< 1 Samweli 11 >

1 Ndipo Nahashi Mwamoni akaenda na kupiga kambi kuzunguka Yabeshi Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia,”
Nahashi yule Mwamoni, akakwea kuuzunguka kwa jeshi mji wa Yabeshi-Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba na sisi, na tutakuwa chini yako.”
2 Nahashi Mwamoni akawajibu, “Kwa sharti hili nitafanya mkataba na ninyi, kwamba wote niwang'oe macho ya kulia, na kwa kitendo hiki kilete fedheha katika Israeli yote.”
Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitangʼoa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.”
3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, “Tuache kwa siku saba, ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Ndiposa, kama hakuna mtu wa kutuokoa, tutasalimu amri kwako.”
Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote, kama hakuna hata mmoja anayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.”
4 Nao wajumbe wakafika Gibea, alipoishi Sauli, na wakawaeleza watu kile kilichotokea. Watu wote wakalia kwa sauti kuu.
Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa juu ya masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa.
5 Na Sauli alikuwa akiwafuata nyuma maksai kutoka shambani. Sauli akauliza, “Watu wamepatwa na nini hadi wanalia?” Ndipo wakamweleza Sauli kile ambacho watu wa Yabeshi walikisema.
Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza jinsi watu wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.
6 Sauli aliposikia kile walichosema, Roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, na akakasirika.
Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira.
7 Akashika nira ya maksai, akawakata hao ng'ombe vipande vipande, na akavituma hivyo vipande katika nchi yote ya Israeli kwa kuwatumia wajumbe, Akasema, “Yeyote asiyejitokeza akimfuata Sauli na Samweli, hivi ndivyo ng'ombe wake watakavyofanywa.” Na hofu ya BWANA ikawaingia watu, na wakajitokeza wote kwa pamoja.
Akachukua jozi ya maksai na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha hofu ya Bwana ikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja.
8 Alipowahesabu hapo Beseki, watu wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na watu wa Yuda elfu thelathini.
Sauli alipowakusanya huko Bezeki, watu wa Israeli walikuwa 300,000 na watu wa Yuda 30,000.
9 Wakawaambia wale wajumbe waliotumwa, “Mtawaambia watu wa Yabeshi Gileadi, 'Kesho, wakati wa jua kali, Mtaokolewa.”' Basi wale wajumbe wakaenda na kuwaambia watu wa Yabeshi, na watu wakafurahi.
Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni watu wa Yabeshi-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’” Wajumbe walipokwenda na kutoa taarifa hii kwa watu wa Yabeshi, wakafurahi.
10 Ndipo watu wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, “Kesho tutasalimu amri kwako, na utaweza kutufanyia chochote unachoona kinakupendeza.”
Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.”
11 Siku iliyofuata Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu. Wakafika katikati ya Kambi wakati wa asubuhi, wakawashambulia na kuwashinda Waamoni ilipofika mchana. Waliosalimika nao walitawanyika, kiasi kwamba hata watu wawili hawakuachwa pamoja.
Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja mpaka mchana. Wale walionusurika wakasambaa, kiasi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja.
12 Ndipo watu wakamwambia Samweli, “Wako wapi waliosema, 'Hivi kweli Sauli atatutawala?' Walete watu hao, ili tuwauwe.”
Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatawala juu yetu?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.”
13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna atakayeuwawa siku ya leo, kwa sababu leo BWANA amemuokoa Isreli.”
Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii Bwana ameokoa Israeli.”
14 Kisha Samweli akawaambia watu, “Njoni, twendeni Gilgali na tuimarishe ufalme tena huko.”
Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.”
15 Hivyo watu wote wakaenda Gilgali na wakamsimika Sauli kuwa mfalme mbele za BWANA huko Gilgali. Na huko walitoa sadaka za amani mbele za BWANA, na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.
Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele za Bwana. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Bwana, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa.

< 1 Samweli 11 >