< 1 Samweli 2 >
1 Hana aliomba akasema, “moyo wangu wamtukuza BWANA. Pembe yangu imejulikana katika BWANA. Kinywa changu kinatamba dhidi ya maadui zangu, kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
2 Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA, kwa kuwa hakuna mwingine zaidi yako; hakuna mwamba kama Mungu wetu.
3 Msijivune sana hivyo kwa kiburi; vinywa vyenu visitoke majivuno. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa; yeye huyapima matendo kwa mizani.
4 Pinde za mashujaa zimevunjika, bali wale wanaojikwaa hujivika nguvu kama mshipi.
5 Wale walio na shibe ya kutosha wamejikodisha ili wapate chakula; wale waliokuwa na njaa hawana njaa tena. Hata yule aliye kuwa tasa amezaa watoto saba, bali mwanamke mwenye watoto wengi amenyong'onyea.
6 BWANA huua na huuisha. Hushusha kuzimu na huleta tena juu. (Sheol )
7 BWANA humfanya maskini, na yeye ndiye humtajirisha mtu. Yeye hudhili, lakini pia hukweza
8 Yeye humwinua juu maskini toka mavumbini: Huwainua wahitaji toka jalalani na kuwaketisha pamoja na wakuu na kuwarithisha kiti cha enzi cha utukufu. Kwa kuwa nguzo za dunia ni za BWANA na ameukalisha ulimwengu juu yake.
9 Yeye atazilinda nyayo za watu wake waaminifu, bali waovu watanyamazishwa gizani, kwa maana hakuna atayeshinda kwa nguvu zake.
10 Wale wampingao BWANA watavunjwa vipande vipande; atawapiga radi kutokea mbinguni. BWANA atahukumu miisho ya dunia; atampa nguvu mfalme wake na kuinua pembe ya mtiwa mafuta wake.”
11 Nndipo Elikana akenda Rama, nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia BWANA machoni pa Eli, kuhani.
12 Basi, watoto wa Eli walikuwa wakorofi. Wao hawakumheshimu BWANA.
13 Desturi ya makuhani na watu ilikuwa kwamba endapo mtu yeyote ametoa dhabihu, mtumishi wa kuhani angekuja akiwa na uma wa meno matatu mkononi mwake, nyama ilipokuwa inatokoswa.
14 Naye angeutia uma huo sufuriani, au birikani au chomboni au chunguni; nyama yote ambayo ingeinuliwa na uma huo ingetwaliwa na kuhani mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokwenda huko.
15 Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, mtumishi wa kuhani alikuja, na kumwambia aliyekuwa akitoa dhabihu, “Tenga nyama ya kuchoma kwa ajili ya kuhani; kwa sababu hataikubali ile ya kutokosa kutoka kwako, bali tu ile mbichi.”
16 Ikiwa mtu atamwambia, “Wachome mafuta kwanza, na kisha uchukue kiasi utakacho.” Ndipo angesema, “Hapana, utanipatia sasa hivi; la sivyo; Nitaichukua kwa lazima.”
17 Dhambi ya vijana hawa ilikuwa mbaya sana mbele za BWANA, kwa sababu waliidharau dhabihu ya BWANA.
18 Lakini Samweli alimtumikia BWANA akiwa mdogo akivaa nguo ya naivera ya kitani.
19 Kila mwaka mama yake alimtengenezea kanzu dogo na kumletea, wakati wakija na mmewe kutoa dhabihu ya kila mwaka.
20 Eli aliwabariki Elikana na mke wake na kusema, “BWANA akupatie watoto zaidi kwa mwanamke huyu kwa sababu ya ahadi yake aliyoitoa kwa BWANA.” Baadaye walirudi nyumbani kwao.
21 BWANA alimsaidia tena Hana, akawa amebeba mimba nyingine. Akazaa watoto watatu wa kiume na wa kike wawili. Wakati huo huo mtoto Samweli akakua akiwa mbele za BWANA.
22 Basi Eli alikuwa mzee sana, akayasikia yote ambayo watoto wake walikuwa wakiwafanyia Waisraeli wote, na jinsi walivyotembea na mwanamke aliyekuwa akitumika katika lango la hema ya kukutania.
23 Akawaambia, “Kwa nini mnafanya mambo hayo? Kwa maana nasikia matendo yenu maovu kutoka kwa watu hawa wote.”
24 Sivyo hivyo, watoto wangu, maana hii ninayoisikia siyo taarifa njema. Mnawakosesha watu wa BWANA.
25 “Kama mtu mmoja akimkosea mwenzake, Mungu atamhukumu; Lakini mtu akimkosea BWANA, ni nani atakayemtetea mtu huyo?” Lakini hawakuitii sauti ya baba yao, sababu BWANA alinuia kuwaua.
26 Yule mtoto Samweli aliongezeka umri, na kupata kibali kwa BWANA na kwa watu pia.
27 Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli na kumwambia, “BWANA asema, 'Je, sikujifunua mwenyewe kwa nyumba ya baba zako, walipokuwa Misri utumwani nyumbani mwa Farao?
28 Mimi nilimchagua yeye kutoka makabila yote ya Israeli awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu, na kufukiza uvumba, na kuvaa kanzu ya naivera mbele yangu. Niliwapa nyumba ya baba zako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto.
29 Kwanini basi, unaidharau dhabihu yangu na sadaka ambazo ninazitaka mahali ninapoishi? Kwanini unawaheshimu watoto wako kuliko mimi, kwa kujinenepesha ninyi wenyewe kwa uzuri wa kila sadaka ya watu wangu Israeli?'
30 Maana, BWANA, Mungu wa Isareli, asema, niliahidi kwamba nyumba yako, na nyumba ya baba yako, yawapasa kwenda mbele zangu milele,' Lakini sasa BWANA asema. 'Mambo haya yapishe mbali. nami nisifanye hivi, maana nitawaheshimu wanaoniheshimu, bali wanaonidharau mimi hawatakuwa na thamani.
31 Tazama, siku zinakuja nitakapoondoa nguvu zako na nguvu za nyumba za baba yako, ili kwamba pasije kuwepo mtu mzee katika nyumba yako.
32 Nawe utalitazama hangaiko katika makao yangu. Ingawa Israeli watapewa jambo jema, hapatakuwapo tena mtu yeyote mzee katika nyumba yako.
33 Yeyote miongoni mwenu nisiye mwondoa kutoka madhabahuni pangu, Nitasababisha macho yenu yaanguke, na ita nitasababisha huzuni maishani mwenu. Wanaume wote waliozaliwa katika familia yako watakufa.
34 Hii ndiyo itakuwa ishara kwako ambayo itawaijia watoto wako wakiume wawili, juu ya Hofni na Finehasi: Wote wawili watakufa siku moja.
35 Nami nitamwinua juu kuhani wangu mwaminifu atakaye fanya kile kilichomo moyoni mwangu na nafisini mwangu. Nami nitamjengea nyumba madhubuti; naye atakwenda mbele ya mfalme wangu mbarikiwa milele.
36 Kila mmoja aliyebakia nyumbani mwako atakuja na kusujudu mbele ya mtu huyo, akiomba kipande cha fedha na mkate mmoja, naye atasema, “Tafadhali uniajiri katika moja ya nafasi za kuhani ili niweze kula kipande cha mkate'”'