< 1 Wafalme 8 >
1 Kisha Sulemani akawakusanya wazee wa Israeli, wakuu wote wa makabila, na viongozi wa familia za wana wa Israeli, mbele yake kuleYerusalemu, ili waliingize ndani lile sanduku la agano la BWANA kutoka mji wa Daudi, ambao ni Sayuni.
Kisha Mfalme Solomoni akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Bwana kutoka Sayuni, Mji wa Daudi.
2 Wanaume wote wa Israeli walikusanyika mbele ya mfalme Sulemani kwenye sherehe, katika mwezi wa Ethanim, ambao ndio mwezi wa saba.
Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Solomoni wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
3 Wazee wote wa Israeli walikuja, na makuhani wakalibeba lile sanduku.
Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika Sanduku la Agano,
4 Wakalileta lile sanduku la BWANA, lIle hema la kukutania na mapambo yote matakatifu ambayo yalikuwa kwenye hema. Makuhani na Walawi wakavileta vitu hivi.
nao wakalipandisha Sanduku la Bwana, na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba,
5 Mfame Sulemani na mkutano wote wa Israeli wakaja pamoja mbele ya sanduku, wakatoa sadaka za kondoo na makisai ambazo hazikuweza kuhasabika.
naye Mfalme Solomoni na kusanyiko lote la Israeli waliokusanyika kumzunguka walikuwa mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu nyingi za kondoo na ngʼombe ambao idadi yao haikuwezekana kuandikwa au kuhesabiwa.
6 Makuhani wakalingiza ndani lile sanduku la agano la BWANA na wakaliweka mahali pake, ndani ya chumba cha ndani, patakatifu sana, chini ya yale mabawa ya makerubi.
Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Bwana hadi mahali pake ndani ya sehemu takatifu ndani ya Hekalu, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi.
7 Kwa kuwa makerubi walitandaza mabawa yao hadi mahali pa sanduku la agano, na walifunika sanduku na miti yake kwani ilitumika kulibeba.
Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea.
8 Ile miti ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba miishio yake ilionekana tokea kwenye eneo takatifu mbele ya chumba cha ndani, lakini haikuweza kuonekana kutokea nje. Miti hiyo iko mpaka leo.
Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo.
9 Ndani ya sanduku hapakuwemo na kitu chochote isipokuwa vile vidonge vya mawe ambavyo Musa aliviweka alipokuwa mlima Horebu, wakati BWANA alipofanya agano na watu wa Israeli walipotoka kwenye nchi ya Misri.
Ndani ya Sanduku hapakuwepo kitu kingine chochote isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo Mose alikuwa ameziweka ndani yake huko Horebu, mahali ambapo Bwana alifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
10 Ilitokea kwamba wakati makuhani walipotoka mahali patakatifu, lile wingu lilifunika hekalu la BWANA.
Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la Bwana.
11 Makuhani hawakuweza kusimama kwa ajili ya kutumika kwa sababu utukufu wa BWANA ulifunika hekalu.
Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu lake.
12 Kisha Sulemani akasema, “BWANA amsema kuwa anaweza kuishi hata kwenye giza nene,
Ndipo Solomoni akasema, “Bwana alisema kwamba ataishi katika giza nene;
13 Lakinni nimekujengea makao ya kujivunia, mahali pako pa kuishi milele.”
naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.”
14 Kisha mfalme akageuka na kuwabariki mkusanyiko wa watu wa Israeli, wakati huo mkusanyiko wa Waisraeli walikuwa wamesimama.
Kusanyiko lote la Israeli lilipokuwa limesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki.
15 Akasema, “BWANA, Mungu wa Israeli, asifiwe, ambaye alisema na baba yangu Daudi, na ametimiza kwa mikono yake, akisema,
Kisha akasema: “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema,
16 'Tangu siku ile niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji wowote toka kwa makabila yote ya Israeli ambako ningeijenga nyumba, kwa ajili ya jina langu kuwemo humo. Hata hivyo, nilimchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.
‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo ili Jina langu lipate kuwamo humo, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’
17 Sasa ilikuwa kwenye moyo wa Daudi baba yangu kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
“Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
18 Lakini BWANA alimwambia baba yangu Daudi, 'Ilikuwa ndani ya moyo wako kunijengea nyumba kwa jina langu, ulifanya vyema kwa hilo kuwa ndani ya moyo wako.
Lakini Bwana akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako.
19 Ingawa hutanijengea nyumba; badala yake mwanao, mmoja wa wanao atakayezaliwa toka viunoni mwako, atanijengea nyumba kwa jina langu,'
Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea hekalu, bali mwanao, ambaye ni nyama yako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
20 BWANA amelibeba lile neno slilokuwa amesema, kwa kuwa nimeinuka mahali pa baba yangu Daudi, na nimeketi kwenye kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi. Nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
“Bwana ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Bwana alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
21 Nimetengeneza mahali kwa ajili ya sanduku ndani yake, ambamo ndani yake kuna agano la BWANA, ambalo alifanya na baba zetu alipowatoa toka nchi ya Misri,”
Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambamo ndani yake kuna lile Agano la Bwana alilofanya na baba zetu wakati alipowatoa Misri.”
22 Sulemani alisimama mbele ya madhabahu ya BWANA, mbela ya mkusanyiko wote wa Waisraeli, naye akanyosha mikono yake kuelekea mbinguni.
Kisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana machoni pa kusanyiko lote la Israeli, akakunjua mikono yake kuelekea mbinguni
23 Akasema, “BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni au chini duniani, ambaye hutunza agano lake kwa uaminifu kwa watumishi wako ambao hutembea mbele yako kwa mioyo yao yote;
na kusema: “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza Agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.
24 wewe ambaye umetunza ahadi yako na mtumishi wako Daudi baba yangu ile uliyomwahidi. Naam, ulisema kwa kinywa chako na sasa umeitimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.
25 Sasa basi, BWANA, Mungu wa Israeli, timiza kile ulichomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu, pale uliposema, 'Hautashindwa kunipa mtu mbele ya macho yangu ambaye ataketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama tu uzao wako watakuwa waangalifu kutembea mbele yangu, kama vile wewe ulivyotembea mbele yangu.'
“Sasa Bwana, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’
26 Sasa basi, Mungu wa Israeli, Ninaomba kwamba ile ahadi uliyofanya kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, itimie.
Sasa, Ee Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie.
27 Je, ni kweli kwamba Mungu ataishi duniani? Tazama, Ulimwengu wote na mbingu hazikutoshi - sembuse nyumba hii niliyoijenga!
“Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga!
28 Kwa hiyo Mungu naomba uyajali maombi haya ya mtumishi wako na maombi yake, BWANA, Mungu wangu; sikiliza kilio na maombi ambayo mtumishi wako anakuomba leo.
Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, Ee Bwana Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo.
29 Naomba ulitazame hekalu hili mchana na usiku, mahali ambapo ulisema, 'Jina langu na uwepo wangu utakuwa' - ili niweze kuwa nasikiliza maombi ambayo mtumishi wako ataomba mahali hapa.
Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa.
30 Kwa hiyo sikia maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli tunapokuwa tunaomba mahali hapa. Ndiyo, sikia kutokea mahali ambapo unaishi, kutoka katika mbingu za mbingu; na unaposikia tafadhali samehe.
Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe.
31 Kama mtu atamtendea uovu jirani yake na anapewa sharti la kiapo, na kama atakuja na kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii,
“Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili,
32 basi usikie kutoka mbinguni ukatende na kuwahukumu watumishi wako, ukamhukumu mwovu, ili kuwaletea tabia zake kichwani mwake, na kumtunza mwenye haki kuwa hana hatia, na kumpa thawabu yake ya haki.
basi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake.
33 Watu wako Israeli watakapopigwa na adui kwa sabau ya kutenda dhambi dhidi yako, na kama watakurudia, na kulikiri jina lako, na kukusihi, na kuomba msamaha kwako katika hekalu hili-
“Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili,
34 tafadhali nakuomba usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi za watu wako Israeli; uwarudishe katika nchi ambayo uliwapa mababu zao.
basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.
35 Kama mbingu zitafungwa na mvua hazinyeshi kwa sababu watu wamekutenda dhambi wewe - na kama wataomba mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kugeuka toka dhambi zao na kama umewapiga -
“Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu,
36 basi sikia tokea mbinguni na usamehe dhambi za watumishi wako na za watu wako Israeli, utakapowafundisha njia njema inayowapasa; basi uinyeshee mvua nchi yako, ambayo uliwapa watu wako kuwa urithi.
basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.
37 Na kama kuna njaa katika nchi, au kama kuna magonjwa, au ukungu, nzige au funza; au kama adui atavamia malango ya mji katika nchi yao, kama kuna tauni au magonjwa yeyote -
“Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia,
38 na kama kuna mtu au wata wa Israeli wataomba - kila mmoja akaijua hiyo tauni katika moyo wake wakati akinyosha mikono yake katika hekalu hili.
wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akitambua taabu za moyo wake mwenyewe, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili:
39 Basi usikie kutoka mbinguni, mahali unapoishi, utende na kusamehe, na umpe kila mtu thawabu anayostahili kwa kile anachofanya; wewe unajua moyo wake, kwa sababu ni wewe pekee yako ujuaye mioyo ya watu.
basi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote),
40 Fanya hivi ili kwamba wawe na hofu kwako katika siku zote za maisha yao wanayoishi katika nchi uliyowapa mababu zetu.
ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
41 Na nyongeza yake, kuhusiana na mgeni ambaye si mtu wako wa Israeli: atakapokuja kutokea nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako -
“Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako,
42 kwa sababu watasikia jina lako lilivyo kuu, mkono wako wenye nguvu, na mkono wako ulioinuliwa - atakapokuja na kuomba mahali hapa pa hekalu,
kwa maana watu watasikia juu ya Jina lako kuu na juu ya mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili,
43 tafadhali usikie kutokea katika mbingu, mahali unapoishi, na umfanyie huyo mgeni akuombacho. Fanya hivi ili makundi ya wtu wote duniani wakujue jina lako na kukuhofia, kama wanavyofanya watu Israeli. Fanya hivyo ili wajue kwamba nyumba hii niliyoijenga inaitwa kwa jina lako.
basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.
44 Na kama watu wko wataenda vitani dhidi ya adui, kwa njia yeyote unayoweza kuwatuma, na kama watakuomba wewe, BWANA, kuelekea mji huu uliuchagua, na kuekea nyumba ambayo nimeijenga kwa jina lako.
“Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa Bwana kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako,
45 Basi sikia tokea mbinguni maombi yao, dua zao, na uwasaidie wanachohitaji.
basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao.
46 Na kama watafanya dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna hata mtu mmoja asiyefanya dhambi, na kama una hasira dhidi yao na kuwapeleka kwa maadui, ili kwamba maadui wawachukue mateka katika nchi yao, mbali au karibu.
“Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu yeyote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu;
47 Na kama watatambua kuwa wako katika nchi ya utumwa, na kama watatubu na kuomba neema kwako kutokea katika nchi ya watekaji. Na kama watasema, 'tumetenda kwa ukaidi na tumefanya dhambi. Tumetenda kwa uovu.'
na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda uovu’;
48 Na kama watarudi kwako kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote katika chi ya maadui ambao wanawakamata, na kama watakuomba wewe kuelekea nchi yao, ambayo uliwapa mababu zao, na kuelekea katika mji uliouchagua, nakuelekea kaika nyumba ambayo nimeijenga kwa jina lako.
kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako;
49 Basi usikie maombi yao, na dua zao tokea mbinguni, mahali unapoishi, na ukaitetee haki yao.
basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na kuitetea haki yao.
50 Wasamehe watu wako waliotenda dhambi dhidi yako, na dhambi zao zote ambazo kwazo wamekukosea wewe dhidi ya amri zako. Uwahurumie mbele ya maadui zao ambao waliwachukua mateka, ili kwamba maadui zao pia wawahurumie watu wako.
Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma;
51 Hawa ni watu wako uliowachagau, ambao uliwaokoa toka nchi ya Misri kama kwamba walikuwa katikati ya tanuru amabamo vyuma huyeyushwa.
kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka kwenye lile tanuru la kuyeyushia chuma.
52 Naomba kwamba macho yako yatazame dua za mtumishi wako na kwa dua za watu wako Issraeli, ili uwasike kila wanapokulilia.
“Macho yako na yafumbuke juu ya ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wowote wanapokulilia.
53 Kwa kuwa uliwatenga toka kwa watu wengine wa duniani ili wawe wako nakupokea ahadi zako, kama vile ulivyomwambia Musa mtumishi wako, wakati ulipowatoa babazetu toka Misri, BWANA.”
Kwa maana uliwachagua wao kutoka mataifa yote ya ulimwengu kuwa urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Mose wakati wewe, Ee Bwana Mwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.”
54 Kwa hiyo ilitokea wakati Sulemaeni alipomaliza kuomba maombi haya na dua zake kwa BWANA, aliamka toka madhabahu ya BWANA, pale alipokuwa amepiga magoti na mikono yake ikiwa imenyoshwa kuelekea mbinguni.
Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwa Bwana, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya Bwana, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni.
55 Alisimama na kuubariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, alisema,
Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa akisema:
56 “Asifiwe BWANA, aliywapatia pumziko watu hawa Israeli, akitunza ahadi zake zote. Hakuna hata moja ambayo haijatekelezwa katika ahadi njema za BWANA ambazo aliahidi akiwa na Musa mtumishi wake.
“Ahimidiwe Bwana, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose.
57 BWANA, mungu wetu awe pamoja nasi, kama alivyokuwa pamoja na mababu zetu. Asituache wala kututelekeza,
Bwana Mungu wetu na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa.
58 kwamba aunganishe mioyo yetu na yeye, ili tuishi katika njia zake na kuzishika amri zake na taratibu zake na maagizo yake, ambayo aliwaagiza baba zetu.
Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kuzishika amri na maagizo na masharti aliyowapa baba zetu.
59 Na maeneo haya ambayo nimesema, ambayo nimesihi mbele ya BWANA, yawe karibu n a BWANA, Mungu wetu usiku na mchana, ili kwamba awasadie katika haki za mtumishi wake na haki za watu wake Israeli, kama watakavyoomba kila siku;
Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za Bwana, yawe karibu na Bwana Mungu wetu usiku na mchana, ili kwamba atetee shauri la mtumishi wake na la watu wake Israeli kulingana na hitaji lao la kila siku,
60 kwamba watu wote duniani wajue kwamba BWANA, ndiye Mungu, na hakuna Mungu mwingine!
ili kwamba mataifa yote ya dunia wajue kwamba Bwana ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine.
61 Kwa hiyo ifanyeni mioyo yenu iwe ya haki mbele ya BWANA. Mungu wetu, ili tutembee katika maagizo na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.
Lakini ni lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa Bwana Mungu wetu, kuishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.”
62 Kwa hiyo mfalme na watu wote pamoja naye wakatoa sadaka kwa BWANA.
Kisha mfalme na Israeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za Bwana.
63 Sulemani akatoa sadaka ya amani, ambayo aliifanya kwa BWANA: Nayo ilikuwa makisai elfu ishirini na mbili, na kondoo 120, 000. Kwa hiyo mfalme na watu wa Israeli wakaiweka wakfu nyumba ya BWANA.
Solomoni akatoa dhabihu sadaka za amani kwa Bwana: ngʼombe 22,000, pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la Bwana.
64 Siku hiyo mfalme aliweka wakfu behewa ya katikati mbele ya hekalu la BWANA, kwa kuwa pale ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za unga, na sadaka za mafuta ya amani, kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele ya BWANA ilikuwa ndogo sana kwa sadaka za kuteketezwa, sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani.
Siku iyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Bwana na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za Bwana ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka ya amani.
65 Kwa hiyo Sulemani akafanya sherehe wakati huo, Nayo Israeli yote pamoja naye, mkutano mkubwa, kutoka Lebo Hamathi hadi kijito cha Misri, wakaja mbele ya BWANA, Mungu wetu kwa muda wa siku saba na pia kwa siku saba zingine, ambayo jumla yake ni siku kumi na nne.
Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za Bwana Mungu wetu kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani, jumla siku kumi na nne.
66 Na ilipofika siku ya nane aliwatawanya watu, nao wakambariki mfalme kisha wakaenda nyumbani kwao kwa furaha na mioyo ya shangwe kwa wema wote ambao BWANA alimwonyesha Daudi, mtumishi wake, na kwa watu wake, Israeli.
Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani, wakiwa na mashangilio na furaha rohoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo Bwana ametenda kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.