< 1 Petro 3 >

1 Kwa njia hii, ninyi ambao ni wake mnapaswa kujitoa kwa waume zenu wenyewe, ili, hata kama baadhi yao hawajalitii neno, kupitia tabia za wake zao wanaweza kuvutwa pasipo neno, 2 kwa sababu wao wenyewe watakuwa wameiona tabia yenu njema pamoja na heshima. 3 Hii ifanyike siyo kwa mapambo ya nje—kusuka nywele, vito vya dhahabu, au mavazi ya mtindo. 4 Lakini badala yake ifanyike kwa utu wa ndani wa moyo, na kuzidi katika uzuri wa unyenyekevu na utulivu wa moyo, ambao ni wa thamani mbele za Mungu. 5 Kwa kuwa wanawake watakatifu walijipamba wenyewe kwa njia hii. Walikuwa na imani katika Mungu na waliwatii waume zao wenyewe. 6 Kwa njia hii Sara alimtii Ibrahamu na kumwita yeye “bwana” wake. Ninyi sasa ni watoto wake kama mtafanya yaliyo mazuri na kama hamwogopi mabaya. 7 Kwa njia hiyo hiyo, ninyi wanaume mnapaswa kuishi na wake zenu mkijua kuwa wao ni wenzi wa kike dhaifu, mkiwatambua wao kama wapokeaji wenzenu wa zawadi ya uzima. Fanyeni hivi ili kwamba maombi yenu yasizuiliwe. 8 Hatimaye, ninyi nyote, muwe na nia moja, wenye huruma, upendo kama ndugu, wanyenyekevu, na wapole. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi. Kinyume chake, mwendelee kubariki, kwa sababu hii mliitwa, ili kwamba muweze kurithi baraka. 10 “Yeye atakaye kupenda maisha na kuona siku njema lazima auzuie ulimi wake kwa mabaya na midomo yake kusema hila. 11 Na ageuke na kuacha mabaya na kufanya yaliyo mazuri. Atafute amani na kuifuata. 12 Macho ya Bwana humwona mwenye haki na masikio yake husikia maombi yake. Lakini uso wa Bwana uko kinyume cha wale watendao uovu.” 13 Ni nani atakayewadhuru ninyi, ikiwa mwatamani lililo zuri? 14 Lakini kama mkiteseka kwa haki, mmebarikiwa. Msiogope yale ambayo wao wanayaogopa. Msiwe na wasiwasi. 15 Badala yake, mmuweke Kristo Bwana katika mioyo yenu kama mtakatifu. Kila mara muwe tayari kumjibu kila mtu anayewauliza ninyi kwa nini mna tumaini katika Mungu. Fanyeni hivi kwa upole na heshima. 16 Muwe na dhamiri njema ili kwamba watu wanaotukana maisha yenu mema katika Kristo waweze kuaibika kwa sababu wanaongea kinyume dhidi yenu kama kwamba mlikuwa watenda maovu. 17 Ni vizuri zaidi, ikiwa Mungu anatamani, kwamba mwateseka kwa kufanya mema kuliko kwa kufanya mabaya. 18 Kristo pia aliteseka mara moja kwa ajili ya dhambi. Yeye ambaye ni mwenye haki aliteseka kwa ajili yetu, ambao hatukuwa wenye haki, ili kwamba atulete sisi kwa Mungu. Alikufa katika mwili, lakini alifanywa mzima katika roho. 19 Katika roho, alikwenda na kuzihubiri roho ambazo sasa ziko kifungoni. 20 Hazikuwa tiifu wakati uvumilivu wa Mungu ulipokuwa unasubiri wakati wa Nuhu, siku za ujenzi wa safina, na Mungu aliokoa watu wachache—nafsi nane—kutoka katika maji. 21 Hii ni alama ya ubatizo unaowaokoa ninyi sasa, siyo kama kuosha uchafu kutoka mwilini, lakini kama ombi la dhamiri njema kwa Mungu, kupitia ufufuo wa Yesu Kristo. 22 Yeye yuko mkono wa kuume wa Mungu. Alikwenda mbinguni. Malaika, mamlaka, na nguvu lazima vimtii yeye.

< 1 Petro 3 >