< 1 Nyakati 28 >

1 Daudi akakusanya waamuzi wote wa Israeli Yerusalemu: waamuzi wa makabila, maafisa wa vitengo walio mtumikia mfalme katika kazi walizo pangiwa, wakuu wa maelfu na mamia, wasimamizi wa mali zote za mfalme na mwanae, na maafisa na wanaume wa mapambano, ukijumuisha wale wenye ujuzi sana.
Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani, maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali zote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na askari wote walio hodari.
2 Daudi mfalme akainuka kwa miguu yake na kusema, “Sikilizeni mimi, kaka zangu na watu wangu. Ilikuwa dhumuni langu kujenga hekalu kwa ajili ya sanduku la agano la Yahweh; stuli ya miguu kwa ajili ya Mungu wetu, na nimefanya maandalizi kuijenga.
Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la Bwana kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga.
3 Lakini Mungu akaniambia, 'Hautajenga hekalu kwa ajili ya jina la langu, kwasababu wewe ni mwanaume wa vita na umemwaga damu.'
Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umepigana vita na umemwaga damu.’
4 Bado Yahweh, Mungu wa Israeli, alinichagua kutoka katika familia ya baba yangu kuwa mfalme wa Israeli milele. Amechagua kabila la Yuda kama kiongozi. Katika kabila la Yuda, na nyumba ya baba yangu, kutoka kwa wana wa baba yangu, amenichagua kuwa mfalme wa Israeli.
“Hata hivyo, Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa yangu yote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote.
5 Kutoka kwa wana wengi ambao Yahweh amenipa, amemchagua Sulemani, mwanangu, kuketi katika kiti cha enzi cha ufalme wa Yahweh, juu ya Israeli.
Miongoni mwa wanangu wote, naye Bwana amenipa wengi, amemchagua Solomoni mwanangu ili kukikalia kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana juu ya Israeli.
6 Aliniambia, 'Sulemani mwanae atanijengea nyumba yangu na nyuani mwangu, kwa kuwa nimemchagua kuwa mwana wangu, nami nitakuwa baba yake.
Aliniambia, ‘Solomoni mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake.
7 Nitaimarisha ufalme wake, akidumu kutii sheria na amri zangu, kama ulivyo siku ya leo.'
Nitaufanya imara ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’
8 Kisha sasa, katika macho ya Waisraeli wote, ili kusanyiko la yahweh, na katika uwepo wa Mungu wetu, nyinyi nyote lazima mshike na kufanya amri zote za Yahweh Mungu wenu. Fanyeni hivi ili mmiliki nchi nzuri na kuacha urithi wa watoto wenu baada yenu milele.
“Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Bwana naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Bwana Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele.
9 Kwako wewe, Sulemani mwanangu, mtii Mungu wa baba yako, mtumikie kwa moyo wako wote na roho ya utayari. Fanya hivi kwasababu yahweh anachunguza mioyo yote na kufahamu amasa ya kila wazo la mtu. Ukimtafuta, ataonekana kwako, lakini ukimtelekeza, atakukataa milele.
“Nawe Solomoni mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Bwana huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali kama ukimwacha, yeye atakukataa milele.
10 Elewa kuwa Yahweh amekuchagua kujenga hekalu ili kama sehemu yake takatifu. Kuwa imara na ufanye.”
Angalia basi, kwa maana Bwana amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”
11 Kisha Daudi akamkabidhi Sulemani mwanae mipango ya baraza la hekalu, jengo la hekalu, vyumba vya hifadhi, vyumba vya juu, vyumba vya ndani, na chumba chenye mfuniko wa maombezi.
Ndipo Daudi akampa Solomoni mwanawe kielelezo kwa ajili ya ukumbi wa Hekalu, nyumba zake, vyumba vyake vya hazina, ghorofa zake, vyumba vyake vya ndani na mahali pa kufanyia upatanisho.
12 Alimpatia mipango aliyo chora ya nyuani kwa ajili ya nyumba ya Yahweh, vyumba vyote vilivyo zunguka, vyumba vya hifadhi katika nyumba ya Mungu, na hazina za vitu vya Yahweh.
Akampa vielelezo vya yote Roho alikuwa ameviweka moyoni mwake kwa ajili ya kumbi za Hekalu la Bwana na vyumba vyote vilivyolizunguka, kwa ajili ya hazina za Hekalu la Mungu na kwa hazina za vitu vilivyowekwa wakfu.
13 Alimpatia masharti kwa vitengo vya makuhani na Walawi, kwa majukumu walio pangiwa katika nyumba ya Yahweh, na kwa vyombo vyote vinavyo tumika katika nyumba ya Yahweh.
Mfalme pia akampa Solomoni maelekezo kwa ajili ya migawanyo ya huduma za makuhani na Walawi, pia kwa ajili ya kazi zote za huduma katika Hekalu la Bwana. Akampa pia maelezo kuhusu vifaa vyote vya kutumika katika huduma ya Hekalu.
14 Alimpa uzito wote wa vifaa vya dhahabu kwa kila huduma na vifaa vyote vya fedha, na vitu vyote kwa kila namna ya huduma.
Akamwagizia uzito wa dhahabu kwa ajili ya vitu vyote vya dhahabu vya kutumika katika huduma mbalimbali, uzito wa fedha kwa ajili ya vitu vyote vya fedha vya kutumika katika huduma mbalimbali.
15 Haya maelekezo yalitolewa kwa uzito, ukijumuisha maelekezo yote ya vinara vya taa vya dhahabu na taa za dhahabu, maelekezo kwa uzito kwa kila vinara vya taa, kwa vinara vya taa vya fedha, na maelekezo kwa matumizi sahihi ya vinara vya taa vyote.
Uzito wa dhahabu kwa ajili ya vinara vya dhahabu na taa zake, kukiwa na uzito kwa ajili ya kila kinara na taa zake, pamoja na uzito wa fedha kwa ajili ya kila kinara cha fedha na taa zake, kulingana na matumizi ya kila kinara;
16 Alitoa uzito wa dhahabu kwa meza za mkate wa uwepo, kwa kila meza, na uzito wa fedha kwa meza za fedha.
uzito wa dhahabu kwa ajili ya meza ya mikate iliyowekwa wakfu, uzito wa fedha kwa ajili ya meza ya fedha;
17 Alitoa uzito wa dhahabu safi kwa uma za nyama, bakuli, na vikombe. Alitoa uzito kwa kila bakuli ya dhahabu, na uzito kwa kila bakuli ya fedha.
uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya nyuma, mabakuli ya kunyunyizia na vikombe, masinia; uzito wa dhahabu kwa ajili ya kila bakuli la dhahabu; uzito wa fedha kwa ajili ya kila bakuli la fedha;
18 Alitoa uzito wa dhahabu ya kutakasika kwa madhabahu ya uvumba, na kwa dhahabu kwa ajili ya mchoro wa makerubi waliye tanda mabawa yao na kufunika sanduku la agano la Yahweh.
na uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya madhabahu ya kufukizia uvumba. Pia alimpa kielelezo kwa ajili ya gari, yaani, wale makerubi wa dhahabu waliokunjua mbawa zao na kuweka kivuli juu ya Sanduku la Agano la Bwana.
19 Daudi akasema, “Nimeeka haya katika maandishi kama Yahweh alivyo ni elekeza na kunipa kuelewa kuhusu mchoro.”
Daudi akasema, “Hii yote, ninayo kwa maandishi kutoka mkononi mwa Bwana ulio juu yangu, naye amenipa ufahamu kwa ajili ya habari zote za kielelezo hiki.”
20 Daudi akasema kwa Sulemani mwanae, “Kuwa hodari na mjasiri. Fanya kazi. Usiogope au kuwa na wasiwasi, kwa kuwa Yahweh Mungu, Mungu wangu, yupo nawe. Hatakuacha wala kukutelekeza mpaka kazi ya huduma ya hekalu la Yahweh imekamilika.
Daudi pia akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe hodari na moyo mkuu, ukafanye kazi hii. Usiogope wala usifadhaike, kwa maana Bwana aliye Mungu, Mungu wangu yu pamoja nawe. Hatakuacha wala hatakupungukia mpaka kazi hii yote kwa ajili ya utumishi wa Hekalu la Bwana itakapokamilika.
21 Ona, hivi ni vitengo vya makuhani na Walawi kwa huduma katika hekalu la Mungu. Watakuwa nawe, pamoja na wanaume walio tayari na wenye ujuzi, kukusaidia katika kazi na kutenda huduma. Waamuzi na watu wote wako tayari kufuata amri zako.”
Migawanyo ya makuhani na Walawi iko tayari kwa ajili ya kazi yote katika Hekalu la Mungu, naye kila mtu mwenye moyo wa kupenda mwenye ustadi katika aina yoyote ya ufundi atakusaidia katika kazi yote. Maafisa na watu wote watatii kila agizo lako.”

< 1 Nyakati 28 >