< 1 Wakorintho 5 >
1 Tumesikia taarifa kuwa kuna zinaa miongoni mwenu, aina ya zinaa ambayo haipo hata katikati ya watu wa Mataifa. Tuna taarifa kwamba mmoja wenu analala na mke wa baba yake.
2 Nanyi mwajisifu! Badala ya kuhuzunika? Yule aliyefanya hivyo anapaswa kuondolewa miongoni mwenu.
3 Ingawa sipo pamoja nanyi kimwili lakini nipo nanyi kiroho, nimekwisha mhukumu yeye aliyefanya hivi, kama vile nilikuwepo.
4 Mnapokutanika pamoja katika jina la Bwana wetu Yesu, na roho yangu ipo pale kama kwa nguvu za Bwana wetu Yesu, nimekwisha mhukumu mtu huyu.
5 Nimekwisha kumkabidhi mtu huyu kwa Shetani ili kwamba mwili wake uharibiwe, ili roho yake iweze kuokolewa katika siku ya Bwana.
6 Majivuno yenu si kitu kizuri. Hamjui chachu kidogo huharibu donge zima?
7 Jisafisheni ninyi wenyewe chachu ya kale, ili kwamba muwe donge jipya, ili kwamba mwe mkate usiochachuliwa. Kwa kuwa, Kristo, Mwana Kondoo wetu wa pasaka amekwisha kuchinjwa.
8 Kwa hiyo tusherekee karamu si kwa chachu ya kale, chachu ya tabia mbaya na uovu. Badala yake, tusherekee na mkate usiotiwa chachu wa unyenyekevu na kweli.
9 Niliandika katika barua yangu kuwa msichangamane na wazinzi.
10 Sina maana wazinzi wa dunia hii, au na wenye tamaa au wanyang'anyi au waabudu sanamu kwa kukaa mbali nao, basi ingewapasa mtoke duniani.
11 Lakini sasa nawaandikia kutojichanganya na yeyote anayeitwa kaka au dada katika Kristo, lakini anaishi katika uzinzi au ambaye ni mwenye kutamani, au mnyang'anyi, au mwabudu sanamu, au mtukanaji au mlevi. Wala msile naye mtu wa namna ile.
12 Kwa hiyo nitajihusishaje kuwahukumu walio nje ya Kanisa? Badala yake, ninyi hamkuwahukumu walio ndani ya kanisa?
13 Lakini Mungu anawahukumu walio nje. “Mwondoeni mtu mwovu miongoni mwenu”