< 1 Wafalme 22 >
1 Miaka mitatu ilipita bila kuwepo na vita kati ya Washami na Wisraeli.
2 Ikawa katika mwaka wa tatu, Yehoshafati mfalme wa Israeli akashuka kwa mfalme wa Isreli.
3 Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia watumishi wake, “Je, mnajua kuwa Ramothi Gileadi ni yetu, ila hatufanyi chochote kuitwaa kutoka kwenye mkono wa mfalme wa Shamu?”
4 Kwa hiyo akamwambia Yehoshafati, “Je, utakwenda na mimi katika vita huko Ramothi Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, na farasi wangu ni kama farasi wako.”
5 Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, “Tafadhali tafuta mwongozo kutoka neno la BWANA juu ya kile unachopaswa kufanya kwanza.”
6 Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii pamoja, walikuwa wanaume elfu nne, akawaambia, “Je, niende Ramothi Gileadi kupigana, au nisiende?” Nao wakamwambia, “Ivamie, kwa kuwa Bwana ataitoa katika mkono wa mfalme.”
7 Lakini Yehoshafati akasema, “Je, hapa hayupo nabii mwingine wa BWANA ambaye tunaweza kupata ushauri?”
8 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Bado kuna mtu mmoja ambaye tunaweza kupata ushauri toka kwa BWANA ili kusaidia, Makaya mwana wa Imla, lakini namchukia kwa sababu huwa hanitabirii mazuri yanayonihusu, ila hunitabiria matatizo tu.” Lakini Yehoshafat akasema, “mfalme na asiseme hivyo,”
9 Kisha mfalme wa Israeli akmwita akida na akamwamuru, “Kamlete Makaya mwana wa Imla, sasa hivi.”
10 Wakati huo Ahabu mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi kila mmoja kwenye kiti cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika eneo la wazi kwenye lango la kuingilia Samaria, na manabii walikuwa wakiwatabiria.
11 Sedekia mwana wa Kenaana akajitengenezea pembe za chuma akasema, “BWANA asema hivi: 'Kwa hili utawasukuma Washami mpaka watakapoisha.'”
12 Na manabii wengine wote wakasema hivyo, wakisema, “Ishambulie Ramothi Gileadi na ushinde, kwa kuwa BWANA ameiweka kwenye mkono wa mfalme.”
13 Yule mjumbe aliyeenda kumwita Makaya akamwambia, akisema, “Tazama sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja wanatabiri mambo mema kwa mfalme. Tafadhali maneno yako yawe kama yao ukaseme mambo mazuri.”
14 Makaya akajibu, “Kama BWANA aishivyo, kile BWANA atakachosema kwangu ndicho nitakachosema.'”
15 Naye alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, “Makaya, je twende Ramothi Gileadi kupigana, au tusiende?” Makaya akamjibu, “Ivamie na ushinde. BWANA ataitoa kwenye mkono wa mfalme.”
16 Kisha mfalme akamwambia. “Je, nikutake mara ngapi ili kuniapia ukweli kwa jna la BWANA?”
17 Makaya akasema, “Ninaiona Israeli yote imesambaa kwenye milima, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, na BWANA amesema, 'Hawa hawana mchungaji. Kila mtu na arudi nyumbani kwake kwa amani.'”
18 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Je sikukwambia kuwa huwa hanitabirii mambo mema yanayonihusu, ila majanga tu?”
19 Kisha Makaya akasema, “Kwa hiyo sikiliza neno la BWANA: Nimemwona BWANA akiwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi, na majeshi yote ya mbinguni yalikuwa yamesimama karibu yake upande wake wa kulia na upande wake wa kushoto.
20 BWANA akasema, 'Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili kwamba apande akafie Ramothi Gileadi? Na mtu mmoja akajibu kwa njia hii, na mwingine akajbu kwa njia ile.
21 Ndipo pepo moja akajitokeza, akasimama mbele ya BWANA, akasema, 'Mimi nitamdanganya.' BWANA akmwuliza, 'Kwa jinsi gani?'
22 Yule pepo akamjibu, 'Nitakwenda na kuwa roho idanganyayo katika vinywa vya manabii wake,' BWANA akamjibu, 'utaweza kumdanganya, na utafanikiwa. Nenda sasa ukafanye hivyo.'
23 Tazama sasa, BWANA ameweka roho idangayo kwenye vinywa vya hawa manabii wako, na BWANA ametangaza janga kwako.”
24 Kisha Sedekia mwana wa Kenaana, akaja, akamzabua Makaya shavuni, akasema, “Je, yule roho wa Bwana alitokaje kwangu ili asema na wewe?”
25 Makaya akasema, “Tazama, “utatambua hilo katika siku hiyo, utakapokimbilia katika chumba cha ndani kujificha.”
26 Mfalme wa Israeli akamwambia mtumishi wake, “Mkamate Makaya umpeleke kwa Amoni, liwali wa mji, na kwa mwanangu, Yoashi.
27 Mwambie, 'mfalme anasema mweke huyo gerezani na awe anampa mkate kidogo na maji kidogo, mpaka nitakaporudi salama.'”
28 Naye Makaya akasema, “Kama utarudi salama basi BWANA hajasema kupitia kinywa changu.” Na akaongeza, “Sikilizeni hili, ninyi watu.”
29 Ahabu, mfalme wa Israeli, na Yehoshafati mfalme wa Yuda, wamepanda Ramothi Gileadi.
30 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitajibadilisha mwenyewe niende vitani, lakini wewe uvae vazi lako la kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na akaenda vitani.
31 Naye mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru majemedari thelathini na mbili wa magari yake, akisema, “Msimwamgamize askari wa muhimu au ambaye si wa muhimu, badala yake mshambulieni mfalme wa Israeli tu.”
32 Ikawa wakati majemedari wa magari walipomwona Yehoshafati wakasema, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Wakageuka ili kumshambulia, kwahiyo Yehoshafati akapiga kelele.
33 Ikawa majemedari wa magari walipoona kuwa yeye hakuwa mfalme wa Israeli, wakamwacha.
34 Lakini mtu mmoja akavuta upinde wake kwa kubahatisha na akampiga mfalme wa Israeli katikati ya mwunganiko wa mavazi yake ya chuma. Ahabu akamawambia dereva wa gari lake, “geuza unirudishe kutoka vitani, kwa kuwa nimeumizwa sana.”
35 Vita ikawa mbaya sana siku hiyo na mfalme akalazwazwa garini mwake akiwakabili Washami. Akafa jioni hiyo. Damu ilimwagika kutoka kwenye jeraha lake ndani ya gari.
36 Ikawa wakati wa kuzama jua, kilio kikatawala kwa jeshi lote, wakisema, “Kila mtu arudi kwenye mji wake; na kila mtu arudi kwenye mkoa wake!”
37 Kwa hiyo mfalme Ahabu akafa na akaletwa Samaria, wakamzika huko Samaria.
38 Wakaliosha lile gari kwenye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake (hapa ni mahali ambapo makahaba waliogea), kama vile neno la BWANA lilivyokuwa limesema.
39 Kwa mambo mengine yanayohusisana na Ahabu, yote ambayo alifanya, ile nyumba ya pembe aliyojenga, na miji yote aliyojenga, je, hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio cha wafalme wa Israeli?
40 Kwa hiyo Ahabu akalala pamoja na mababu zake, na Ahaziya mwanae akawa mfalme mahali pake.
41 Kisha Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.
42 Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano alipoanza kutawala, na akatawala Yerusalemu kwa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba, binti wa Shilhi.
43 Akatembea katika njia za Asa, baba yake, hakuziacha; akafanya yaliyokuwa mema mbele ya macho ya BWANA. Lakini bado mahali pa juu palikuwa hapajabomolewa. Watu walikuwa bado wanaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba mahali pa juu.
44 Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli.
45 Kwa mambo mengine kuhusiana na Yehoshafati, na nguvu zake alizoonyesha, na jinsi alivyopigana vita, je, hayajaandikwa katika kitabu cha matukio cha wafalme wa Israeli?
46 Aliwaondoa kutoka katka nchi wale makahaba wa kipagani waliokuwa wamebaki katika siku za baba yake Asa.
47 Hapakuwepo mfalme katika Edomu isipokuwa kaimu mtawala.
48 Yehoshafati alijenga merikebu: ziende Tarshishi na Ofri kuleta dhahabu, lakini hazikusafiri kwa sababu zile merikebu zilivunjika kule Esioni Geberi. Kisha
49 Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Naomba watumishi wangu waende pamoja na watumishi wako merikebuni. “Lakini Yehoshafati hakuruhusu hilo.
50 Yehoshafati akalala na mababu zake na akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi, babu yake; Yoramu mwanawe akawa mfalme mahali pake.
51 Ahazia mwana Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli ya Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa mfalme Yehoshafati mfalme wa Yuda, na akatawala kwa mika miwili juu ya Israeli.
52 Naye akafanya yaliyo maovu mbele ya macho ya BWANA akatembea katika njia za baba yake, katika njia za mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwazo aliifanya Israeli kufanya dhambi.
53 Alimtumikia Baali na kumwabudu na kwa hiyo akamghadhabisha BWANA, Mungu wa Israeli, katika hasira, kama vile baba yake alivyofanya.