< 1 Samweli 23 >
1 Wakamwambia Daudi, “Tazama, Wafilisti wanaupiga Keila na wanapora nafaka inayopurwa.”
Daudi alipoambiwa kuwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,”
2 Hivyo Daudi akamwomba BWANA kwa ajili ya msaada, na akamuuliza,” Je, niondoke niwapige hawa Wafilisti? BWANA akamwambia Daudi, “Nenda ukawapige Wafilisti na kuokoa Keila.”
akauliza kwa Bwana, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?” Bwana akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.”
3 Daudi akaambiwa na watu wake, “Angalia, hapa Yuda tunaogopa. Je, si zaidi sana kama tutaenda Keila kupambana na majeshi ya Wafilisti?”
Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Si zaidi sana, kama tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!”
4 Ndipo Daudi akamwomba BWANA kwa ajili ya msaada, bado tena, BWANA akamjibu, “Amka, uteremke hadi Keila. Maana nitakupatia ushindi dhidi ya Wafilisti.”
Daudi akauliza kwa Bwana tena, naye Bwana akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.”
5 Daudi na watu wake wakaenda Keila na kupigana na Wafilisti. Wakahamisha ng'ombe wao na kuwapiga kwa mauaji makubwa mno. Hivyo Daudi akawaokoa wenyeji wa Keila.
Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila.
6 Abiathari mwana wa Ahimeleki alipokuwa amekimbilia kwa Daudi huko Keila, alibeba naivera mkononi mwake.
(Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kisibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.)
7 Sauli aliambiwa kwamba Daudi amekwenda Keila. Sauli akasema, “Mungu amemweka mkononi mwangu. Bila shaka amefungiwa ndani kwa sababu ameingia katika mji ulio na malango na makomeo.”
Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa amekwenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.”
8 Sauli akayaita majeshi yake yote kwa ajili ya vita, waende hadi Keila, wamteke Daudi na watu wake.
Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi.
9 Daudi alijua kwamba Sauli alikuwa anapanga njama za kumdhuru yeye. Ndipo akamwambia kuhani Abiathari kuhani, “Ulete hapa naivera.”
Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kisibau.”
10 Kisha Daudi akasema, “BWANA, Mungu wa Israeli, mtumishi wako hakika amesikia kwamba Sauli anatafuta namna ya kuja Keila, ili auteketeze mji kwa ajili yangu.
Daudi akasema, “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu.
11 Je, watu wa Keila watanisalimisha mkononi mwake? Je, Sauli atashuka hadi huko, kama mtumishi wako alivyosikia? BWANA, Mungu wa Israeli, nakusihi, tafadhali mwambie mtumishi wako. “BWANA akasema, “Atakuja huko.”
Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.” Naye Bwana akasema, “Ndiyo, atashuka.”
12 Kisha Daudi akauliza, “Je, watu wa Keila watanisalimisha mimi na watu wangu katika mkono wa Sauli?” BWANA akasema, “Watu hao watawasalimisha kwao.”
Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?” Naye Bwana akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.”
13 Kisha Daudi na watu wake, waliokuwa kama mia sita, walitoka na kwenda mbali na Keila, na wakazunguka kila sehemu. Kisha Sauli akaambiwa kwamba Daudi ametoroka kutoka Keila, hivyo akasitisha kumfuatia.
Basi Daudi na watu wake, wapatao 600, wakaondoka Keila wakawa wanakwenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakwenda huko.
14 Daudi alikaa ngomeni katika jangwa, kwenye nchi ya milima katika jangwa la Zifu. Kila siku Sauli alimtafuta, lakini Mungu hakumweka mkononi mwake.
Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwake.
15 Daudi aliona kwamba Sauli amejitokeza kuangamiza maisha yake; basi Daudi alikuwa katika jjangwa la Zifu huko Horeshi.
Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue.
16 Kisha Yonathani, mwana wa Sauli, akaamuka akaenda kwa Daudi huko Horshi, naye akamtia moyo amtumainie Mungu.
Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu.
17 Akamwambia, “Usiogope. Kwa maana mkono wa baba yangu Sauli hautakupata. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, na mimi nitakuwa msaidizi wako. Baba yangu Sauli pia anajua hivyo.”
Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.”
18 Basi wote wawili wakafanya agano mbele za BWANA. Kisha Daudi alibaki Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani.
Wote wawili wakaweka agano mbele za Bwana. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.
19 Nndipo Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea wakisema, “Je, Daudi hakujificha kati yetu kwenye ngome huko Horeshi, juu ya mlima wa Hakila, ulioko kusini mwa Yeshimoni?
Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni?
20 Basi uje, mfalme! Kulingana na matakwa yako, uje! Kazi yetu itakuwa kumtia katika mkono wa mfalme.”
Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.”
21 Sauli akasema, “Mbarikiwe na BWANA. Kwa sababu mmenihurumia.
Sauli akajibu, “Bwana awabariki kwa kunifikiria.
22 Nendeni, mhakikishe sawasawa. Tafuteni na kujua maficho yake yako wapi na ni nani amemwona huko. Nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana.
Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali ambapo Daudi huenda mara kwa mara na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mwerevu sana.
23 Kwa hiyo chunguzeni, mjue sehemu zote anakojificha. Baadaye rudini kwangu mkiwa na taarifa kamili, na kisha nitaongozana nanyi. Ikiwa yupo katika nchi, nitamtafuta kutoka miongoni mwa elfu zote za Yuda.”
Jueni kila mahali anapojificha mrudi na kunipa taarifa kamili. Kisha nitakwenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.”
24 Ndipo wakaamka na kwenda hadi Zifu mbele ya Sauli. Wakati huo Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, huko Araba upande wa kusini mwa Yeshimoni.
Basi wakaondoka na kwenda mpaka Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni.
25 Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta Daudi. Na Daudi akaambiwa habari hiyo, hivyo akateremka hadi kwenye mlima wa miamba na akakaa katika jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hivyo, akamfukuza Daudi katika Jangwa la Maoni.
Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka mpaka mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi.
26 Sauli akaenda akawa upande mmoja wa mlima, na Daudi na watu wake walikuwa wakienda upande mwingine wa mlima. Daudi kwa haraka akatoweka akae mbali na Sauli. Kwa sababu Sauli na watu wake walikuwa wakimzunguka Daudi na watu wake wawakamate,
Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Wakati Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake,
27 mjumbe mmoja akaja kwa Sauli na kusema, “Njoo, harakisha maana Wafilisti wamepanga uvamizi juu ya nchi.”
mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.”
28 Kwa hiyo Sauli akarudi asimfuatie Daudi na akaenda kupambana na Wafilisti. Kwa hiyo sehemu ile iliitwa Mwamba wa Maficho.
Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi.
29 Daudi akapanda kutoka huko na kukaa katika ngome ya Engedi.
Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.