< 1 Samweli 28 >
1 Ikawa katika siku hizo Wafilisti walikusanya majeshi yao pamoja kwa ajili ya vita, wapigane na Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Ujue kwa hakika kwamba utakwenda nami ndani ya jeshi, wewe na watu wako.”
2 Naye Daudi akamwambia Akishi, “Sasa utajua kile ambacho mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamwambia Daudi, “Basi sasa, nitakufanya uwe mlinzi wangu binafsi daima.”
3 Samweli alikuwa amefariki; Waisraeli wote walimwomboleza na kumzika huko Rama, katika mji wake mwenyewe. Wakati huo Sauli alikuwa amewafukuza kutoka nchini wote walioongea na wafu au pepo.
4 Wafilisti walijikusanya wao wenyewe wakaja na kuweka kambi huko Shunemu; na Sauli akawakusanya Israeli wote pamoja, na wakaweka kambi yao huko Gilboa.
5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, aliogopa na moyo wake ukatetemeka sana.
6 Sauli alipomuomba BWANA kwa ajili ya msaada, BWANA hakumjibu - si kwa ndoto wala kwa Urimu, wala kwa manabii.
7 Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, “Mnitafutie mwanamke ambaye anaweza kuongea na wafu, ili ni mwendee na kutafuta msaada wake.” Watumishi wake wakamwambia, “Tazama, yupo mwanamke huko Endori awezaye kuongea na wafu.”
8 Basi Sauli akajigeuza, akavaa nguo nyingine tofauti, akaondoka yeye pamoja na watu wawili; wakamwendea yule mwanamke wakati wa usiku. Akasema, “Nitabirie, nakuomba, kwa kuongea na wafu, na uniinulie yule nitakayekutajia.”
9 Yule mwanamke akamwambia, “Tazama, unajua alichofanya Sauli, jinsi alivyowafukuza kutoka katika nchi wanaoongea na wafu au mizimu. Basi kwa nini mnatega mtego kwa ajili ya uhai wangu, ili kuniua?”
10 Sauli akamwapia kwa BWANA na kusema, “Kama BWANA aishivyo, hakuna adhabu utakayopata kutokana na jambo hili.”
11 Kisha yule mwanamke akasema, “Je, nikuinulie nani?” Sauli akasema, “Niinulie Samweli.”
12 Yule mwanamke alipomwona Samweli, akalia kwa sauti kuu na kusema na Sauli, akisema, “Kwa nini umenidanganya? Maana wewe ni Sauli.”
13 Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona kitu gani?” Yule mwanamke akamwambia Sauli, “Naona mungu akitoka katika nchi.” Akamuuliza mwanamke,
14 “Je, anafanana na nani?” Mwanamke akajibu, “Mtu mzee anazuka; naye amevaa kanzu.” Sauli akafahamu kuwa huyo ni Samweli, naye Sauli akainamisha uso wake hadi chini akionesha heshima.
15 Samweli akamwambia Sauli, “Kwa nini umenisumbua na kuniinua juu?” Sauli akajibu, “Nimetaabika sana, maana Wafilisti wamepanga vita dhidi yangu, na Mungu ameniacha na hanipi majibu tena, si kwa manabii, wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita, ili unijulishe kile nitakachofanya.”
16 Samweli akasema, “Kwa kuwa BWANA amekuacha, basi unaniuliza nini, naye amekuwa adui yako?
17 BWANA amekutendea kile alichosema kuwa angekifanya. BWANA amerarua ufalme kutoka mkononi mwako na amempa ufalme mtu mwingine - amempa Daudi.
18 Kwa sababu hukuitii sauti ya BWANA na hukutekeleza hasira yake kali juu ya Amaleki, kwa hiyo leo naye amefanya hili kwako.
19 Zaidi ya hayo, BWANA atamweka Israeli pamoja na wewe katika mkono wa Wafilisti. Kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. BWANA pia ataliweka jeshi la Israeli katika mkono wa Wafilisti.”
20 Ndipo ghafla Sauli alianguka chini kifudifudi na aliogopa kwa sababu ya yale maneno ya Samweli. Aliishiwa nguvu mwilini mwake, kwa kuwa siku hiyo alikuwa hajala chakula, hata kwa usiku huo wote.
21 Ndipo yule mwanamke akaja kwa Sauli na akaona kwamba Sauli amepata shida, naye akamwambia, “Tazama, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako; Nimeyaweka maisha yangu mkononi mwangu na nimeyasikiliza maneno uliyoniambia.
22 Hivyo basi, nakusihi, sikiliza pia sauti ya mjakazi wako, na uniruhusu nilete chakula kidogo mbele yako. Ule ili upate nguvu za kwenda kule uendako.”
23 Lakini Sauli alikataa na kusema, “Sitakula.” Lakini watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha hatimaye alisikiliza sauti zao. Hivyo aliinuka kutoka chini na kukaa kitandani.
24 Yule mwanamke alikuwa na ndama mnono hapo nyumbani; akafanya haraka na kumchinja; akachua unga, akaukanda, na akatengeneza mikate isiyotiwa chachu kwa unga huo.
25 Akaileta mbele ya Sauli na watumishi wake, nao wakala. Baaadaye waliinuka na kuondoka usiku huo.