< 1 Samweli 24 >

1 Sauli aliporudi kuwafukuza Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika jangwa la Engedi.”
Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.”
2 Ndipo Sauli akachukua watu elfu tatu waliochaguliwa kutoka Iraeli yote, wakaenda kumtafuta Daudi na watu wake katika miamba ya Mbuzi Mwitu.
Basi Sauli akachukua watu hodari 3,000 kutoka Israeli yote kwenda kumsaka Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu.
3 Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, mahali palipokuwa na pango. Sauli akaingia ndani yake kujisaidia. Wakati huo Daudi na watu wake walikuwa wamekaa mbali zaidi ndani ya pango lilelile.
Akaja mpaka kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi.
4 Watu wake Daudi wakamwambia, “Hii ndiyo siku ambayo BWANA aliisema akikuambia, 'Nitamweka adui wako mkononi mwako, ili umtendee kama unavyotaka.”' Kisha Daudi akainuka na kumnyemelea kwa mbele kimya kimya na kulikata pindo la kanzu ya Sauli.
Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Bwana akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli.
5 Baadaye moyo wa Daudi ukamchoma kwa sababu alilikata pindo la kanzu ya Sauli.
Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli.
6 Akawaambia watu wake, “BWANA anisamehe, sikupaswa kumtendea jambo hili bwana wangu, Mtiwa mafuta wa BWANA, kwa kunyoosha mkono wangu juu yake, maana yeye ni masihi wa BWANA.”
Akawaambia watu wake, “Bwana na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Bwana, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Bwana.”
7 Hivyo Daudi akawakemea watu wake kwa maneno haya, na kuwazuia wasimpige Sauli. Sauli akasimama, akatoka pangoni, na kwenda zake.
Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake.
8 Baadaye tena, Daudi akasimama juu, akatoka pangoni, na kumwita Sauli: “Bwana wangu mfalme.” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akasujudu hadi chini na kuonyesha heshima.
Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kusujudu uso wake mpaka nchi.
9 Daudi akamwambia Sauli, “Kwa nini unawasikiliza watu ambao wanasema, “Angalia, Daudi anatafuta kukudhuru?'
Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’?
10 Leo macho yako yameona jinsi BWANA alivyokuweka mkononi mwangu tulipokuwa ndani ya pango. Wengine waliniambia nikuuwe, lakini nilikuacha hai. Nikasema, 'Sitanyoosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa kuwa ni masihi wa BWANA.'
Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa Bwana.’
11 Tazama, baba yangu, angalia pindo la kanzu yako mkononi mwangu. Kwa maana kama nilikata pindo la kanzu yako na sikukuua, basi ujuwe na uone kwamba sina uovu au kosa katika mkono wangu, na sijafanya dhambi juu yako, ingawa unawinda kuutoa uhai wangu.
Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala ya kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuuondoa uhai wangu.
12 BWANA aamue kati yangu na wewe, na BWANA anilipizie kisasi juu yako, lakini mkono wangu kamwe hautakuwa juu yako.
Bwana na ahukumu kati yangu na wewe. Naye Bwana alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa.
13 Kama mithali ya wazee isemavyo, 'Katika waovu hutoka uovu.' Lakini mkono wangu hautakuwa juu yako.
Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe.
14 Mfalme wa Israeli ametoka kumuandama nani? Unamsaka nani? Unasaka mzoga wa mbwa! Unasaka kiroboto!
“Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto?
15 BWANA na awe mwamuzi na atoe hukumu kati yangu na wewe, na akaione, na akatetee sababu yangu na aniruhusu kuepuka mkono wako.”
Bwana na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.”
16 Daudi alipomaliza kuongea maneno haya kwa Sauli, Sauli akasema, “Hii ni sauti yako, mwanangu Daudi?” Sauli alinyanyua sauti yake akalia.
Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu, akisema,
17 Akamwambia Daudi, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi. Kwa sababu umenilipa mazuri, wakati mimi nimekulipa maovu.
“Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya.
18 Leo umetangaza jinsi ulivyonitendea mazuri, kwa sababu hukuniua wakati BWANA aliponiweka katika rehema yako.
Sasa umeniambia juu ya mema uliyonitendea. Bwana alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua.
19 Kwa kuwa mtu akimpata adui yake, atamwacha aende zake salama? Na BWANA akuzawadie mema kwa kile ulichonifanyia leo.
Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? Bwana na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo.
20 Basi, najua kwa hakika kwamba utakuwa mfalme na kwamba ufalme wa Israeli utaimarika katika mkono wako.
Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na ya kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako.
21 Niapie kwa BWANA kwamba baada yangu hautawakatilia mbali uzao wangu, na kwamba hautaliharibu jina langu katika nyumba ya baba yangu.”
Sasa niapie kwa Bwana kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.”
22 Hivyo Daudi akamwapia Sauli kiapo. Kisha Sauli akaenda nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.
Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.

< 1 Samweli 24 >