< 1 Wakorintho 14 >

1 Utafuteni upendo na kutamani sana karama za rohoni, zaidi sana mpate kutoa unabii.
Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii.
2 Maana yeye anenaye kwa lugha hasemi na watu bali husema na Mungu. Maana hakuna aelewaye kwa sababu anena mambo yaliyofichika katika Roho.
Kwa maana mtu yeyote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa roho.
3 Lakini yeye atoaye unabii, asema na watu na kuwajenga, kuwatia moyo, na kuwafariji.
Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji.
4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, lakini yeye atoaye unabii hulijenga kanisa.
Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa.
5 Sasa natamani kwamba ninyi nyote mnene kwa lugha. Lakini zaidi ya hayo, natamani ya kwamba mtoe unabii. Yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha (labda awepo wa kutafasiri), ili kwamba kanisa lipate kujengwa.
Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili kanisa lipate kujengwa.
6 Lakini sasa, kaka na dada zangu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini ninyi? Siwezi, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya maarifa, au unabii, au kwa njia ya fundisho.
Sasa ndugu zangu, kama nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho?
7 Ikiwa vitu visivyo na uhai kama filimbi au kinubi visipotoa sauti zilizo na tofauti, itatambulikanaje ni chombo gani kinachezwa?
Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji?
8 Kwa maana ikiwa baragumu itatoa sauti isiyojulikana, ni jinsi gani mtu atatambua ya kuwa ni muda wa kujiandaa kwa vita?
Tena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita?
9 Vivyo hivyo na ninyi. Mkitoa kwa ulimi neno lisilo dhahiri, ni jinsi gani mtu ataelewa mnachosema? Mtakuwa mkiongea, na hakuna atakayewaelewa.
Vivyo hivyo na ninyi, kama mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu.
10 Hakuna shaka kwamba kuna lugha nyingi mbalimbali duniani, na hakuna hata moja isiyo na maana.
Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana.
11 Lakini ikiwa sijui maana ya lugha, nitakuwa mgeni kwake yeye anenaye, naye anenaye atakuwa mgeni kwangu.
Basi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu.
12 Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani sana kuona uthihirisho wa Roho, takeni kwamba mzidi sana kulijenga kanisa.
Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kulijenga kanisa.
13 Hivyo, yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kutafasiri.
Kwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena.
14 Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.
Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda.
15 Nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili zangu. Nitaimba kwa roho yangu, na nitaimba kwa akili zangu pia.
Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia.
16 Vinginevyo, ukimsifu Mungu kwa roho, yeye aliye mgeni ataitikaje “Amina” utoapo shukurani, akiwa hayajui usemayo?
Ikiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema?
17 Maana ni kweli wewe washukuru vema, lakini yule mwingine hajengwi.
Mnaweza kuwa mnatoa shukrani kweli, sawa, lakini huyo mtu mwingine hajengeki.
18 Namshukuru Mungu kwa kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote.
Namshukuru Mungu kwamba mimi nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote.
19 Lakini katika kanisa ni heri ninene maneno matano kwa ufahamu wangu ili nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.
Lakini ndani ya kanisa ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno 10,000 kwa lugha.
20 Kaka na dada zangu, msiwe watoto katika kufikiri kwenu. Badala yake, kuhusiana na uovu, iweni kama watoto wachanga. Lakini katika kufikiri kwenu mkawe watu wazima.
Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima.
21 Imeandikwa katika sheria, “Kwa watu wa lugha nyingine na kwa midomo ya wageni nitasema na watu hawa. Wala hata hivyo hawatanisikia,” asema Bwana.
Katika Sheria imeandikwa kwamba: “Kupitia kwa watu wenye lugha ngʼeni na kupitia midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, lakini hata hivyo hawatanisikiliza,” asema Bwana.
22 Hivyo, ndimi ni ishara, sio kwa walioamini, bali kwa wasioamini. Lakini kutoa unabii ni ishara, sio kwa wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio.
Basi kunena kwa lugha ni ishara, si kwa watu waaminio, bali kwa wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio.
23 Haya, ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja na wote wanene kwa lugha, na wageni na wasioamini wameingia, je hawawezi kusema kwamba mna wazimu?
Kwa hiyo kama kanisa lote likikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioelewa wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu?
24 Lakini ikiwa wote mnatoa unabii na asiyeamini au mgeni akaingia, atashawishiwa na yote asikiayo. Atahukumiwa na yote yasemwayo.
Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote,
25 Siri za moyo wake zingefunuliwa. Matokeo yake, angeanguka kifudifudi na kumwabudu Mungu. Angekiri ya kwamba Mungu yu kati yenu.
nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”
26 Nini kifuatacho basi, kaka na dada zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana Zaburi, mafundisho, mafunuo, lugha au tafsiri. Fanyeni kila kitu ili kwamba mlijenge kanisa.
Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa.
27 Kama yeyote ananena kwa lugha, wawepo wawili au watatu, na kila mmoja katika zamu. Na mtu lazima atafasiri kilichosemwa.
Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri.
28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafasiri, basi kila mmoja wao akae kimya ndani ya kanisa. Basi kila mmoja aongee peke yake na kwa Mungu.
Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.
29 Na manabii wawili au watatu wanene, na wengine wasikilize kwa kupambanua kilichosemwa.
Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo.
30 Lakini aliyeketi akifunuliwa jambo katika huduma, yule ambaye alikuwa ananena na anyamaze.
Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze.
31 Kwa kuwa kila mmoja wenu anaweza kutoa unabii mmoja baada ya mwingine ili kwamba kila mmoja aweze kujifunza na wote waweze kutiwa moyo.
Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo.
32 Kwa kuwa roho za manabii ziko chini ya uangalizi wa manabii.
Roho za manabii huwatii manabii.
33 Kwa kuwa Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani. Kama ilivyo katika makanisa yote ya waumini,
Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani. Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu,
34 imewapasa wanawake wakae kimya katika kanisa. Kwa kuwa hawaruhusiwi kuzungumza. Badala yake, wanapaswa kuwa katika unyenyekevu, kama pia sheria inavyosema.
wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo.
35 Kama kuna chochote wanatamani kujifunza, basi wawaulize waume zao nyumbani. Kwa kuwa ni aibu kwa mwanamke kuongea katika kanisa.
Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani.
36 Je neno la Mungu lilitoka kwenu? Je limewafikia ninyi tu?
Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia?
37 Kama mtu akijiona kuwa ni nabii au wa rohoni, inampasa ayatambue mambo ninayowaandikia ya kwamba ni maagizo ya Bwana.
Kama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana.
38 Lakini asipotambua haya, mwacheni asitambuliwe.
Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.
39 Hivyo basi, kaka na dada zangu, takeni sana kutoa unabii, na msimzuie mtu yeyote kunena kwa lugha.
Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha.
40 Lakini mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.
Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.

< 1 Wakorintho 14 >