< 1 Wakorintho 15 >

1 Sasa ninawakumbusha, akina kaka na akina dada, juu ya injili niliyowahubiria, ambayo mliipokea na kusimama kwayo.
Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama.
2 Ni katika injili hii mmeokolewa, kama mkilishika imara neno nililowahubiri ninyi, isipokuwa mliamini bure.
Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.
3 Kama kwanza nilivyo ipokea kwa umuhimu niliileta kwenu kama ilivyo: kwamba kutokana na maandiko, Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu,
Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemavyo Maandiko,
4 kutokana na maandiko alizikwa, na kwamba alifufuka siku ya tatu.
ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama yasemavyo Maandiko,
5 Na kwamba alimtokea Kefa, kisha kwa wale kumi na wawili.
na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili.
6 Kisha aliwatokea kwa wakati mmoja akina kaka na akina dada zaidi ya mia tano. Wengi wao bado wako hai, lakini baadhi yao wamelala usingizi.
Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala.
7 Kisha alimtokea Yakobo, kisha mitume wote.
Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote.
8 Mwisho wa yote, alinitokea mimi, kama vile kwa mtoto aliye zaliwa katika wakati usio sahihi.
Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.
9 Kwa kuwa mimi ni mdogo kati ya mitume. Sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu.
Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu.
10 Lakini kwa neema ya Mungu nipo kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Badala yake, nilifanya bidii kuliko wote. Lakini haikuwa mimi, bali neema ya Mungu iliyo ndani yangu.
Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.
11 Kwa hiyo kama ni mimi au wao, tuna hubiri hivyo na tunaamini hivyo.
Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.
12 Sasa kama Kristo alihubiriwa kama aliyefufuka kwa wafu, iweje baadhi yenu mseme hakuna ufufuo wa wafu?
Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu?
13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo pia hakufufuka.
Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuliwa.
14 Na kama Kristo hakufufuka, hivyo mahubiri yetu ni bure, na imani yenu ni bure.
Tena ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili.
15 Na tumepatikana kuwa mashahidi wa uongo kumuhusu Mungu, kwa sababu tulimshushuhudia Mungu kinyume, kusema alimfufua Kristo, wakati hakumfufua.
Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Kristo kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi.
16 Kama ikiwa wafu hawafufuliwi, Yesu pia hakufufuliwa.
Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Kristo hajafufuka.
17 Na kama Kristo hakufufuliwa, imani yenu ni bure na bado mko kwenye dhambi zenu.
Tena kama Kristo hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu.
18 Hivyo hata wale waliokufa katika Kristo pia wameangamia.
Hivyo basi, wote waliolala katika Kristo wamepotea.
19 Ikiwa kwa maisha haya peke yake tunaujasiri kwa wakati ujao ndani ya Kristo, watu wote, sisi niwakuhurumiwa zaidi ya watu wote.
Ikiwa tumaini letu ndani ya Kristo ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote.
20 Lakini sasa Kristo amefufuka kutoka kwa wafu, matunda ya kwanza ya wale waliokufa.
Lakini kweli Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala.
21 Kwa kuwa kifo kilikuja kupitia mwanadamu, pia kupitia mwanadamu ufufuo wa wafu.
Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja.
22 Kwa kuwa kama katika Adam wote wanakufa, hivyo pia katika Kristo wote watafanywa hai.
Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai.
23 Lakini kila moja katika mpango wake: Kristo, matunda ya kwanza, na kisha wale walio wa Kristo watafanywa hai wakati wa kuja kwake.
Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja.
24 Ndipo utakuwa mwisho, pale Kristo atakapo kabidhi ufalme kwa Mungu Baba. Hii ni pale atakapo komesha utawala wote na mamlaka yote na nguvu.
Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu.
25 Kwa kuwa lazima atawale mpaka atakapoweka maadui zake wote chini ya nyayo zake.
Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake.
26 Adui wa mwisho kuharibiwa ni kifo.
Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti.
27 Kwa kuwa “ameweka kila kitu chini ya nyayo zake.” Lakini inaposema “ameweka kila kitu,” ni wazi kwamba hii haihusishi wale walioweka kila kitu chini yake mwenyewe.
Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa.
28 Wakati vitu vyote vimewekwa chini yake, kisha Mwana mwenyewe atawekwa chini kwake Yeye ambaye aliviweka vitu vyote chini yake. Hii itatokea ili kwamba Mungu Baba awe yote katika vyote.
Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.
29 Au pia watafanya nini wale waliobatizwa kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kabisa, kwa nini tena wanabatizwa kwa ajili yao?
Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao?
30 Na kwa nini tuko katika hatari kila saa?
Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa?
31 Kaka na dada zangu, kupitia kujisifu kwangu katika ninyi, ambayo ninayo katika Kristo Yesu Bwana wetu, natangaza hivi: nakufa kila siku.
Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku.
32 Inanifaidia nini, katika mtazamo wa wanadamu, kama nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, kama wafu hawafufuliwi? “Acha basi tule na kunywa, kwa kuwa kesho tunakufa.”
Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa.”
33 Msidanganywe: “Makundi mabaya huharibu tabia njema.
Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”
34 “Muwe na kiasi! muishi katika haki! msiendelee kutenda dhambi. Kwa kuwa baadhi yenu hamna maarifa ya Mungu. Nasema hivi kwa aibu yenu.
Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.
35 Lakini mtu mwingine atasema, “Jinsi gani wafu wanafufuliwa? Nao watakuja na aina gani ya mwili?”
Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”
36 Wewe ni mjinga sana! Kile ulichopanda hakiwezi kuanza kukua isipokuwa kimekufa.
Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa.
37 Na kile unachopanda sio mwili ambao utakuwa, bali ni mbegu iliyochipua. Inaweza kuwa ngano au kitu kingine.
Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine.
38 Lakini Mungu ataipa mwili kama apendavyo, na katika kila mbengu mwili wake mwenyewe.
Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake.
39 Miili yote haifanani. Isipokuwa, kuna mwili mmoja wa wanadamu, na mwili mwingine wa wanyama, na wili mwingine wa ndege, na mwingine kwa ajili ya samaki.
Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti.
40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani. Lakini utukufu wa miili ya mbinguni ni aina moja na utukufu wa duniani ni mwingine.
Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na fahari wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine.
41 Kuna utukufu mmoja wa jua, na utukufu mwingine wa mwezi, na utukufu mwingine wa nyota. Kwa kuwa nyota moja inatofautiana na nyota nyingine katika utukufu.
Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.
42 Hivyo ndivyo ulivyo pia ufufuo wa wafu. Kinacho pandwa kinaharibika, na kinacho ota hakiharibiki.
Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika,
43 Kimepandwa katika matumizi ya kawaida, kinaoteshwa katika utukufu. Kimepandwa katika udhaifu, kinaoteshwa katika nguvu.
unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu,
44 Kimepandwa katika mwili wa asili, kinaoteshwa katika mwili wa kiroho. Kama kuna mwili wa asili, kuna mwili wa kiroho pia.
unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho. Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia.
45 Hivyo pia imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika roho inayo ishi.” Adamu wa mwisho alifanyika roho itoayo uhai.
Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima.
46 Lakini wa kiroho hakuja kwanza bali wa asili, na kisha wa kiroho.
Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho.
47 Mtu wa kwanza ni wa dunia, alitengenezwa kwa mavumbi. Mtu wa pili anatoka mbinguni.
Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni.
48 Kama vile yule aliyetengenezwa kwa mavumbi, hivyo pia wale waliotengenezwa kwa mavumbi. Kama vile mtu wa mbinguni alivyo, hivyo pia wale wa mbinguni.
Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni.
49 Kama ambavyo tumebeba mfano wa mtu wa mavumbi, tutabeba pia mfano wa mtu wa mbinguni.
Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.
50 Sasa nawaambia, kaka na dada zangu, kwamba mwili na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Wala wakuharibika kurithi wakutoharibika.
Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika.
51 Tazama! Nawaambia ninyi siri ya kweli: Hatutakufa wote, bali wote tutabadilishwa.
Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa
52 Tutabadilishwa katika wakati, katika kufumba na kufumbua kwa jicho, katika tarumbeta ya mwisho. Kwa kuwa tarumbeta italia, na wafu watafufuliwa na hali ya kutoharibika, na tutabadilishwa.
ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa.
53 Kwani huu wa kuharibika lazima uvae wa kutoharibika, na huu wa kufa lazima uvae wa kutokufa.
Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa.
54 Lakini wakati huu wa kuharibika ukivikwa wa kutokuharibika, na huu wa kufa ukivaa wa kutokufa, ndipo utakuja msemo ambao umeandikwa, “Kifo kimemezwa katika ushindi.”
Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”
55 “Kifo, ushindi wako uko wapi? Kifo, uko wapi uchungu wako?” (Hadēs g86)
“Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako? Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?” (Hadēs g86)
56 Uchungu wa kifo ni dhambi, na nguvu ya dhambi ni sheria.
Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria.
57 Lakini shukurani kwa Mungu, atupaye sisi ushindi kupitia Bwana wetu Yesu Kristo!
Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
58 Kwa hiyo, wapendwa kaka na dada zangu, iweni imara na msitikisike. Daima itendeni kazi ya Bwana, kwa sababu mnajua kuwa kazi yenu katika Bwana siyo bure.
Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

< 1 Wakorintho 15 >