwa hajala chakula, hata kwa usiku huo wote.
Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.
21 Ndipo yule mwanamke akaja kwa Sauli na akaona kwamba Sauli amepata shida, naye akamwambia, “Tazama, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako; Nimeyaweka maisha yangu mkononi mwangu na nimeyasikiliza maneno uliyoniambia.
Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye.
22 Hivyo basi, nakusihi, sikiliza pia sauti ya mjakazi wako, na uniruhusu nilete chakula kidogo mbele yako. Ule ili upate nguvu za kwenda kule uendako.”
Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”
23 Lakini Sauli alikataa na kusema, “Sitakula.” Lakini watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha hatimaye alisikiliza sauti zao. Hivyo aliinuka kutoka chini na kukaa kitandani.
Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.” Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.
24 Yule mwanamke alikuwa na ndama mnono hapo nyumbani; akafanya haraka na kumchinja; akachua unga, akaukanda, na akatengeneza mikate isiyotiwa chachu kwa unga huo.
Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu.
25 Akaileta mbele ya Sauli na watumishi wake, nao wakala. Baaadaye waliinuka na kuondoka usiku huo.
Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.

< 1 Samweli 28 >