< 1 Wakorintho 2 >
1 Nilipokuja kwenu kaka na dada zangu, sikuja kwa maneno ya ushawishi na hekima kama nilivyohubiri kweli iliyofichika kuhusu Mungu.
2 Niliamua kutojua chochote nilipokuwa miongoni mwenu isipokuwa Yesu Kristo, na yeye aliyesulubiwa.
3 Na nilikuwa nanyi katika udhaifu, na katika hofu, na katika kutetemeka sana.
4 Na ujumbe wangu na kuhubiri kwangu hakukuwa katika maneno ya ushawishi na hekima. Badala yake, yalikuwa katika kumdhihirisha Roho na ya nguvu,
5 ili kwamba imani yenu isiwe katika hekima ya wanadadamu, bali katika nguvu ya Mungu.
6 Sasa tunaizungumza hekima miongoni mwa watu wazima, lakini si hekima ya dunia hii, au ya watawala wa nyakati hizi, ambao wanaopita. (aiōn )
7 Badala yake, tunaizungumza hekima ya Mungu katika ukweli uliofichika, hekima iliyofichika ambayo Mungu aliichagua kabla ya nyakati za utukufu wetu. (aiōn )
8 Hakuna yeyote wa watawala wa nyakati hizi aliyeijua hekima hii, Kama wangeifahamu katika nyakati zile, wasingelimsulubisha Bwana wa utukufu. (aiōn )
9 Lakini kama ilivyoandikwa, “Mambo mbayo hakuna jicho limeyaona, hakuna sikio lililoyasikia, mawazo hayakufikiri, mambo ambayo Mungu ameyaandaa kwa ajili ya wale wampendao yeye.”
10 Haya ni mambo ambayo Mungu ameyafunua kwetu kupitia Roho, Kwa kuwa Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani ya Mungu.
11 Kwa kuwa nani afahamuye mawazo ya mtu, isipokuwa roho ya mtu ndani yake? Hivyo pia, hakuna ajuaye mambo ya ndani ya Mungu, isipokuwa Roho wa Mungu.
12 Lakini hatukupokea roho ya dunia, lakini Roho ambaye anatoka kwa Mungu, ili kwamba tuweze kujua kwa uhuru mambo tuliyopewa na Mungu.
13 Tunasema mambo haya kwa maneno, ambayo hekima ya mtu haiwezi kufundisha, lakini ambayo Roho hutufundisha. Roho hutafasiri maneno ya kiroho kwa hekima ya kiroho.
14 Mtu asiye wa kiroho hapokei mambo ambayo ni ya Roho wa Mungu, kwa kuwa hayo ni upuuzi kwake. Hawezi kuyajua kwa sababu yanatambuliwa kiroho.
15 Kwa yule wa kiroho huhukumu mambo yote. Lakini huhukumiwa na wengine.
16 “Ni nani anaweza kuyajua mawazo ya Bwana, ambaye anaweza kumfundisha yeye?” Lakini tuna mawazo ya Kristo.