< 1 Samweli 27 >

1 Daudi alisema moyoni mwake, “Basi, siku moja nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jambo zuri kwangu kuliko kutoroka hadi nchi ya Wafilisti; Sauli atakata tamaa asinitafute tena ndani ya mipaka yote ya Israeli; kwa njia hii nitaponyoka kutoka mkono wake.”
Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka popote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.”
2 Daudi akaondoka na kuvuka, akiwa pamoja na watu mia sita hadi kwa Akishi mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.
Hivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi.
3 Daudi akaishi na Akishi huko Gathi pamoja na watu wake, na kila mtu na familia yake, na Daudi akiwa na wake zake wawili, Ahinoamu Myezreeli, na Abigaili Mkarmeli aliyekuwa mke wa Nabali.
Daudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali.
4 Sauli akaambiwa kuwa Daudi amekimbilia Gathi, hivyo hakumtafuta tena.
Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena.
5 Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, wanipatie mahali katika mojawapo ya miji ya nchi, ili nikae huko: kwa nini mtumishi wako akae pamoja na wewe katika mji wa kifalme?”
Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko. Kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?”
6 Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi Ziklagi; ndiyo sababu mji wa Ziklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hadi leo.
Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo.
7 Idadi ya siku ambazo Daudi aliishi katika nchi ya Wafilisti ulikuwa mwaka mmoja na miezi minne.
Daudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne.
8 Daudi na watu wake walizipiga sehemu mbalimbali, wakiteka nyara Wageshuri, Wagirizi, na Waamaleki; kwa maana mataifa hayo ndio walikuwa wakaaji wa nchi, kwa uelekeo wa kwenda Shuri hadi kufika nchi ya Misri. Walikuwa wamekaa katika nchi hiyo toka nyakati za zamani.
Basi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia iteremkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.)
9 Daudi aliipiga nchi na hakumwacha mwanaume wala mwanamke akiwa hai; akatwaa kondoo, ng'ombe, punda, ngamia, na nguo; kisha alirudi na kufika tena kwa Akishi.
Kila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ngʼombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi.
10 Ndipo Akishi humuuliza, “Je, leo umefanya mashambulizi dhidi ya nani?” Daudi humjibu, “Nimefanya dhidi ya kusini mwa Yuda,” au dhidi ya kusini mwa Wayerameeli,” au “dhidi ya kusini mwa Wakeni.”
Akishi alipomuuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda,” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli,” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.”
11 Daudi asingemwacha mwanaume wala mwanamke akiwa hai awalete hadi Gathi, akisema, “ili wasije kututeta, 'Daudi amefanya hivi na vile.”' Hivi ndivyo alivyofanya kwa kipindi chote alichokaa katika nchi ya Wafilisti.
Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana Daudi aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’” Hii ndiyo ilikuwa desturi yake wakati wote aliishi katika nchi ya Wafilisti.
12 Akishi alimwamini Daudi, akisema, “Amesababisha watu wake Israeli wamchukie kabisa; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu milele.”
Akishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.”

< 1 Samweli 27 >