< Sefania 3 >
1 Ole mji wa wadhalimu, waasi na waliotiwa unajisi!
2 Hautii mtu yeyote, haukubali maonyo. Haumtumaini Bwana, haukaribii karibu na Mungu wake.
3 Maafisa wake ni simba wangurumao, watawala wake ni mbwa mwitu wa jioni, ambao hawabakizi chochote kwa ajili ya asubuhi.
4 Manabii wake ni wenye kiburi, ni wadanganyifu. Makuhani wake hunajisi patakatifu na kuihalifu sheria.
5 Bwana aliye ndani yake ni mwenye haki, hafanyi kosa. Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake, kila kukipambazuka huitimiza, bali mtu dhalimu hana aibu.
6 “Nimeyafutilia mbali mataifa, ngome zao zimebomolewa. Nimeziacha barabara ukiwa, hakuna anayepita humo. Miji yao imeharibiwa; hakuna mmoja atakayeachwa: hakuna hata mmoja.
7 Niliuambia huo mji, ‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’ Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali, wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake. Lakini walikuwa bado na shauku kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
8 Bwana anasema, “Kwa hiyo ningojee mimi, siku nitakayosimama kuteka nyara. Nimeamua kukusanya mataifa, kukusanya falme na kumimina ghadhabu yangu juu yao, hasira yangu kali yote. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wa hasira yangu.
9 “Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa, kwamba wote waweze kuliitia jina la Bwana na kumtumikia kwa pamoja.
10 Kutoka ngʼambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniabudu, watu wangu waliotawanyika, wataniletea sadaka.
11 Siku hiyo hutaaibishwa kwa ajili ya makosa yote ulionitendea, kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu wale wote wanaoshangilia katika kiburi chao. Kamwe hutajivuna tena katika kilima changu kitakatifu.
12 Lakini nitakuachia ndani yako wapole na wanyenyekevu, ambao wanatumaini jina la Bwana.
13 Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa; hawatasema uongo, wala udanganyifu hautakuwa katika vinywa vyao. Watakula na kulala wala hakuna yeyote atakayewaogopesha.”
14 Imba, ee Binti Sayuni; paza sauti, ee Israeli! Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee Binti Yerusalemu!
15 Bwana amekuondolea adhabu yako, amewarudisha nyuma adui zako. Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe; kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu, “Usiogope, ee Sayuni; usiiache mikono yako ilegee.
17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe, yeye ni mwenye nguvu kuokoa. Atakufurahia kwa furaha kubwa, atakutuliza kwa pendo lake, atakufurahia kwa kuimba.”
18 “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa nitaziondoa kwenu; hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
19 Wakati huo nitawashughulikia wote waliokudhulumu; nitaokoa vilema na kukusanya wale ambao wametawanywa. Nitawapa sifa na heshima katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
20 Wakati huo nitawakusanya; wakati huo nitawaleta nyumbani. Nitawapa sifa na heshima miongoni mwa mataifa yote ya dunia wakati nitakapowarudishia mateka yenu mbele ya macho yenu hasa,” asema Bwana.