< 1 Wafalme 18 >
1 Kwa hiyo baada ya siku nyingi neno la BWANA likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu wa ukame, likisema, “Nenda ukajionyeshe mwenyewe kwa Ahabu nami nitainyeshea ardhi mvua.”
2 Eliya akaenda kujionyesha mwenyewe kwa Ahabu; sasa njaa ilikuwa kali sana kule Samaria.
3 Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa mkuu wa ikulu. Obadia alimheshimu sana BWANA,
4 kwa kuwa wakati Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa BWANA, Obadia alichukua manabii mia akawaficha katika makundi ya hamsini hamsini katika pango na akawalisha kwa mikate na maji.
5 Ahabu akamwambia Obadia, “Pita katika nchi yote na katika chemichemi zote za maji na vijito. Yamkini tunaweza kupata maji na nyasi ili tuwaokoa hawa farasi na nyumbu, ili tusiwakose wanyama wote.”
6 Kwa hiyo wakaigawa nchi kati yao ili wapite kati yake wakitafuta maji. Ahabu akaenda njia yake mwenyewe na Obadia naye akaenda njia yake.
7 Wakati Obadia akiwa njiani, akakutana na Eliya pasipo kutegemea. Obadia akamtambua na akalala kifudifudi chini. Akamwambia, “Ndiye wewe, bwana wangu Eliya?”
8 Naye Eliya akamjibu, Ni mimi. Nenda umwambie bwana wako, 'Tazama, Eliya yuko hapa.'”
9 Obadia akamjibu. “Nimekoseaje, kwamba umtoe mtumishi wako katika mkono wa Ahabu ili aniue?
10 Kama BWANA Mungu wako aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambapo bwana wangu hajatuma watu kukutafuta. Kila taifa au ufalme unaposema, “Eliya hayuko hapa,' Ahabu hufanya waape ni kweli hawajakuona.
11 Na sasa wewe unasema, 'Nenda, ukamwambie bwana wako kwamba Eliya yuko hapa.'
12 Mara tu baada ya kukuacha Roho wa BWANA atakuchukua na kukupeleka mahali ambapo sitapajua. Kisha nikienda na kumwambia Ahabu, na asipokuona, ataniua. Bado, mimi, mtumishi wako, nimekuwa nikimwabudu BWANA kutoka ujana wangu.
13 Je, haujaambiwa, bwana wangu, nilichokifanya wakati Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA, jinsi nilivyowaficha wale manabii mia moja wa BWANA katika makundi ya hamsini kwenye pango na kuwalisha kwa mikate na maji?
14 Na sasa unasema, 'Nenda umwambie bwana wako kwamba Eliya yuko hapa,' kwa hiyo ataniua.”
15 Ndipo Eliya alipomjibu, “Kama vile BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye mimi ninasimama, Kwa hakika nitajionyeshakwa Ahabu leo.”
16 Kwa hiyo Obadia akaenda kukutana na Ahabu, nakumwambia kile Eliya alichokuwa amemwambia. Ndipo mfalme alipoenda kukutana na Eliya.
17 Ahabu alipomwona Eliya, akamwambia, “Je, ni wewe? Wewe mtabishaji wa Israeli!”
18 Eliya akamwambia, “Mimi sijaitabisha Israeli, Lakiini wewe na familia ya baba yako ndio watabishaji kwa kuziacha amri za BWANA na kufuata sanamu za Baali.
19 Kwa hiyo sasa, Tuma neno na unikusanyie Israeli yote katika mlima Kameli, pamoja na manabii 450 wa Baali na wale manabii 400 wa Ashera wanaokula kwenye meza ya Yezebeli.”
20 Kwa hiyo Ahabu akatuma neno kwa watu wote wa Israeli na akawakusanya manabii wote kwenye mlima Kameli.
21 Eliya akaja karibu na watu wote akasema, “Mtaendelea kubadilisha mawazo yenu mpaka lini? Kama BWANA ni Mungu, mfuateni yeye, Lakini kama Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye,” Lakini watu hawakumjibu neno.
22 Kisha Eliya akawaambia wale watu, “Mimi, pekee yangu, ndiye niliyebaki kuwa nabii wa BWANA, lakini manabii wa Baali wako 450.
23 Hebu tutoleeni ng'ombe wawili. Nao wajichagulie ng'ombe mmoja na wamchinje na kumkatakata katika vipnde, na wamweke kwenye kuni, na wasitie moto chini yake. Nami nitamwandaa yule wa pili na kumweke juu ya kuni nami sitatia moto chini yake.
24 Kisha mtaliita jina la mungu wenu, nami nitaliita jina la BWANA, na Mungu atakayejibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Watu wote wakajibu na kusema, “Hilo ni jambo jema.”
25 Kwa Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni ng'ombe mmoja kwa ajili yenu na mwe wa kwanza kumwamdaa, kwa kuwa ninyi ni wengi, Kisha liiteni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
26 Nao wakamchukua yule ng'ombe waliokuwa wamepewa na wakamwandaa, na ndipo walipoliita jina la Baali kuanzia asubuhi hadi adhuhuri, wakisema, “Baali, tusikie.” Lakini hapakuwepo na Sauti, na wala hakuna aliyejibu. Wakachezacheza kuizunguka madhabahu waliyotengeneza.
27 Ilipofika adhuhuri Eliya akawakejeli akisema, “Mwiteni kwa nguvu! Huyo ni mungu! labda anawaza kitu, au amepumzika, au yuko safarini, au pengine amelala sharti aamshwe.”
28 Kwa hiyo wakamwita kwa nguvu, wakajikatakata kama kawaida yao ilivyokuwa, kwa upanga na nyembe, mpaka damu ikawachuruzika.
29 Ikawa wakati wa adhuhuri ulipopita, na bado walikuwa wakiendelea kutabiri mpaka wakati wa jioni wa kutoa dhabihu, lakini hapakuwepo na sauti wala mtu wa kuwajibu; wala hapakuwepo na yeyote wa kujibu wala wa kuangalia.
30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Nisogeleeni,” na watu wote wakamsogelea. Naye akatengeneza ile madhabahu ya BWANA ambayo ilikuwa imeharibika.
31 Eliya akachukua mawe kumi na mawili, kila jiwe moja liliwakilisha kabila moja la wana wa Yakobo - ni kupitia Yakobo kwamba neno la BWANA lilikuja, likisema, “Jina lako litakuwa Israel.”
32 Kwa kutumia hayo mawe aliijenga ile madhabahu kwa jina la BWANA na akachimba mfereji kuizunguka ile madhabahu kubwa kiasi cha kubeba lita kumi na tano za maji.
33 Kisha akaweka kuni kwa ajili ya moto na akamkatakata yule ng'ombe katika vipande vipande na akaweka vile vipande juu ya kuni. Na akasema, “Vijazeni maji hivyo vyombo na yamwageni kwenye hiyo sadaka ya kueketezwa na juu ya hizo kuni.”
34 Akasema tena fanyeni hivyo mara ya pili,” nao wakafanya kwa mara ya pili. kisha akasema, “Fanyeni mara ya tatu,” nao wakafanya kwa mara ya tatu.
35 Maji yakaizunguka ile madhabahu na kuujaza ule mfereji.
36 Ikawa wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea na akasema, “BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu wa Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako, na kwamba nimeyafanya mambo haya yote kwa jina lako.
37 Nisikie, BWANA, nisike, ili hawa watu wajue kuwa wewe, BWANA, ndiye Mungu, na kwamba umeirudisha mioyo yao kwako tena.”
38 Ndipo moto wa BWANA ukashuka ukairamba ile sadaka, pamoja na zile kuni, mawe na mavumbi, na kuyaramba yale maji yaliyokuwa kwenye ule mfereji.
39 watu wote walipoona haya, wakalala kifudifudi chini wakasema, “BWANA, ndiye Mungu! BWANA ndiye Mungu!
40 Kwa hiyo Eliya akawaambia, “Wakamateni manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja wao atoroke.” Kwa hiyo wakawakamata, na Eliya akawaleta manabii wa Baali chini kwenye kijito cha Kishoni na akawaua huko.
41 Eliya akamwambia Ahabu, “Inuka, ule na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.”
42 Kwa hiyo Ahabu akaenda akala na knywa. Kisha Eliya akaenda juu ya mlima Kameli, akasudu chini na akaweka uso wake katikati ya magoti.
43 Akamwambia mtumishi wake, “Nenda sasa, utazame upande wa bahari.” mtumishi wake akaenda na akasema, “Hakuna kitu,” Eliya akamwambia, “Nenda tena, mpaka mara saba.”
44 Ile mara ya saba mtumishi wake akasema, “Tazama, kuna wingu linapanda kutoka baharini, ni dogo kama mkono wa mtu.” Eliya akamjibu, Nenda ukamwambie Ahabu, 'Andaa gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.'”
45 Ikatokea baada ya muda mfupi mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, na kulikuwa na mvua kubwa. Ahabu akapanda gari akaenda zake Yezreeli,
46 lakini mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Eliya. Akalikaza vazi lake kwa mshipi wake na akakimbia mbele ya Ahabu kwenye lango la Yezreeli.