< 1 Wafalme 3 >
1 Sulemani akawa na ushirikiano wa kindoa na Farao mfalme wa Misri. Alimwoa binti wa Farao na kumleta katika mji wa Daudi mpaka alipomaliza kujenga nyumba yake, nyumba ya BWANA, na ukuta wa Yerusalemu.
Solomoni akafanya urafiki na Mfalme Farao wa Misri na kumwoa binti yake. Akamleta huyo binti katika Mji wa Daudi mpaka alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Bwana, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu.
2 Watu walikuw wakitoa sadaka kwenye maeneo ya juu, kwa sababu hapakuwa bado na nyumba iliyokuwa imejengwa kwa jina la BWANA.
Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye vilima, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Bwana.
3 Sulemani alionyesha upendo wake kwa BWANA kwa kutembea katika maagizo ya Daudi baba yake, isipokuwa tu alitoa dhabihu na kuchoma uvumba mahali pa juu.
Solomoni akaonyesha upendo wake kwa Bwana kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu.
4 Mfalme akaenda Gibioni kutoa sadaka kule, kwa kuwa hilo ndilo lilikuwa eneo kuu la juu. Sulemani katoa sadaka maelfu katika madhabu hiyo.
Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia, naye Solomoni akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu.
5 BWANA akaonekana kwa Sulemani huko Gibioni katika ndoto ya usiku; akasema, “Omba! uanataka nikupe nini?”
Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”
6 Kwa hiyo Sulemani akasema, “umeonyesha uaminifu wa agano mkuu kwa mtumishi wako, Daudi baba yangu, kwa sababu alitembea mbele yako kwa ukweli na uaminifu, katika haki ya moyo na katika unyofu wa moyo. Umetunza kwa ajili yake hili agano kuu kwa uaminifu na umempa mwana wake kuketi kwenye kiti chake cha enzi leo.
Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.
7 Na sasa, BWANA, Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako kuwa mfalme katika nafasi ya Daudi baba yangu, japo mimi ni mtoto mdogo. Sijui namna ya kuiingia na kutoka.
“Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu.
8 Mtumishi wako yuko katikati ya watu wako uliowachagua, kundi kubwa, watu wangi wasiohesabika.
Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao.
9 Kwa hiyo umpe mtumishi wako moyo wa uelewa wa kuwahukumu watu wako. Kwani ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi?”
Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”
10 Ombi hili la Sulemani likampendeza Bwana.
Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili.
11 Kwa hiyo Mungu akamwambia. “Kwa sababu umeomba jambo hili na haujajiombea maisha marefu au utajiri au uhai wa maadui wako, lakini umeomba ufahamu wa kutambua hukumu ya haki,
Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki,
12 Tazama sasa nitafanya yote uliyoniomba wakati uliponipa ombi lako. Ninakupa moyo wa hekima na ufahamu, kwa kuwa hapajawahi kuwa na mtu wa kuwa kama wewe kabla yako, na hakuna wa kuwa kama wewe atakayeinuka baada yako.
nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako.
13 Pia ninakupa hata ambayo hujaomba, vyote heshima na utajiri, ili kwamba pasije pakawa na mfalme wa kuwa kama wewe katika siku zako zote.
Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme.
14 Kama utatembea katika njia zangu na kuyatunza maagizo yangu na maagizo yangu, kama alivyofanya baba yako Daudi, ndipo nitakapoziongeza siku zako.”
Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.”
15 Kisha Sulemani alipoamka, na tazama, ilikuwa ndoto. Akaja Yerusalemu na akasimama mbele ya sanduku na agano la Bwana. Akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, na akawafanyia sherehe watumishi wake wote.
Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto. Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.
16 Kisha wanawake wawili waliokuwa makahaba wakaja mbele ya mfalme wakasimama mbele yake.
Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake.
17 Mwanamke mmoja akasema, “Aa, bwana wangu, mwanamke huyu na mimi tunaishi katika nyumba moja, Nilizaa mtoto tukiwa pamoj na yeye katika nyumba yetu.
Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami.
18 Ikatokea siku ya tatu baada ya kujifungua na yeye akajifungua. Tulikuwa sisi tu. Hapakuwepo na mtu mwingine yeyote katika nyumba yetu, ila sisi tu wawili katika hiyo nyumba.
Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili.
19 Kisha mtoto wa mwanamke huyu akafa wakati wa usiku, kwa sababu alimlalia.
“Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia.
20 kwa hiyo akamka wakati huo wa usiku wa manane akamchukua mwanangu toka pembeni yangu, wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa usingizini, na akamlaza kwenye kifua chake, na akamlaza mtoto wake aliyekufa juu ya kifua changu.
Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu.
21 Asubuhi nilipoamka ili kumhudumia mwanangu, nikaona kuwa alikuwa amekufa. Lakini nilipomwangalia kwa makini wakati huo wa asubuhi, nikagundua kuwa hakuwa yule mwanangu niliyezaa,”
Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa.”
22 Yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana, Huyu aliye hai ndiye wangu. Na yule aliyekufa ndiye wako.” Yule mwanamke wa kwanza akasema, “Hapana, Yule mtoto aliyekufa ndiye mwanao, na huyu aliye hai ndiye wangu.” Hivi ndivyo walivyoongea mbele ya mfalme.
Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.” Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme.
23 Kisha mfalme akasema, “Mmoja wenu anasema, 'huyu aliye hai ni wangu, na kumbe mwanao ndiye aliye kufa,'na mwingine naye anasema, 'Hapana, mwanao ni yule aliyekufa, na mwanangu ni huyu aliye hai.'”
Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’”
24 Mfalme akasema, ''Nileteeni upanga.” Kwa hiyo wakaleta upanga kwa mfalme.
Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga.
25 Kisha mfalme akasema, “Mgawe mtoto aliye hai katika vipande viwili, na huyu mwanamke apewe nusu na yule mwingine naye apewe nusu.”
Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.”
26 Yule mwanamke mwenye mtoto aliyekuwa hai akamwambia mfalme, kwa kuwa moyo wake ulikuwa na huruma sana kwa mwanae, akasema, “Aa, bwana wangu, mpatie huyu mtoto aliye hai, na usimwue kamwe.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hatakuwa wangu wala wako. Mgawe.”
Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!”
27 Ndipo mfalme aliposema, “Mpe yule mwanamke wa kwanza mtoto aliye hai, na kamwe usimwue. Yeye ndiye mama wa mtoto huyu.”
Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimuue; ndiye mama yake.”
28 Israeli wote waliposikia hukumu ambayo mafalme ametoa, walimwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake kwa ajili ya kutoa kuhukumu.
Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.