< 1 Samweli 15 >
1 Samweli akamwambia Sauli, “BWANA alinituma nikutie mafuta uwe mfalme wa watu wake Israeli. Basi sikiliza maneno ya BWANA.
Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye ambaye Bwana alinituma nikutie mafuta uwe mfalme juu ya watu wake Israeli, basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa Bwana.
2 Hivi ndivyo BWANA wa majeshi asemavyo, 'Nilichunguza jinsi Amaleki alivyomfanyia Israeli kwa kuwapinga njiani, walipopanda kutoka Misri.
Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri.
3 Sasa nenda umshambulie Amaleki na ukaangamize kabisa vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache, ua wote mwanamme na mwanamke, mtoto na mtoto mchanga, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.”'
Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, ngʼombe na kondoo, ngamia na punda.’”
4 Sauli akwaita watu na kuwahesabu katika mji wa Talemu: watu mia mbili elfu waendao kwa miguu, na watu elfu kumi kutoka Yuda.
Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu 200,000 pamoja na watu 10,000 kutoka Yuda.
5 Kisha Sauli akaja hadi mji wa Amaleki akangoja huko bondeni.
Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni.
6 Ndipo Sauli akawaambia Wakeni, “Nendeni, muondoke, mkajitenge na Waamaleki, nisije kuwaangamiza pamoja nao. Kwa maana ulionesha wema kwa watu wote wa Israeli, walipotoka Misri.” Kwa hiyo Wakeni wakajitenga na Waamaleki.
Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki.
7 Kisha sauli akawashambulia Waamaleki, kutoka Havila hadi kufika Shuri, ulio mashariki mwa Misri.
Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila mpaka Shuri, hadi mashariki ya Misri.
8 Basi akamchukua Agagi mfalme wa Waamaleki akiwa hai; aliwaangamiza kabisa watu wote kwa ncha ya upanga.
Akamchukua Agagi, mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga.
9 Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi akiwa hai, pamoja na kondoo wazuri, ng'ombe, ndama wanono, na wanakondoo. Kila kitu kilichokuwa kizuri, hawakukiangamiza. Bali waliangamiza kabisa chochote kilichodharaulika na kisicho na thamani.
Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi na kondoo na ngʼombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa.
10 Baadaye neno la BWANA likamjia Samweli, kusema,
Kisha neno la Bwana likamjia Samweli kusema:
11 “Inanihuzunisha kwamba nimemchagua Samweli awe mfalme, kwa maana aligeuka nyuma asinifuate na hakutekeleza maagizo yangu.” Samweli alikasirika; akamlilia BWANA usiku kucha.
“Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamlilia Bwana usiku ule wote.
12 Samweli aliamka mapema akutane na Sauli wakati wa asubuhi. Samweli aliambiwa, “Sauli alifika Karmeli na amejijengea ukumbusho kwa ajili yake, kisha aligeuka na kuendelea chini hadi Gilgali.” Ndipo
Asubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli amekwenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.”
13 Samweli akamwendea Sauli, na Sauli akamwambia, “Umebarikiwa na BWANA! Nami nimetekeleza amri ya BWANA.”
Samweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “Bwana akubariki! Nimetimiza yale Bwana aliniagiza.”
14 Samweli akasema, “Hicho kilio cha kondoo ni cha nini basi masikioni mwangu, na hiyo milio ya ng'ombe ninayosikia?
Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ngʼombe ninaousikia ni kitu gani?”
15 Sauli akamjibu, “Wao wamewaleta kutoka kwa Waamaleki. Kwa sababu watu waliwaacha hai kondoo wazuri na ng'ombe, kwa ajili ya sadaka kwa BWANA Mungu wako. Zilizobaki tuliziangamiza kabisa.”
Sauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ngʼombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.”
16 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, “Subiri nitakumbia kile ambacho BWANA amekisema kwangu usiku.” Sauli akamwambia, “Sema!”
Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lile Bwana aliloniambia usiku huu.” Sauli akajibu, “Niambie.”
17 Samweli akasema, “Ingawa wewe ni mdogo machoni pako mwenyewe, je, hukufanywa mkuu wa kabila za Israeli? Na BWANA akakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli;
Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa kabila za Israeli? Bwana alikutia mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli.
18 BWANA alikutuma katika safari yako akisema, 'nenda na uangamize kabisa wenye dhambi, Waamaleki, na upigane dhidi yao hadi wameangamizwa.'
Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita mpaka utakapowaangamiza kabisa.’
19 Kwa nini basi haukuitii sauti ya BWANA, bali badala yake ulishikilia nyara na ukafanya uovu machoni pa BWANA?”
Kwa nini hukumtii Bwana? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa Bwana?”
20 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Kweli kabisa niliitii sauti ya BWANA, Na nimeifuata njia ambayo BWANA alinituma. Nimemteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, na kuwaangamiza kabisa Waamaleki.
Sauli akasema, “Lakini nilimtii Bwana. Nilikamilisha ile kazi ambayo Bwana alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao.
21 Lakini watu walichukua baadhi ya nyara-kondoo na ng'ombe, na vitu vizuri vilivyokusudiwa kuangamizwa, ili wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali.”
Askari walichukua kondoo na ngʼombe kutoka kwenye nyara, zile ambazo ni nzuri sana zimewekwa wakfu kwa Mungu, ili zitolewe dhabihu kwa Bwana Mungu wako huko Gilgali.”
22 Samweli akajibu, “Je, BWANA hufurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama ilivyo kuitii sauti yake? Utii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia ni bora kuliko mafuta ya beberu.
Lakini Samweli akajibu: “Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama vile kuitii sauti ya Bwana? Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu, nako kusikia ni bora kuliko mafuta ya kondoo dume.
23 Kwa maana uasi ni sawa na dhambi ya uchawi, na ukaidi ni sawa na uovu na udhalimu. Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, naye pia amekukataa usiwe mfalme.”
Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. Kwa sababu umelikataa neno la Bwana, naye amekukataa wewe kuendelea kuwa mfalme.”
24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi; kwa maana nimevunja amri ya BWANA na maneno yako, kwa sababu niliwaogopa watu na kuitii sauti yao.
Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Bwana na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka.
25 Sasa, tafadhali nisamehe dhambi yangu, na urudi nami ili nipate kumcha BWANA.”
Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana.”
26 Samweli akamwambia Sauli, “Sitarudi pamoja na wewe; kwa sababu umekataa neno la BWANA, naye BWANA amekukataa usiwe mfalme juu ya Israeli.”
Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la Bwana, naye Bwana amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!”
27 Samweli alipogeuka kuondoka, Sauli akashika pindo la kanzu yake, na likachanika.
Samweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akangʼangʼania pindo la joho lake, nalo likararuka.
28 Samweli akamwambia, “BWANA ameuchana ufalme wa Israeli kutoka kwako leo na amempa ufalme huo jirani yako, aliye bora kuliko wewe.
Samweli akamwambia, “Bwana ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe.
29 Pia, yeye ni Uwezo wa Israeli hatasema uongo wala kubadili nia yake; kwa sababu si mwanadamu, kwamba abadili nia yake.”
Yeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.”
30 Kisha Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali nipe heshima wakati huu mbele ya wakuu wa watu wangu na mbele ya Israeli. Urudi tena pamoja nami, kusudi niweze kumcha BWANA, Mungu wako.”
Sauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana Mungu wako.”
31 Hivyo Samweli akamrudia tena Sauli, na Sauli akamcha BWANA.
Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabudu Bwana.
32 Kisha Samweli akasema, “Mmlete hapa kwangu Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akafika kwake akiwa amefungwa minyororo na kusema, “Hakika uchungu wa kifo umepita.”
Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.”
33 Naye Samweli akamjibu, “Jinsi upanga wako ulivyofanya wanawake wapoteze watoto, vivyo hivyo mama yako naye hatakuwa na mtoto miongoni mwa wanawake.” Kisha Samweli akamkata Agagi vipande vipande mbele za BWANA huko Gilgali.
Lakini Samweli akasema, “Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, ndivyo mama yako atakavyokuwa hana mtoto miongoni mwa wanawake.” Naye Samweli akamuua Agagi mbele za Bwana huko Gilgali.
34 Samweli akaenda Rama, na Sauli akapanda kwenda nyumbani kwake Gibea ya Sauli.
Kisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli.
35 Samweli hakumuona tena Sauli hadi siku ya kifo chake, lakini alimwombolezea Sauli. Na BWANA alijuta kwa kumfanya Sauli awe mfalme juu ya Israeli.
Hadi siku Samweli alipofariki hakwenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwombolezea. Naye Bwana alihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli.