< Zekaria 6 >
1 Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba!
Kisha nikageuka na kuinua macho na nikaona vibandawazi vinne vya farasi vikija kutoka kati ya milima miwili; na milima hiyo ilikuwa imetengenezwa kwa shaba.
2 Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi,
Kibandawazi cha kwanza kilikuwa na farasi wekundu, kibandawazi cha pili kilikuwa na farasi weusi,
3 la tatu lilivutwa na farasi weupe na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu.
kibandawazi cha tatu kilikuwa na farasi weupe, na kibandawazi cha nne kilikuwa na farasi wa kijivu.
4 Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani bwana wangu?”
Hivyo nikamwuliza malaika aliyesema nami, “Ni vitu gani hivi bwana wangu?”
5 Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake.
Malaika akajibu na kuniambia, “Hizi ni pepo nne za mbinguni zisimamazo mbele ya Bwana wa dunia yote.
6 Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.”
Lenye farasi weusi linakwenda nchi ya kaskazini; farasi weupe wanakwenda nchi ya magharibi; na farasi wa kijivu wanakwenda nchi ya kusini.”
7 Wakati hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote.
Farasi hawa wenye nguvu walitoka na wanatafuta kwenda na kuzunguka juu ya nchi, hivyo malaika akasema, “Nendeni na mzunguke juu ya nchi!” nao wakaenda juu ya dunia yote.
8 Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaokwenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho yangu katika nchi ya kaskazini.”
Kisha akaniita na kuniambia, “Tazama wale wanaokwenda nchi ya kaskazini, wataituliza roho yangu juu nchi hiyo.”
9 Neno la Bwana likanijia kusema:
Hivyo neno la Yahwe likanijia kusema,
10 “Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku iyo hiyo nenda nyumbani kwa Yosia mwana wa Sefania.
“Chukua sadaka kutoka kwa waliohamishwa - kutoka kwa Helidai, Tobiya na Yedaya - leo hii uende na kuipeleka katika nyumba ya Yosia mwana wa Zefania, aliyetoka Babeli.
11 Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uiweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki.
Kisha uchukue fedha na dhahabu, ufanye taji na uivike katika kichwa cha Yoshua mwana wa Yehosadaki kuhani mkuu.
12 Umwambie, hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Huyu ndiye mtu ambaye jina lake ni Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la Bwana.
Ongea naye na useme, Yahwe wa majeshi asema hivi: Mtu huyu, jina lake Tawi! Naye atakuwa alipo na kisha atajenga hekalu la Yahwe!
13 Ni yeye atakayejenga Hekalu la Bwana, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki katika kiti cha enzi naye atakuwa kuhani katika kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa amani kati ya hao wawili.’
Ndiye atakayejenga hekalu la Yahwe naye atauinua utukufu wake; kisha ataketi na kutawala katika kiti chake cha enzi. Atakuwa kuhani juu ya kiti cha enzi na ufahamu wa amani utakuwa kati ya vyote viwili.
14 Taji itatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la Bwana.
Taji itawekwa hekaluni mwa Yahwe kwa heshima ya Heldai, Tobiya na Yedaya na kama kumbukumbu ya ukarimu wa mwana wa Zefania.
15 Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la Bwana, nanyi mtajua ya kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii Bwana Mungu wenu kwa bidii.”
Ndipo waliombali watakapokuja na kulijenga hekalu la Yahwe, hivyo mtajua kuwa Yahwe wa majeshi amenituma kwenu; kwani ikiwa kweli mnaisikiliza sauti ya Yahwe Mungu wenu hili litatendeka!”