< 1 Petro 2 >
1 Kwa hiyo wekeni pembeni uovu wote, udanganyifu, unafiki, wivu na kashifa.
2 Kama watoto wachanga, mtamani maziwa safi ya kiroho, ili kwamba mweze kukua ndani ya wokovu,
3 kama mmeonja kwamba Bwana ni mwema.
4 Njoni kwake aliye jiwe hai linaloishi ambalo limekataliwa na watu, lakini hilo limechaguliwa na Mungu na ni la thamani kwake.
5 Ninyi pia ni kama mawe yaliyo hai yanayojengwa juu kuwa nyumba ya kiroho, ili kuwa ukuhani mtakatifu ambao hutoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa kwa Mungu kupitia Yesu Kristo.
6 Andiko husema hivi, “Tazama, nimeweka katika Sayuni jiwe la pembeni, kuu na lililochaguliwa na la thamani. Yeyote aaminiye katika yeye hataona aibu”.
7 Hivyo heshima ni yenu kwenu ninyi mnaoamini. Lakini, “jiwe lililokataliwa na wajenzi, hili limekuwa jiwe kuu la pembeni”-
8 na, “jiwe la kujikwaa na mwamba wa kujikwaa.”Wao hujikwaa, wanaolikataa neno, kwa lile ambalo pia walikuwa wameteuliwa kwalo.
9 Lakini ninyi ni ukoo uliochaguliwa, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa miliki ya Mungu, ili kwamba mweze kutangaza matendo ya ajabu ya yule aliyewaita kutoka gizani kuja kwenye nuru yake ya ajabu.
10 Ninyi kwanza hamkuwa watu, lakini sasa ninyi ni watu wa Mungu. Ninyi hamkupokea rehema, lakini sasa mmepokea rehema.
11 Wapendwa, nimewaita kama wageni na wazurujaji kujinyima kutoka kwenye tamaa mbaya za dhambi, ambazo zinapigana vita na roho zenu.
12 Mnapaswa kuwa na tabia njema kati ya mataifa, ili kwamba, kama watawasema kama kwamba mmefanya mambo maovu, wataziangalia kazi zenu njema na kumsifu Mungu katika siku ya kuja kwake.
13 Tii kila mamlaka ya mwanadamu kwa ajili ya Bwana, ikiwa mfalme kama mkuu,
14 ikiwa watawala waliotumwa kuwaadhibu watenda mabaya na kuwasifu wale wanaotenda mema.
15 Kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kufanya mema mwanyamazisha mazungumzo ya kipuuzi ya watu wapumbavu.
16 Kama watu huru, msiutumie uhuru wenu kama kifuniko kwa maovu, bali muwe kama watumishi wa Mungu.
17 Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mwogopeni Mungu. Mweshimuni mfalme.
18 Watumwa, watiini bwana zenu kwa heshima yote, siyo tu bwana walio wazuri na wapole, lakini pia walio waovu.
19 Kwa kuwa ni sifa kama yeyote atavumilia maumivu wakati anapoteseka pasipo haki kwa sababu ya dhamiri yake kwa Mungu.
20 Ni faida gani iliyopo kama mwadumu kutenda dhambi kisha mwendelee kuadhibiwa? Lakini kama mmefanya mema na ndipo mteseke kwa kuhukumiwa, hii ni sifa njema kwa Mungu.
21 Kwa hili mliitwa, kwa sababu Kristo pia aliteswa kwa ajili yenu, amewaachia mfano kwa ajili yenu kufuata nyayo zake.
22 Yeye hakufanya dhambi, wala haukuonekana udanganyifu wowote kinywani mwake.
23 Wakati yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano, alipoteseka, hakutisha bali alijitoa mwenyewe kwake Yeye ahukumuye kwa haki.
24 Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake kwenye mti, ili kwamba tusiwe na sehemu tena katika dhambi, na kwamba tuishi kwa ajili ya haki. Kwa kupigwa kwake ninyi mmepona.
25 Wote mliokuwa mkitangatanga kama kondoo aliyepotea, lakini sasa mmerudi kwa mchungaji na mlinzi wa roho zenu.