< 1 Wafalme 21 >

1 Basi ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu kule Yezreeli, karibu na ikulu ya Ahabu, mfalme wa Samaria.
Baada ya hayo, Nabothi, Myezreeli, alikuwa na shamba la mizabibu jirani na jumba la kifalme la Ahabu mfalme wa Samaria.
2 Ahabu akamwambia Nabothi, akisema, “Nipe shamba lako, ili nilifanye kuwa bustani ya mboga, kwa sababu iko karibu na nyumba yangu. Badala yake nitakupa shamba zuri la mizabibu, au, kama ukipenda nitakulipa thamani yake kwa fedha.”
Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilitumie kwa bustani ya mboga, kwa kuwa liko karibu na jumba langu la kifalme. Badala yake, nitakupa shamba jingine la mizabibu zuri zaidi au, kama utapenda, nitakulipa kiasi chochote unachoona ni thamani yake.”
3 Nabothi akamjibu Ahabu, “BWANA na alizuie hilo nisije nikatoa urithi wa mababu zangu kwako.”
Lakini Nabothi akamjibu, “Bwana na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.”
4 Ahabu akaingia kwenye ikulu yake akiwa mchovu na mwenye hasira kwa sababu ya jibu ambalo Nabothi Myezreeli alimpa aliposema, “Sitakupa urithi wa mababu zangu.” Akalala kitandani kwake, akiwa amegeuza uso wake upande ule, na akagoma kula chakula chochote.
Basi Ahabu akaenda nyumbani, mwenye huzuni na hasira kwa sababu ya yale ambayo Nabothi, Myezreeli, alikuwa amesema, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula.
5 Yezebeli mke wake akaiingia kwake, akamwambia “Kwa nini moyo wako una huzuni, kiasi kwamba hutaki kula?”
Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?”
6 Naye akamjibu,” Niliongea na Nabothi Myezreeli nikamwambia, 'Nipe shamba lako nami nitakupa pesa, au kama inakupendeza, nitakupa shamba jingine ili liwe lako.' Naye akanijibu, 'Sitakupa shamba langu.'”
Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi, Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au kama ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’”
7 Naye Yezebeli mkewe akamjibu, “Je, wewe si mtawala wa ufalme wa Israeli? Inuka ule; na moyo wako uwe na amani. Nitalichukua hilo shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli kwa ajili yako.
Yezebeli mke wake akasema, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme katika Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupatia shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”
8 Kwa hiyo Yezebeli akaandika barua kwa jina la Ahabu, akaitia muhuri wake, akazituma kwa wazee na kwa watu tajiri alioketi nao kwenye vikao, na ambao pia waliishi karibu na Nabothi.
Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu akaweka muhuri wake juu ya hizo barua, akazipeleka kwa wazee na kwa watu wenye cheo walioishi katika mji pamoja na Nabothi.
9 Katika ile barua aliyoandika, ilisema hivi, “Pigeni mbiu ya kufunga mkamkalishe Nabothi juu mbele ya watu.
Katika barua hizo aliandika: “Tangazeni siku ya watu kufunga na mkamketishe Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu.
10 Pia mwaweke watu wawili wasiokuwa waaminifu pamoja naye na wale watu watoe ushahidi kinyume naye, waseme, 'Ulimlaani Mungu na mfalme.”Halafu mchukueni nje mkampige kwa mawe mpaka afe.
Lakini waketisheni watu wawili wabaya kabisa mkabala naye, nao washuhudie kuwa yeye amemlaani Mungu na mfalme. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.”
11 Kwa hiyo watu wa mji wake, wazee na watu tajiri waishio kwenye huo mji, wakafanya kama Yezebeli alivyowaeleza, kama ilivyoandikwa kwenye zile baraua ambazo alikuwa amewatumia.
Hivyo wazee na watu wenye cheo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua aliyowaandikia.
12 Wakapiga mbiu ya kufunga wakamkalisha Nabothi juu mbele ya watu.
Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu.
13 Na wale watu wawili wasiokuwa waaminifu wakaja wakakaa mbele ya Nabothi; nao wakatoa ushuhuda wao dhidi ya Nabothi kuwa amemlaani Mungu na mfalme.” Kisha wakamchukua nje ya mji wakampiga kwa mawe mpaka akafa.
Kisha watu wawili wabaya kabisa wakaja wakaketi mkabala naye, nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa.
14 Kisha wazee wakatuma neno kwa Yezebeli, wakisema, “Nabothi ameshapigwa mawe na amekufa.”
Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.”
15 Naye Yezebeli aliposikia kuwa Nabothi ameshapigwa mawe na alikuwa amekufa, akamwabia Ahabu, “Inuka na ukamiliki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia, kwa sababu Nabothi hayuko hai, bali amekufa.”
Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na uchukue lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.”
16 Ahabu aliposikia kuwa Nabothi amekufa, akainuka ili aende kwenye lile shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli na kulimiliki.
Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka na kushuka ili kulichukua shamba la mizabibu la Nabothi.
17 Ndipo neno la BWANA likamjia Eliya Mtishibi, likisema,
Kisha neno la Bwana likamjia Eliya, Mtishbi:
18 “Inuka uende ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye anaishi Samaria. Yumo kwenye shamba la Nabothi, ambako ameenda kuchukua umiliki wa shamba hilo.
“Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambapo amekwenda alimiliki.
19 Ukaongee naye umwambie kwamba BWANA anasema, 'Je, umeua na kujimilikisha?' na utamwambia kwamba BWANA anasema, 'Mahali pale ambapo mbwa wameramba damu ya Nabothi, ndipo mbwa watakaporamba damu yako, ndiyo, damu yako.'”
Umwambie, ‘Hivi ndivyo Bwana asemavyo: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Mahali ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako, naam, yako wewe!’”
20 Ahabu akamwambia Eliya, “Je, umenipatia, adui yangu?” Eliya akamjibu, “Nimekupata wewe kwa sababu, umejiuza mwenyewe kufanya yaliyo maovu mbele ya macho ya BWANA.
Ahabu akamwambia Eliya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!” Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kufanya uovu mbele ya macho ya Bwana.
21 BWANA anakwambia hivi: 'Tazama, Nitaleta janga kwako na litakuangamiza kabisa na kufutilia mbali kila mtoto mume na mtumwa na mtu huru katika Israeli.
‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kutoka kwa Ahabu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, wa mtumwa au wa mtu huru.
22 Nitaifanya familia yako kama familia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama familia ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhabisha na umewasababisha Israeli kufanya dhambi.
Nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ile ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kuwa umesababisha Israeli kutenda dhambi.’
23 Pia BWANA ameongea kuhusu Yezebeli, amesema, “mbwa watamla Yezebeli pembeni mwa ukuta wa Yezreeli.'
“Pia kwa habari ya Yezebeli Bwana anasema, ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’
24 Yeyote ambaye ni mtu wa familia ya Ahabu ambaye atafia mjini - mbwa watamla. Na yeyote ambaye atafia shambani - ataliwa na ndege wa angani.”
“Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.”
25 Hapakuwepo na mtu kama Ahabu, ambaye alijiuza mwenyewe kufanya maovu mbele ya macho ya BWANA, ambaye mke wake Yezebeli alimchochea kufanya dhambi.
(Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni mwa Bwana, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe.
26 Ahabu alifanya matendo yachukizayo kwa ajili ya sanamu alizofanya, kama vile yale yote ambayo Waamori walifanya, BWANA akawafukuza mbele ya watu wa Israeli.
Alitenda kwa uovu sana katika kuabudu sanamu, kama wale Waamori ambao Bwana aliowafukuza mbele ya Israeli.)
27 Ahabu aliposikis maneno haya, Akachana mavazi yake na akavaa magunia kwenye mwili wake na akfaunga, na akalala kwenye magunia na akahuzunika sana.
Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu.
28 Kisha neno la BWANA likamjia Eliya Mtishibi likisema,
Ndipo neno la Bwana lilipomjia Eliya Mtishbi kusema,
29 “Je, unamwona jinsi Ahabu anavyojinyenyekeza mbele yangu? Kwa sababu anajinyeyenyekeza mwenyewe mbele yangu, Sitaleta lile janga katika siku zake; Ni katika siku za mwanae, nitakpolileta hilo janga katika familia yake.”
“Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”

< 1 Wafalme 21 >