< 1 Wakorintho 6 >

1 Mmoja wenu anapokuwa na tatizo na mwenzake, anathubutu kwenda kwa mahakama ya wasio haki kuliko mbele ya waumini?
Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu muumini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu?
2 Hamjui kuwa waumini watauhukumu ulimwengu? Na kama mtauhukumu ulimwengu, hamuwezi kuamua mambo yasiyo muhimu?
Je, hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo?
3 Hamjui kuwa tutawahukumu malaika? Kwa kiasi gani zaidi, tunaweza kuamua mambo ya maisha haya?
Je, hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika?
4 Kama tunaweza kuhukumu mambo ya maisha haya, kwa nini mnathubutu kupeleka mashitaka mbele ya wasiosimama kanisani?
Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu ambao hata hawalijali kanisa?
5 Nasema haya kwa aibu yenu. Hakuna mwenye busara miongoni mwenu wa kutosha kuweka mambo sawa kati ya ndugu na ndugu?
Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini?
6 Lakini kama ilivyo sasa, mwamini mmoja huenda mahakamani dhidi ya muumini mwingine, na mashitaka hayo huwekwa mbele ya hakimu asiyeamini!
Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini.
7 Ukweli ni kwamba kuna matatizo katikati ya Wakristo yaliyoleta tayari usumbufu kwenu. Kwanini msiteseke kwa mabaya? Kwanini mnakubali kudanganywa?
Kwa kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa! Haingekuwa bora zaidi kwenu kunyang'anywa mali yenu?
8 Lakini mmetenda uovu na kudanganya wengine, na hao ni kaka na dada zenu!
Lakini, badala yake, ninyi ndio mnaodhulumu na kunyang'anya; tena, hayo mnawafanyia ndugu zenu!
9 Hamjui kwamba wasio haki hawataurithi ufalme wa Mungu? Msiamini uongo. Waasherati, waabudu sanamu, wazinzi, wafiraji, walawiti,
Au je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi Utawala wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti,
10 wevi, wachoyo, walevi, wanyang'anyi, watukanaji-hakuna miongoni mwao atakayeurithi ufalme wa Mungu.
wevi, wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyang'anyi, hao wote hawatashiriki Utawala wa Mungu.
11 Na hao walikuwa baadhi yao ni ninyi. Lakini mmekwisha kutakaswa, lakini mmekwisha kuoshwa, lakini mmekwisha kutengwa kwa Mungu, lakini mmefanywa haki mbele za Mungu katika jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
Baadhi yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kupatanishwa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
12 “Vitu vyote ni halali kwangu”, lakini si kila kitu kina faida. “Vitu vyote ni halali kwangu,” lakini sitatawaliwa na kimoja cha hivyo.
Mtu anaweza kusema: “Kwangu mimi kila kitu ni halali.” Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote.
13 “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula,” lakini Mungu atavitowesha vyote. Mwili haujaumbwa kwa ajili ya ukahaba, badala yake, mwili ni kwa ajili ya Bwana, na Bwana atauhudumia mwili.
Unaweza kusema: “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula.” Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili.
14 Mungu alimfufua Bwana na sisi pia atatufufua kwa nguvu zake.
Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake.
15 Hamjui kwamba miili yenu ina muunganiko na Kristo? Mwawezaje kuvitoa viungo vya Kristo na kwenda kuviunganisha na kahaba? Haiwezekani!
Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo!
16 Hamjui kwamba anayeungana na kahaba amekuwa mwili mmoja naye? Kama andiko lisemavyo, “Wawili watakuwa mwili mmoja.”
Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye—kama ilivyoandikwa: “Nao wawili watakuwa mwili mmoja.”
17 Lakini anayeungana na Bwana anakuwa roho moja pamoja naye.
Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye.
18 Ikimbieni zinaa! “Kila dhambi aifanyayo mtu ni nje na mwili wake. Lakini zinaa, mtu hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
19 Hamjui kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu, akaaye ndani yenu, yule ambaye mlipewa kutoka kwa Mungu? Hamjui kwamba si ninyi wenyewe?
Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Ninyi basi, si mali yenu wenyewe.
20 Kwamba mlinunuliwa kwa thamani. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu kwa miili yenu.
Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

< 1 Wakorintho 6 >