< 1 Samweli 17 >
1 Basi Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa ajili ya vita. Walikusanyika huko Soko, iliyoko Yuda. Nao wakapiga kambi kati ya Soko na Aseka katika Efesdamimu.
2 Sauli na watu wa Israeli alijikusanya na kuweka kambi katika bonde la Ela, na wakapanga vita kukutana na Wafilisti.
3 Wafilisti walisimama juu ya mlima upande mmoja, na Iraeli nao walisimama juu ya mlima upande mwingine wakitenganishwa na bonde kati yao.
4 Mtu mmoja mwenye nguvu akatoka katika kambi ya Wafilisti, mtu huyo aliitwa Goliathi wa Gathi, kimo chake mikono sita na shubiri moja.
5 Alikuwa na chepeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya chuma. Hiyo dirii ilikuwa na uzito wa shekeli elfu hamsini za shaba.
6 Alikuwa na mabampa ya shaba kwenye miguu yake na mkuki wa shaba katikati ya mabega yake.
7 Ule mpini wa mkuki wake ulikuwa mkubwa, wenye kamba iliyo na kitanzi kwa ajili ya kuutupia kama kamba ya sindano ya mfumaji. Kichwa cha mkuki wake kilikuwa na uzito wa shekeli mia sita za chuma. Aliyembebea ngao alitembea mbele yake.
8 Alisimama akayapigia kelele majeshi ya Israeli, “Kwa nini mmekuja na mmejipanga kwa ajili ya vita? Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Chagueni mtu kutoka kwenu ateremke na kuja kwangu.
9 Kama anaweza kupigana nami na kuniua, hapo ndipo tutakuwa watumwa wenu. Lakini kama nitamshinda na kumuua, basi mtakuwa watumwa wetu na kututumikia.”
10 Mfilisti huyo akasema tena, “Leo ninayapa changamoto majeshi ya Israeli. Mnipe mtu ili tuweze kupigana naye.”
11 Sauli na Israeli wote waliposikia alichosema Mfilisti huyo, walikata tamaa na kuogopa sana.
12 Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefraimu wa Bethtelehemu ya Yuda, aliyeitwa Yese. Naye alikuwa na watoto wanane wa kiume. Yese alikuwa mtu mzee katika siku za Sauli, mwenye umri mkubwa kati ya watu.
13 Watoto watatu wakubwa wa Yese walimfuata Sauli vitani. Majina ya watoto wake watatu waliokwenda vitani yalikwa ni Eliabu mzaliwa wa kwanza, aliyemfuata Abinadabu, na watatu aliitwa Shama.
14 Daudi ndiye aliyekuwa mdogo kabisa. Hao wakubwa watatu walimfuata Sauli.
15 Basi Daudi alikwenda na kurudi akipita kati ya majeshi ya Sauli akiwa na kondoo za baba yake huko Bethtelehemu, ili kuwachunga.
16 Kwa muda wa siku arobaini yule Mfilisti mwenye nguvu alikuwa akijitokeza asubuhi na jioni kwa ajili ya vita.
17 Kisha Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Wapelekee kaka zako efa ya bisi na hii mikate kumi, na uzipeleke upesi kule kambini kwa ajili ya kaka zako.
18 Pia peleka hizi jibini kumi kwa jemedari wa kikosi chao cha elfu. Ukawaangalie wako na hali gani kisha uniletee habari kuhusu wanavyoendelea vizuri.
19 Kaka zako wako pamoja na Sauli na watu wote wa Israeli katika bonde la Ela, wanapigana na Wafilisti.”
20 Daudi aliamka asubuhi na mapema na kuliacha kundi chini ya uangalizi wa mchungaji. Akachukua vile vitu na kuondoka, kama Yese alivyomwamuru. Akafika kambini wakati jeshi linaondoka kwenda uwanja wa vita wakipiga kelele za vita.
21 Nao Israeli na Wafilisti walijipanga kivita, jeshi dhidi ya jeshi.
22 Daudi aliviacha vitu vyake kwa mtunza mahitaji, akalikimbilia jeshi, na kuwasalimia kaka zake.
23 Alipoongea nao, yule mtu mwenye nguvu, Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akajitokeza kutoka majeshi ya Wafilisti, naye akasema maneno yaleyale kama hapo mwanzo. Naye Daudi akayasikia.
24 Watu wote wa Israeli walipomwona Goliathi, walimkimbia na waliogopa sana.
25 Watu wa Israeli walisema, “Umemuona mtu huyu aliyejitokeza? Amekuja kuipa changamoto Israeli. Basi mfalme atampa mali nyingi mtu atakayemua, atamuozesha binti yake, na familia ya baba yake haitalipa kodi katika Israeli.”
26 Daudi akawauliza watu waliosimama karibu naye, “Atafanyiwa nini mtu ambaye atamuua Mfilisti huyu na kuiondolea Israeli fedheha? Ni nani Mfilisti huyu asiyetahiriwa ayatukanaye majeshi ya Mungu aliye hai?”
27 Ndipo watu wakarudia kile walichokuwa wamesema na kumwambia, “Ndivyo iitakavyofanyika kwa mtu atakayemuua.”
28 Kaka yake mkubwa Eliabu, alisikia wakati akisema na watu. Hasira ya Eliabu ikawaka moto dhidi ya Daudi, naye akamuuliza, “Kwa nini umekuja hapa? Wale kondoo wachache umewaacha na nani huko nyikani? Nakijua kiburi chako, na utundu wa moyo wako; maana umekuja hapa ili uweze kuona mapigano.”
29 Naye Daudi akamjibu, “Nimefanya nini sasa? Mimi si nuliuliza swali tu?
30 Akamgeukia mtu mwingine na kumwacha huyo, na kusema vivyo hivyo. Nao watu wakajibu vilevile kama mwanzo.
31 Maneno aliyosema Daudi yaliposikika, askari waliyasema tena kwa Sauli, naye akawatuma kwa Daudi.
32 Kisha Daudi akamwambia Sauli, “Pasiwepo moyo wa mtu atakayezimia kwa sababu ya Mfilisti huyo; Mtumishi wako atakwenda kupigana na Mfilisti huyu.”
33 Sauli akamwambia Daudi, “Huwezi kumpinga Mfilisti ama kupigana naye; wewe ni kijana tu, na yeye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.”
34 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake. Mara simba au dubu alikuja akamchukua mwana kondoo kutoka kundini,
35 Nilimfukuza na kumshambulia na kumpokonya kutoka kinywani mwake. Na aliponirukia, nilimshika ndevu zake, nilimpiga, na kumuua.
36 Mtumishi wako amekwisha kmuua simba na dubu. N huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa wanyama hao, kwa kuwa ameyadharau majeshi ya Mungu aliye hai.”
37 Daudi akasema, “BWANA aliyeniokoa kutoka makucha ya simba na makucha ya dubu. Ataniokoa kutoka mkono wa Mfilisti huyu.” Kisha Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, BWANA awe pamoja nawe.”
38 Sauli akamvika Daudi vazi lake la vita. Akamvika chepeo ya shaba kichwani pake, na akamvika koti la chuma.
39 Daudi akaufunga upanga wake juu ya vazi la Sauli. Lakini hakuweza kutembea, kwa sababu hakupata mafunzo kwa mavazi hayo. Ndipo Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda kupigana nikiwa na haya, maana sikupata mafunzo kwa haya.” Kwa hiyo Daudi akayavua.
40 Akachukua fimbo mkononi mwake na akachagua mawe matano laini kutoka katika kijito; akayaweka kwenye mfuko wake wa kichungaji. Kombeo lake lilikuwa mkononi akawa anamsogelea yule Mfilisti.
41 Yule Mfilisti akaja na kumsogelea Daudi, mbeba ngao yake akiwa mbele yake.
42 Mfilisti alipotazama kila upande na kumuona Daudi, akamdharau, maana alikuwa kijana tu, mwekundu, na umbo la kupendeza.
43 Ndipo Mfilisti akamuuliza Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata ukanijia na fimbo? Naye Mfilisti kwa miungu yake akamlaani Daudi.
44 Huyo Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu, na nyama yako nitawatupia ndege wa angani na wanyama wa mwituni.”
45 Daudi akamjibu Mfilisti, “Unaniijia kwa upanga, kwa mkuki na mkuki mdogo. Bali mimi nakuijia kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa Majeshi ya Israeli, uliyemdharau.
46 Leo BWANA atanipa ushindi dhidi yako, na nitakuua na kukiondoa kichwa chako kwenye kiwiliwili. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni walioko duniani mizoga ya jeshi la Wafilisti, ili dunia yote ijue kwamba yupo Mungu katika Israeli,
47 na kusanyiko hili lote lijue kwamba BWANA hatoi ushindi kwa upanga wala kwa mkuki. Kwa kuwa vita ni ya BWANA, na atawaweka katika mkono wetu.”
48 Mfilisti aliponyanyuka na kukaribia akutane na Daudi, ndipo Daudi akakimbia kwa haraka kuelekea jeshi la adui ili akutane naye.
49 Daudi aliweka mkono wake mfukoni, akachukua jiwe kutoka humo, akalitupa kwa kombeo, na likampiga Mfilisti kwenye paji la uso, akaanguka chini kifudifudi.
50 Daudi alimshinda Mfilisti kwa kombeo na kwa jiwe moja. Alimpiga huyo Mfilisti na kumuua. Mkononi mwa Daudi hakukuwa na upanga.
51 Ndipo Daudi akakimbia akasimama juu ya Mfilisti na kutwaa upanga wake, akauchomoa kutoka alani, akamuua, na kukata kichwa chake kwa upanga huo.
52 Ndipo watu wa Israeli na wale wa Yuda wakaamka kwa kelele, na kuwafukuza Wafilisti kuvuka bonde na malango ya Ekroni. Na maiti za Wafilisti walilala katika njia iendayo Shaaraimu, na njia yote kuelekea Gathi na Ekroni.
53 Watu wa Israeli wakarejea kutoka kuwafukuza Wafilisti, na wakateka nyara kambi yao.
54 Daudi akachukua kichwa cha Mfilisti na kukipeleka Yerusalemu, lakini akaliweka vazi la vita katika hema lake.
55 Sauli alipomuona Daudi akienda kukabiliana na yule Mfilisti, akamwambia Abneri, jemedari wa jeshi, “Abneri, kijana huyu ni mtoto wa nani? Abneri akasema, “Kama uishivyo, mfalme, mimi sijui.”
56 Naye mfalme akasema, “Waulize wanaoweza kufahamu, mvulana huyu ni kijana wa nani.”
57 Daudi aliporudi kutoka kumuua yule Mfilisti, Abneri alimchukuwa, na kumleta mbele ya Sauli akiwa na kichwa cha Mfilisti mkononi mwake.
58 Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mtoto wa nani? Na Daudi akamjibu, “Mimi ni mtoto wa mtumishi wako Yese Mbethlehemu.”