< 1 Samweli 23 >
1 Wakamwambia Daudi, “Tazama, Wafilisti wanaupiga Keila na wanapora nafaka inayopurwa.”
2 Hivyo Daudi akamwomba BWANA kwa ajili ya msaada, na akamuuliza,” Je, niondoke niwapige hawa Wafilisti? BWANA akamwambia Daudi, “Nenda ukawapige Wafilisti na kuokoa Keila.”
3 Daudi akaambiwa na watu wake, “Angalia, hapa Yuda tunaogopa. Je, si zaidi sana kama tutaenda Keila kupambana na majeshi ya Wafilisti?”
4 Ndipo Daudi akamwomba BWANA kwa ajili ya msaada, bado tena, BWANA akamjibu, “Amka, uteremke hadi Keila. Maana nitakupatia ushindi dhidi ya Wafilisti.”
5 Daudi na watu wake wakaenda Keila na kupigana na Wafilisti. Wakahamisha ng'ombe wao na kuwapiga kwa mauaji makubwa mno. Hivyo Daudi akawaokoa wenyeji wa Keila.
6 Abiathari mwana wa Ahimeleki alipokuwa amekimbilia kwa Daudi huko Keila, alibeba naivera mkononi mwake.
7 Sauli aliambiwa kwamba Daudi amekwenda Keila. Sauli akasema, “Mungu amemweka mkononi mwangu. Bila shaka amefungiwa ndani kwa sababu ameingia katika mji ulio na malango na makomeo.”
8 Sauli akayaita majeshi yake yote kwa ajili ya vita, waende hadi Keila, wamteke Daudi na watu wake.
9 Daudi alijua kwamba Sauli alikuwa anapanga njama za kumdhuru yeye. Ndipo akamwambia kuhani Abiathari kuhani, “Ulete hapa naivera.”
10 Kisha Daudi akasema, “BWANA, Mungu wa Israeli, mtumishi wako hakika amesikia kwamba Sauli anatafuta namna ya kuja Keila, ili auteketeze mji kwa ajili yangu.
11 Je, watu wa Keila watanisalimisha mkononi mwake? Je, Sauli atashuka hadi huko, kama mtumishi wako alivyosikia? BWANA, Mungu wa Israeli, nakusihi, tafadhali mwambie mtumishi wako. “BWANA akasema, “Atakuja huko.”
12 Kisha Daudi akauliza, “Je, watu wa Keila watanisalimisha mimi na watu wangu katika mkono wa Sauli?” BWANA akasema, “Watu hao watawasalimisha kwao.”
13 Kisha Daudi na watu wake, waliokuwa kama mia sita, walitoka na kwenda mbali na Keila, na wakazunguka kila sehemu. Kisha Sauli akaambiwa kwamba Daudi ametoroka kutoka Keila, hivyo akasitisha kumfuatia.
14 Daudi alikaa ngomeni katika jangwa, kwenye nchi ya milima katika jangwa la Zifu. Kila siku Sauli alimtafuta, lakini Mungu hakumweka mkononi mwake.
15 Daudi aliona kwamba Sauli amejitokeza kuangamiza maisha yake; basi Daudi alikuwa katika jjangwa la Zifu huko Horeshi.
16 Kisha Yonathani, mwana wa Sauli, akaamuka akaenda kwa Daudi huko Horshi, naye akamtia moyo amtumainie Mungu.
17 Akamwambia, “Usiogope. Kwa maana mkono wa baba yangu Sauli hautakupata. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, na mimi nitakuwa msaidizi wako. Baba yangu Sauli pia anajua hivyo.”
18 Basi wote wawili wakafanya agano mbele za BWANA. Kisha Daudi alibaki Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani.
19 Nndipo Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea wakisema, “Je, Daudi hakujificha kati yetu kwenye ngome huko Horeshi, juu ya mlima wa Hakila, ulioko kusini mwa Yeshimoni?
20 Basi uje, mfalme! Kulingana na matakwa yako, uje! Kazi yetu itakuwa kumtia katika mkono wa mfalme.”
21 Sauli akasema, “Mbarikiwe na BWANA. Kwa sababu mmenihurumia.
22 Nendeni, mhakikishe sawasawa. Tafuteni na kujua maficho yake yako wapi na ni nani amemwona huko. Nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana.
23 Kwa hiyo chunguzeni, mjue sehemu zote anakojificha. Baadaye rudini kwangu mkiwa na taarifa kamili, na kisha nitaongozana nanyi. Ikiwa yupo katika nchi, nitamtafuta kutoka miongoni mwa elfu zote za Yuda.”
24 Ndipo wakaamka na kwenda hadi Zifu mbele ya Sauli. Wakati huo Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, huko Araba upande wa kusini mwa Yeshimoni.
25 Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta Daudi. Na Daudi akaambiwa habari hiyo, hivyo akateremka hadi kwenye mlima wa miamba na akakaa katika jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hivyo, akamfukuza Daudi katika Jangwa la Maoni.
26 Sauli akaenda akawa upande mmoja wa mlima, na Daudi na watu wake walikuwa wakienda upande mwingine wa mlima. Daudi kwa haraka akatoweka akae mbali na Sauli. Kwa sababu Sauli na watu wake walikuwa wakimzunguka Daudi na watu wake wawakamate,
27 mjumbe mmoja akaja kwa Sauli na kusema, “Njoo, harakisha maana Wafilisti wamepanga uvamizi juu ya nchi.”
28 Kwa hiyo Sauli akarudi asimfuatie Daudi na akaenda kupambana na Wafilisti. Kwa hiyo sehemu ile iliitwa Mwamba wa Maficho.
29 Daudi akapanda kutoka huko na kukaa katika ngome ya Engedi.