< 1 Wakorintho 6 >
1 Mmoja wenu anapokuwa na tatizo na mwenzake, anathubutu kwenda kwa mahakama ya wasio haki kuliko mbele ya waumini?
Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu?
2 Hamjui kuwa waumini watauhukumu ulimwengu? Na kama mtauhukumu ulimwengu, hamuwezi kuamua mambo yasiyo muhimu?
Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo?
3 Hamjui kuwa tutawahukumu malaika? Kwa kiasi gani zaidi, tunaweza kuamua mambo ya maisha haya?
Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya?
4 Kama tunaweza kuhukumu mambo ya maisha haya, kwa nini mnathubutu kupeleka mashitaka mbele ya wasiosimama kanisani?
Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa.
5 Nasema haya kwa aibu yenu. Hakuna mwenye busara miongoni mwenu wa kutosha kuweka mambo sawa kati ya ndugu na ndugu?
Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio?
6 Lakini kama ilivyo sasa, mwamini mmoja huenda mahakamani dhidi ya muumini mwingine, na mashitaka hayo huwekwa mbele ya hakimu asiyeamini!
Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!
7 Ukweli ni kwamba kuna matatizo katikati ya Wakristo yaliyoleta tayari usumbufu kwenu. Kwanini msiteseke kwa mabaya? Kwanini mnakubali kudanganywa?
Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa?
8 Lakini mmetenda uovu na kudanganya wengine, na hao ni kaka na dada zenu!
Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.
9 Hamjui kwamba wasio haki hawataurithi ufalme wa Mungu? Msiamini uongo. Waasherati, waabudu sanamu, wazinzi, wafiraji, walawiti,
Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti,
10 wevi, wachoyo, walevi, wanyang'anyi, watukanaji-hakuna miongoni mwao atakayeurithi ufalme wa Mungu.
wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu.
11 Na hao walikuwa baadhi yao ni ninyi. Lakini mmekwisha kutakaswa, lakini mmekwisha kuoshwa, lakini mmekwisha kutengwa kwa Mungu, lakini mmefanywa haki mbele za Mungu katika jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.
12 “Vitu vyote ni halali kwangu”, lakini si kila kitu kina faida. “Vitu vyote ni halali kwangu,” lakini sitatawaliwa na kimoja cha hivyo.
“Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote.
13 “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula,” lakini Mungu atavitowesha vyote. Mwili haujaumbwa kwa ajili ya ukahaba, badala yake, mwili ni kwa ajili ya Bwana, na Bwana atauhudumia mwili.
“Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana na Bwana kwa ajili ya mwili.
14 Mungu alimfufua Bwana na sisi pia atatufufua kwa nguvu zake.
Naye Mungu aliyemfufua Bwana kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake.
15 Hamjui kwamba miili yenu ina muunganiko na Kristo? Mwawezaje kuvitoa viungo vya Kristo na kwenda kuviunganisha na kahaba? Haiwezekani!
Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Kristo mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Kristo na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha!
16 Hamjui kwamba anayeungana na kahaba amekuwa mwili mmoja naye? Kama andiko lisemavyo, “Wawili watakuwa mwili mmoja.”
Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.”
17 Lakini anayeungana na Bwana anakuwa roho moja pamoja naye.
Lakini mtu aliyeungwa na Bwana anakuwa roho moja naye.
18 Ikimbieni zinaa! “Kila dhambi aifanyayo mtu ni nje na mwili wake. Lakini zinaa, mtu hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe.
19 Hamjui kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu, akaaye ndani yenu, yule ambaye mlipewa kutoka kwa Mungu? Hamjui kwamba si ninyi wenyewe?
Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe,
20 Kwamba mlinunuliwa kwa thamani. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu kwa miili yenu.
kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.